Ndugu zangu,
Jioni hii kupitia runinga nilimsikia
Profesa Costa Mahalu, Mwenyekiti wa Tume ndogo ya Bunge Maalum kwa kazi
ya kuandaa rasimu ya kanuni akitamka, kuwa swali la ama kura ya faragha
(siri) au ya dhahiri ( wazi) wataachiwa Wabunge wenyewe waamue.
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo,
Mheshimiwa Kificho naye hakuficha kuonyesha kwa sura na hata kauli, juu
ya ugumu wa jambo hilo. Akatolea mfano wa mpira, kwamba sasa uko kwa
Wabunge.
Kwa kuziangalia baadhi ya sura za
Wabunge wale, hakika ni vigumu kuwaonea wivu kwamba wamo ndani ya jengo
lile. Wana wakati mgumu, maana, umma nao unawaangalia.
Naam, nimepata kuandika, kuwa Afrika
safari zetu nyingi ni za bure tu. Na nyongeza hapa, ni kuwa , safari
zetu nyingine Afrika huanza na njia panda. Kwamba unapoianza tu safari
unakutana na njia panda.
Na ni kwenye njia panda ndipo
mwanadamu unatakiwa utumie hekima na busara. Njia panda inakutaka
ufikiri kwa makini. Maana, ukichagua njia kwa makosa, basi, safari yako
itakuwa ni ya mwelekeo mwingine. Si kule ulikotaka kwenda. Na kazi ya
kuirudia njia sahihi huwa ni ngumu sana.
Jioni hii pia nimesoma tena baadhi ya
vifungu vya Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba. Kwa mara ya kwanza
nimeipitia rasimu hii kwa masikitiko, maana, mbali ya kwamba ina mambo
mengi sana mazuri kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake, kwa kizazi
hiki na vijavyo, nahofia, kuwa kinachoendelea Dodoma, ambapo, ni
dhahiri, kuwa zinaonekana dalili za mijadala kutawaliwa na ushabiki wa
vyama kuliko wa nchi na mustakabali wake. Ni dalili za kuwa njia panda
na pengine tumeshaanza kuifuata njia isiyo sahihi. Kwamba tunapotea kama
Taifa.
Na ninaposoma rasimu ya Katiba ya Tume
ya Jaji Warioba na kupitia vifungu kama kile cha Sura ya Tisa,
kinachohusu Bunge la Muungano, sehemu ya Kwanza, Ibara ya 113 kifungu
cha 3 kinachosema;
" Katika kila Jimbo la Uchaguzi kutakuwa na nafasi mbili za Ubunge, moja kwa ajili ya mwanamke na moja kwa ajili ya mwanamme."
Kabla ya hapo wanawake wengi waliingia
Bungeni kwa njia ya Viti Maalum. Kwa rasimu hii ya Katiba, wanawake
watapata nafasi ya kushindana wenyewe kwenye majukwaa ya uchaguzi. Ni
maendeleo ya kidemokrasia.
Najiuliza, hivi ni kwa nini Tume ya
Jaji Warioba hawakuandaa Plan B kwa maana ya mpango 'B' . Na plan B hapa
ingelikuwa ni kuandaa mazingira, kuwa endapo rasimu hii ya Katiba
itakwama, basi, yale yote mazuri yaliyomo kwenye rasimu na
yanayokubaliwa na pande zote, na yenye kuweza kuhamishiwa kwenye Katiba
ya sasa bila kusababisha matatizo, basi, yangefanyiwa utaratibu wa
kuingizwa, kwa maana ya kuifanyia marekebisho ya ' dharura' Katiba
iliyopo. Najaribu kufikiri tu, kwa uhuru.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)
No comments:
Post a Comment