- Nafasi yake ni kubwa zaidi ya Tume, muhimu kuliko kura za maoni
BUNGE Maalumu la Katiba (constituent
assembly) ni chombo mahsusi cha wananchi cha kutunga Katiba yao. Katika falsafa
za kisiasa na kikatiba, wananchi ndiyo wenye mamlaka (sovereign power) na kwa
kutumia mamlaka yao wananchi ndiyo huunda chombo chao cha kujadili na kupitisha
Katiba. Ndiyo maana, nchi nyingi duniani, hutumia Bunge Maalumu na kura ya
maoni kujiwekea Katiba za nchi zao. Bunge Maalumu la Katiba ni kielelezo cha
mamlaka ya wananchi. Kwa hivyo, kiuhalisia, wajumbe wa Bunge Maalumu wanatakiwa
kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika Uchaguzi Mkuu. Kazi ya Bunge
Maalumu ni moja tu: kutunga Katiba na baada ya hapo uhai wake unamalizika.
Kwa kuwa wananchi hawawezi kukutana
wote kujadili kwa pamoja Katiba yao, wananchi kwa hiari yao wanawachagua
wajumbe wao kukaa, kujadili na kuwatungia Katiba na hatimaye wananchi
wanakubali au kukataa Katiba iliyopitishwa na Bunge lao katika kura ya maoni.
Kwa hiyo, Bunge la Katiba linakuwa na madaraka makubwa kuliko hata Bunge la
kawaida kwa sababu mamlaka na madaraka ya Bunge la Katiba yanatokana na
wananchi moja kwa moja. Hii ni dhana ya Bunge Maalumu. Katika hali halisi,
mambo yanakuwa tofauti.
Mchakato wa kutunga Katiba unaweza kuwa
tofauti kutokana na hali halisi na mazingira ya kisiasa ya nchi inayohusika. Na
wajumbe wa Bunge Maalumu pia wanaweza wakachaguliwa moja kwa moja au
kuchaguliwa kupitia vyombo vingine. Katika historia ya nchi yetu, hatujawahi
kuwa na Bunge Maalumu lililochaguliwa na wananchi moja kwa moja. Bunge Maalumu
la kwanza katika Tanganyika lilikuwa mwaka 1962 lililopitisha Katiba ya Jamhuri
ya Tanganyika. Bunge la kawaida (National Assembly) lilipitisha sheria ya
kujigeuza kuwa Bunge Maalumu. Hata hivyo, ili kuthibitisha kazi na mamlaka
yake, Katiba na sheria zingine zilizopitishwa na Bunge Maalumu hazikuwasilishwa
kwa Gavana kwa ajili ya kupata idhini yake kama zilivyokuwa taratibu za
kupitisha sheria wakati ule.
Bunge Maalumu la Katiba la pili
lilikuwa mwaka 1977. Kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Rais, Mwalimu Julius
Nyerere, na Mkataba wa Muungano (Articles of Union), Mwalimu, kwa makubaliano
na Rais wa Zanzibar, aliunda Bunge Maalumu la Katiba lililopitisha Katiba ya
1977, ambayo ni Katiba tuliyonayo. Ni kweli kwamba wajumbe walioteuliwa na rais
kuingia katika Bunge Maalumu wote walikuwa wabunge, theluthi moja wakiwa kutoka
Zanzibar na theluthi mbili kutoka Bara. Lakini hawakuingia katika Bunge Maalumu
kwa nyadhifa zao za kibunge bali kwa kuteuliwa na Rais, chini ya mamlaka
aliyopewa na Mkataba wa Muungano.
Pia kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano
kulikuwa na Tume ya Katiba. Watu ishirini, 10 kutoka Bara na 10 kutoka
Zanzibar, walioandaa katiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ndiyo waligeuzwa kuwa
wajumbe wa Tume ya Katiba ya Muungano. CCM kupitia Tume hii ilitoa maelekezo
kwa Wizara ya Sheria kuandika Rasimu ya Katiba. Waziri wa Sheria alikuwa Mama
Julie Manning na Joseph Sinde Warioba alikuwa Mwanasheria Mkuu. Niongeze pia
kwamba katibu wa Tume alikuwa Pius Msekwa na Mwenyekiti Mzee Thabit Kombo
(marehemu).
Pamoja na kwamba mchakato unaweza
kutofautiana na hata upatikanaji wa wajumbe wa Bunge Maalumu, bado kidhana
hadhi na mamlaka ya Bunge Maalumu yanabaki pale pale, kama kielelezo cha
mamlaka ya wananchi. Dhana hii ya Bunge Maalumu ilieleweka kwa ufasaha
mkubwa nyakati zile. Marehemu Edward Sokoine, ambaye alikuwa Waziri Mkuu,
alielezea vizuri wakati akiwasilisha rasimu/mapendekezo mbele ya Bunge Maalumu.
Namnukuu: “Katiba ya nchi ndiyo sheria
ya msingi kabisa kwa taifa lolote, na chombo kinachotunga sheria hiyo ni lazima
kiwe ni chombo chenye madaraka makubwa kabisa. Kwa hiyo, Bunge hili Maalumu
lina madaraka kuliko Bunge la kawaida. Bunge hili linaweza kukataa au kukubali
mapendekezo haya.
“Lakini Ndugu Spika, katika kutumia
madaraka yetu ni lazima tujue mipaka ya madaraka hayo. Mapendekezo
tutakayofikiria hivi sasa yametokana na maagizo ya Chama. Kwa busara yetu
Watanzania tumeamua, na bila kusita, kwamba Chama kitashika hatamu za uongozi
nchini. Kwa hiyo Bunge hili linaweza kabisa kuyakataa ama kuyabadilisha
mapendekezo ya Serikali iwapo litaona kuwa yanapinga maagizo ya Chama. Na iwapo
mapendekezo yote yanayopendekezwa yanatekeleza maagizo ya Chama naomba Bunge
lisione uzito wa kuyapokea na kuyapitisha bila kusita. (Makofi.)
Pamoja na ukweli kwamba enzi zile
zilikuwa enzi za chama kimoja, na chama kushika hatamu, Sokoine hakutafuna
maneno yake au kupinda dhana ya Bunge Maalumu. Alichokuwa anawakumbusha wajumbe
ni kwamba wao wote walikuwa wanachama wa CCM na walikuwa wanabanwa na uamuzi wa
chama chao. Kwa mantiki hiyo, mipaka ya madaraka ya Bunge Maalumu hayakutokana
na nyadhifa zao kama wajumbe, bali ilitokana na uanachama wao.
Kwa sababu zisizoeleweka, katika
mchakato wetu wa sasa, dhana na maana ya Bunge Maalumu imepotoshwa sana na
baadhi ya wasomi na wasemaji. Jaji Warioba katika hotuba yake aliyoitoa katika
mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania amejenga hoja kama
ifuatavyo:
“Madaraka ya Bunge Maalumu yanakuwa na mipaka
endapo Rasimu ya Katiba imeandaliwa na Tume ya Maadiliko (sic!) ya Katiba au
chombo cha aina hiyo. Bunge Maalumu linaweza kuwa huru kurekebisha baadhi ya
masharti yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba, lakini si suala la kawaida Bunge
Maalumu kubadili hoja ya msingi. Jinsi ushirikishaji wa wananchi unavyokuwa wa
wazi na mpana ndivyo madaraka ya Bunge Maalumu yanavyopungua. Mantiki ni kuzuia
Bunge Maalumu kunyang’anya madaraka ya wananchi, yaani “act of popular
sovereignty”. Watalaamu wa masuala ya Katiba, wanaeleza kuwa madaraka ya Bunge
Maalumu katika mazingira haya ni kuboresha Rasimu ya Katiba.
“Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba
sharti zizingatie kwamba Bunge Maalumu, kwa mujibu wa madaraka liliyopewa chini
ya kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura ya 83, ni chombo
cha kuboresha masharti ya Rasimu ya Katiba.
“Katika kutekeleza madaraka ya kujadili
na kupitisha masharti ya kikatiba, Bunge Maalumu litazingatia msingi kwamba
masharti ya kikatiba ndani ya Rasimu ya Katiba ni taswira, dira na ndoto za
wananchi ambazo zimeelezwa kupitia maoni ya mwananchi mmoja mmoja na makundi ya
wananchi kupitia asasi, taasisi, jumuiya na makundi ya watu wenye malengo
yanayofanana.
“Bunge Maalumu litafanya kazi ya
kuboresha masharti ya kikatiba yailiyomo ndani ya Rasimu ya Katiba pasipo
kuweka masharti mapya ambayo kwa taathira yake yanabadilisha au kufifisha
masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba. (uk. 10-11).”mwisho wa
kunukuu.
Tunaweza tukajumlisha hoja kuu za Jaji
Warioba kama ifuatavyo:
Mosi, madaraka ya Bunge Maalumu
kubadilisha misingi mikuu ya rasimu au la inategemea nani aliandika rasimu.
Kama Bunge lenyewe limeandika rasimu, Bunge lina madaraka hayo, lakini kama
rasimu imeandaliwa na ‘Tume ya Mabadiliko ya Katiba au Chombo cha aina hiyo’,
Bunge Maalumu linaweza kuirekebisha na kuiboresha, lakini sio kuibadilisha
misingi yake.
Pili, hoja hii inatokana na ukweli
kwamba wananchi wameshiriki kutoa maoni yao yaliyowekwa katika rasimu. Bunge
likibadilisha misingi itakuwa sawa na kunyang’anya ‘madaraka ya wananchi, yaani
“act of popular sovereignty”. Hii maana yake halisi ni kwamba utolewaji wa
maoni mbele ya rasimu ilikuwa “act of popular sovereignty” ya wananchi; maoni
yao ni kielelezo cha mamlaka yao.
Tatu, hoja hizi kuu ni kwa mujibu wa
(a) ‘Wataalam wa masuala ya Katiba’; na (b) kifungu cha 25(1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83.
Kutokana na hoja hizi za Jaji Warioba,
anatoa maelekezo kwamba kanuni za Bunge Maalumu zitakazotungwa na Bunge Maalumu
lenyewe ‘sharti zizingatie kwamba Bunge Maalumu… ni chombo cha kuboresha
masharti ya Rasimu ya Katiba.’
Hatuna budi tuchambue hoja hizi moja
baada ya nyingine kama ifuatavyo.
Madaraka ya Bunge kutegemea mchakato
Kama nilivyoeleza hapo juu, historia ya
dhana ya Bunge Maalumu (Constituent Assembly) inasisitiza kwamba Bunge Maalumu
ni mwakilishi wa mamalaka (sovereignty) ya watu. Kujitungia Katiba yao ni kwa
mujibu wa mamlaka (sovereignty) ya watu. Kwa kuwa mamilioni ya wananchi
hawawezi kukaa chini ya mti na kujadili na kuandika Katiba yao, wao wanachagua
wajumbe wao na wanawatuma kufanya kazi moja ya kuwatungia Katiba.
Rasimu yenyewe ya Katiba inaweza
kuandikwa na kamati iliyoteuliwa na Bunge lenyewe (kama ilivyokuwa India wakati
wa kuandika Katiba yao ya 1950) au rasimu inaweza kuandaliwa na kuandikwa na
Tume (kama ilivyokuwa Uganda wakati wa kuandika Katiba yao ya 1995). Lakini hii
haibadilishi dhana na maana ya Bunge Maalumu au kuweka mipaka ya madaraka ya
Bunge Maalumu. Katika mifano hii yote miwili, Bunge Maalumu lilibadilisha mambo
makubwa katika rasimu. Ukweli ni kwamba, mchakato wa Uganda haukuwa na tofauti
kubwa sana na mchakato wetu.
Tume ya Katiba ya Uganda chini ya Jaji
Mkuu ilikusanya maoni na kuandaa rasimu pamoja na taarifa ya uchambuzi wa kina
(majuzuu matatu yenye kurasa zaidi ya 1,000). Lakini mikono ya Bunge Maalumu
haikufungwa na rasimu, bali lilijadili mambo mengi sana ya msingi kinyume
kabisa cha misingi ya rasimu. Kwa mfano, kulikuwa na sauti nzito kutoka kwa
wawakilishi wa Buganda ambao walitaka muundo wa shirikisho (federal structure)
badala ya muundo wa serikali moja (unitary state). Hata hivyo, hakuna yeyote
katika Bunge hili – na lilikuwa na wanasheria waliobobea pamoja na marehemu
Profesa Nabudere - waliopinga kwa msingi kwamba mjadala ule ulikuwa ni batili
kwa sababu ulikuwa unapingana na misingi ya rasimu. Kulikuwa pia na mjadala
mkali kuhusu mfumo wa vyama vingi badala ya mfumo wa vuguvugu yaani ‘movement
system’ uliopendekezwa na Tume. Vilevile, hakuna aliyepinga kwa msingi kwamba
mjadala ulikuwa kinyume cha sheria au taratibu kwa sababu rasimu iliandaliwa na
Tume kutokana na maoni ya wananchi. Isitoshe, pendekezo la Tume lililotokana na
maoni ya wananchi kuwa na ‘National State Council’ kusuluhisha migogoro kati ya
mihimili ya dola lilitupiliwa mbali na Bunge Maalumu, tena kwa sauti moja.
Kwa kujumuisha, ni wazi kwamba mchakato
wenyewe wa kuandika Rasimu ya Katiba unaweza kutofautiana kutokana na hali
halisi. Lakini mchakato haubadilishi mamlaka ya Bunge Maalumu au haiathiri
dhana yake kama chombo mahsusi cha wananchi.
Ingawa, kisiasa Bunge Maalumu
lililochaguliwa moja kwa moja na wananchi linakuwa na uhalali zaidi na hadhi ya
juu kabisa, katika hali halisi, kutokana na uwiano wa nguvu za kitabaka na
makundi katika jamii, wanaoingia katika Bunge Maalumu wanaweza wakapatikana kwa
njia mbalimbali, ikiwemo kuteuliwa, kama tutakavyoona hivi punde. Hata hivyo,
bila kujali nani ni wajumbe wa Bunge la Katiba, kisheria dhana na hadhi ya
Bunge Maalumu haibadiliki.
Kuhusu ushirikishaji wa watu kutoa maoni
Hoja hii ya Jaji Warioba kwa kweli ni
kuhalalisha pendekezo la Tume la serikali tatu, ambalo ndiyo msingi mkuu wa
rasimu. Hoja ni kwamba pendekezo hili limetokana na wananchi wenyewe. Niseme
tu, kwanza, pamoja na kazi nzito iliyofanywa na Tume, pamoja na kukusanya maoni
ya wananchi, hii haitoshi kunyang’anya wananchi mamlaka yao ambayo
wanayadhihirisha kupitia Bunge Maalumu. Tume kamwe haiwezi kuwa na hadhi
sawa au zaidi ya Bunge Maalumu. Tume sio mwakilishi wa wananchi, wala
haikuchaguliwa na wananchi, wala sio chombo cha kufanya uamuzi. Tume inatoa mapendekezo.
Mapendekezo yanaweza kukubaliwa au kutupiliwa mbali.
Kama kweli, jukumu la Bunge Maalumu ni
kuboresha tu au kurekebisha tu mapendekezo bila kubadili misingi yake, basi
hatukuwa na haja ya kuwa na Bunge lenyewe. Mapendekezo ya Tume yangeenda moja
kwa moja kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.
Pili, ukiangalia kwa makini takwimu
zilizotolewa na Tume yenyewe, wala sio sahihi kusema kwamba wananchi waliowengi
walitaka serikali tatu. Kwa jumla, waliotoa maoni mbele ya Tume ni watu 351,664
(angalia Jedwali 3, uk. 9) kati ya hao, 47,820 tu (asimilia 14) waligusia
muundo wa Muungano. Asilimia 86 wala hawakuzungumzia muundo wa Muungano kwa
maana ya serikali moja, mbili au tatu au Muungano wa Mkataba. Wao walikuwa na
mambo tofauti kabisa kuhusu maisha yao. Kati ya waliogusia muundo asilimia 30
walitaka serikali mbili, asilimia 37 walipendekeza serikali tatu na asilimia 25
walitaka Muungano wa Mkataba; asilimia nane walitaka serikali moja.
Kwa hivyo, waliopendekeza serikali tatu
ni theluthi moja tu ya waliogusia muundo wa Muungano, na ni asilimia tano tu ya
waliotoa maoni. Waliotaka serikali mbili na Muungano wa Mkataba ni asilimia 55,
yaani zaidi ya nusu ya waliotoa maoni juu ya muundo wa Muungano. Hata ukichanganya
waliotaka serikali moja na serikali mbili ni asilimia 38, inazidi kidogo wale
waliotaka serikali tatu. Kwa takwimu hizi za Tume yenyewe, utasemaje kwamba
serikali tatu ni chaguo la wananchi na ni ‘taswira, dira na ndoto za wananchi’?
Sidhani kama kuna haja ya kusema zaidi
juu ya hoja hii: haina mashiko wala ushahidi wa maana.
Kuhusu maoni ya wataalamu wa kikatiba
Jaji Warioba anadai kwamba wataalamu wa
masuala ya kikatiba wanaunga mkono kwamba Bunge Maalumu lina mipaka ikiwa
mchakato umefuata kuwa na Tume ya kuandaa rasimu. Bahati mbaya hakutaja majina
yao wala kunukuu maandishi yao. Kwa hivyo ni vigumu kujua hao wataalamu ni nani
na walisema nini na katika muktadha upi.
Kuhusu kifungu cha 25(1) ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba
Inadaiwa na Jaji Warioba na wengine
kwamba kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imeweka mipaka ya
madaraka ya Bunge Maalumu. Kifungu hiki kwa lugha ya Kiswahili kinasema: “25(1)
Bunge Maalumu litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba
inayopendekezwa … .”
Kwa mujibu wa kifungu hiki Bunge
Maalumu lina uwezo wa kwanza; kujadili na pili; kupitisha. Kifungu hiki
hakisemi kwamba baada ya kujadili masharti ya rasimu, Bunge halina mamlaka ya
kuyabadili. Yaani maana sahihi ni kwamba baada ya kujadili Bunge (a) linaweza
kupitisha masharti haya kama yalivyo; au (b) kubadili, na kuyapitisha
mabadiliko. Hakuna popote pale neno ‘kuboresha’ limetumika. Kama kweli, nia
ilikuwa ni kulipa Bunge mamlaka ya kuboresha au kurekebisha tu sheria ingesema
hivyo. Kuna mantiki gani ya kujadili kama huna uwezo wa kuibadili au hata
kuitupilia mbali?
Kifungu 25(1) cha Kiingereza kimeliweka
jambo hili wazi zaidi: kwamba; “The Constituent Assembly shall have and
exercise powers to make provisions for the New Constitution of the United
Republic of Tanzania … .”
Maana ya ibara hii ni wazi kabisa.
Bunge Maalumu ndicho chombo kinachoweka masharti ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya
Muungano. Inaelekea tafsiri ya Kiswahili ni mbaya lakini mantiki yake ni ileile
ya yale yanayoelezwa katika kifungu cha Kiingereza.
Kwa kuhitimisha, ni wazi kabisa kwamba
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haikuweka mipaka ya mamlaka ya Bunge Maalumu
kama invyodaiwa. Na isingeweza kufanya hivyo kwa sababu sheria yenyewe
ilipitishwa na Bunge la kawaida, tena sio kwa theluthi mbili, ambayo ingeipa
sheria ya mabadiliko hadhi ya sheria ya kikatiba (constitutional act). Na
hatimaye pendekezo (proposed constitution) la Bunge Maalumu halirudi kwa Bunge
la kawaida bali linapelekwa moja kwa moja kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni.
Kwa hivyo, wananchi watalipigia kura pendekezo la Bunge Maalumu na sio rasimu
ya Tume. Rasimu ya Tume itakuwa na
nafasi ya kihistoria tu, sio ya nguvu za
kisheria.
Nafasi ya Bunge Maalumu ni ya kipekee
kabisa katika mchakato wa kutunga Katiba Mpya. Nafasi yake ni nzito kuliko ile
ya Tume na muhimu kuliko kura ya maoni. Hii ni kwa sababu Bunge Maalumu ndicho
chombo cha kufanya uamuzi mzito, sio Tume. Bunge ndilo litapitia rasimu ibara
kwa ibara, kufanya uchambuzi, kutathmini athari zake kwa taifa, kuhakikisha
kwamba hakuna migongano katika ibara, kuangalia kwa undani mfumo na muundo
unaopendekezwa unatekelezeka au hapana na, muhimu kuliko yote, mfumo
unaopendekezwa utaimarisha utulivu, amani na umoja wa nchi (national and
territorial integrity) au utazaa vurugu, migogoro na hatimaye uvunjaji wa nchi.
Ndiyo maana, wachache wetu
tulipendekeza tuwe na Bunge Maalumu la kuchaguliwa na wananchi moja kwa moja.
Lakini watawala wetu, pamoja na watawala watarajiwa na wengi wa wanaharakati,
katika busara zao na kwa maslahi yao, hawakutilia maanani pendekezo letu.
Tumepoteza nafasi ya kipekee ya kihistoria ya kuwa na Bunge Maalumu la
kuchaguliwa, jambo ambalo limetufikisha hapa tulipo.
Tufanye lolote linalowezekana pamoja na
kuibua mijadala na uelewa miongoni mwa wananchi bila jazba za kichama. Hili ni
jukumu letu kama wasomi. Tusije tukavunja nchi yetu na kulisambaratisha taifa.
Historia na vizazi vijavyo havitatusamehe.
Source:www.raiamwema.co.tz-
Issa Shivji
No comments:
Post a Comment