Mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba tangu lianze
shughuli zake mjini Dodoma wiki iliyopita umeonyesha dalili za kuwapo
uwezekano mkubwa wa Bunge hilo kushindwa kutunga Katiba Mpya ambayo
wananchi wengi waliitarajia.
Hata kabla Bunge hilo halijamchagua Mwenyekiti wake wa kudumu na kuanza kazi ya msingi ya kujadili Rasimu ya Katiba, kuiboresha na hatimaye kutoa Rasimu ya mwisho itakayopelekwa kwa wananchi ili ipigiwe kura ya maoni, mijadala katika Bunge hilo imetekwa na misimamo mikali ya kisiasa na kiitikadi.
Badala ya kujadili hoja zilizotokana na mijadala
kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge iliyowasilishwa na Kamati ya Muda ya
Kanuni, wajumbe wengi walijikita katika kutetea misimamo ya vyama au
makundi yao na kuyakataa baadhi ya mapendekezo muhimu yaliyowasilishwa
na Kamati ya Kanuni.
Matarajio ya wananchi ni kwamba Bunge lijadili mapendekezo hayo kwa kuweka mbele masilahi mapana ya Taifa, kwa maana ya kupitisha kanuni hizo kulingana na uzito wa hoja zilizotolewa.
Mvutano huo katika Bunge hilo ni mwendelezo wa hali ya kutovumiliana tuliyoishuhudia wakati Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipokuwa likijadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.
Pamoja na Muswada huo kupitishwa na Bunge katika mazingira ya kisiasa na hatimaye kuwa sheria, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho baada ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kupelekwa bungeni kutokana na upungufu uliotokana na wabunge kuweka mbele itikadi na misimamo ya vyama vyao vya siasa.
Ni kutokana na mazingira kama hayo, tunadiriki kusema kwamba kama Bunge la Katiba linalokutana mjini Dodoma halitabadili mwelekeo na kutafuta mwafaka wa kitaifa badala ya wajumbe wake kushikilia misimamo ya vyama, tusitegee miujiza ya kupatikana Katiba Mpya itakayobeba ndoto, matakwa na maono ya wananchi.
Moja ya matatizo yanayochochea hali ya kutokuwapo maridhiano wakati wa mijadala ndani ya Bunge ni kila kambi kutaka kupata kila kitu, hivyo kushindwa kukubali ukweli kwamba katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya kuna kupata hili na kukosa lile.
Wasiwasi wetu ni kwamba yaliyotokea bungeni tangu wiki iliyopita sio tu yanatishia kutopatikana mwafaka kuhusu namna ya kumaliza tofauti zilizopo miongoni mwa kambi hizo, bali pia upatikanaji wa Katiba Mpya katika wakati uliopangwa.
Mbali na Bunge hilo kupoteza muda mwingi likijadili suala la wajumbe kuongezewa posho, kila kambi imeituhumu nyingine kwa kukwamisha mjadala wa Kanuni za Bunge kwa malengo ya kisiasa. Moja ya kanuni zilizolivuruga Bunge ni kama upigaji kura uwe wa siri au wa wazi.
Sisi tunadhani zinahitajika nguvu za ziada kulirudisha Bunge ndani ya mstari kama tunataka kupata Katiba itakayokubalika. Kuna msemo kwamba wengi wape, lakini wachache nao wasikilizwe. Maana ya msemo huo ni kwamba sio lazima walio wengi wakati wote wawe na maoni sahihi. Kuna wakati walio wachache nao huwa na maoni sahihi.
Kwa mfano, Tume ya Nyalali ilitoa ripoti iliyoonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania waliotoa maoni yao walitaka utawala wa chama kimoja, lakini Tume hiyo ilipendekeza uwapo wa vyama vingi vya siasa. Kama sote tunavyoshuhudia hivi sasa, mfumo wa vyama vingi uliotakiwa na wachache hatimaye ndiyo uliopitishwa.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment