Dodoma. Mwenyekiti Mteule wa
Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano wa kutumia
kura ya siri katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya Katiba.
Sitta aliyechaguliwa juzi kushika wadhifa huo,
alisema atashirikiana na kamati ya uongozi itakayoundwa ya wenyeviti wa
Kamati 15 za Bunge hilo na kamati ya ushauriano kupata jawabu la suala
hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani
kwake mjini Dodoma juzi, Sitta alisema: “Unajua kuna baadhi ya vifungu
na ibara za Rasimu ya Katiba ni vizuri vipigiwe kura ya wazi na vingine
ambavyo ni nyeti zaidi vipigiwe kura ya siri.”
Alisema si vizuri vifungu vyote vipigiwe kura sawa, yaani si lazima zote ziwe za siri au ziwe za wazi.
Alitoa mfano wa ibara inayosema kutakuwa na
Mahakama Kuu ya Tanzania na kusema: “Hatuwezi kushindana katika suala la
kuwapo kwa Mahakama na ni wazi kuwa jambo hilo mnaweza kupiga kura ya
wazi. Nasema hivyo kwa sababu Katiba yoyote lazima ionyeshe mihimili
yote ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.”
Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki alishinda kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika juzi
kwa kura 487 kati ya 563 (sawa na asilimia 85).
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki ambaye kaulimbiu
yake ni ‘kasi na viwango’, alisema vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba
vinavyoweka misingi ya Katiba, ni vizuri vikapigiwa kura ya siri.
“Unajua tuna viongozi wa dini na halitakuwa jambo
la busara kama tukizijua hisia zao. Kama wewe uko karibu na imamu au
askofu halafu anapiga kura ya wazi ya kutaka Serikali tatu wakati wewe
muumini unataka Serikali mbili ni wazi kuwa jambo hilo linaweza kuleta
hisia tofauti na kuwanyima watu haki na uhuru wa kuamua,” alisema Sitta.
Alitoa mfano wa Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba
inayozungumzia Serikali na muundo wa madaraka katika Jamhuri ya Muungano
na kufafanua kuwa katika sura hiyo atapendekeza ipigiwe kura ya siri.
Kuhusu suala hilo la muundo wa Serikali alisema:
“Kikubwa ni wajumbe kujenga hoja, hatuwezi kwenda na misimamo
isiyobadilika kwa sababu tunataka maridhiano. Nitatenda haki na nitatoa
muda mrefu zaidi kwa wajumbe kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo
zina uzito mkubwa kuliko sura nyingine ambazo ni za maelezo tu. Mfano
suala la haki za binadamu ambazo wote tunakubaliana nazo.”
Alisema wakati wa kujadili muundo wa Serikali
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifika, ataishauri kamati ya
uongozi, kutenga muda wa ziada katika suala hilo na mengine yenye utata.
Mwenyekiti huyo alisema suala la upigaji kura
linatakiwa kuamuliwa kwa busara na atatumia hekima zake na za wajumbe wa
Bunge hilo, kutatua mgogoro wa kura ya siri au ya wazi
Wakati wa kujadili rasimu ya kanuni za Bunge hilo, kulizuka
mvutano mkali katika vifungu vya 37 na 38 vinavyozungumzia aina ya kura
itakayopigwa wakati wa kufanya uamuzi na kulazimika kuviweka kando. CCM
kimekuwa kikinadi kura ya wazi kikisema ni ya haki huku wapinzani
wakitaka kura ya siri.
Hata hivyo, kamati ya muda iliyoandaa kanuni za
Bunge hilo, ilipendekeza kuwa Bunge Maalumu ndilo litakaloamua aina ya
kura itakayopigwa.
Akizungumzia suala hilo Sitta alisema: “Pamoja na
kuwapo kwa hali hiyo, lazima ifikie wakati tuamue. Hatuwezi kuwa na
kanuni ambazo hazielekezi namna ya kupiga kura kwa sababu upigaji wa
kura unaweza kuanza kufanyika wiki ya kwanza tu baada ya kuanza kujadili
Rasimu ya Katiba.”
Samia Makamu Mwenyekiti
Wakati huohuo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan jana alichaguliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti wa Bunge hilo baada ya kumshinda mpinzani wake, Amina
Abdallah Amour.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi, Dk
Thomas Kashililah alisema kati ya kura 523 zilizopigwa, Suluhu alipata
kura 390 sawa na asilimia 74.6, Amina kura 126 sawa na asilimia 24.1.
Kura saba ziliharibika.
Kukamilika kwa uchaguzi huo kunafungua milango kwa
Yahya Hamad Hamis kuapishwa kuwa Katibu wa Bunge la Katika na Dk Thomas
Kashililah kuwa Naibu Katibu kwa mujibu wa sheria.
Makatibu hao wataapishwa leo saa nne asubuhi na
Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ndogo ya Dodoma. Baada ya kuapishwa,
Katibu atawaapisha Sitta na Samia katika Ukumbi wa Bunge kuanzia saa 10
jioni leo.
Awali wakati wakijieleza Amina alizua gumzo baada
ya kueleza kuwa licha ya kuwa na watoto watano, ameachika na kwa sasa
hana mume.
“Mimi ni mama wa watoto watano, nina shahada ya
uzamili ya masuala ya fedha, nina stashahada ya sheria na nimefanya kazi
katika Benki ya Biashara kwa miaka 23 ila kwa bahati mbaya nimeachika,”
alisema na kusababisha wajumbe kuangua kicheko.
Baada ya kuchaguliwa, Suluhu alisema: “Nitafanya
naye (Sitta) kazi kwa ushirikiano na uadilifu mkubwa. Pia ninawaahidi
wajumbe wote kuwa nitawapa ushirikiano.”
Mbowe amuonya Sitta
Wakati huohuo; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtumia
salamu za pongezi Sitta huku akimtaka kuachana na masilahi ya chama
chake.
“Ningependa kutuma salamu kwa Samuel Sitta ambaye
amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, nataka aelewe
kuwa alichokabidhiwa ni majukumu si cheo,” alisema na kuongeza:
“Mamilioni ya Watanzania watakuwa wanamfuatilia na
kumtazama kwa makini mno... maana wananchi kwa sasa wanajua mchakato wa
Katiba Mpya umebeba matumaini ya Taifa lao kwa miaka 50 hadi 100 ijayoSOURCE: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment