Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba na
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza bungeni
Dodoma juzi. Picha na Emmanuel Herman.
Suala la utaratibu upigaji kura kwenye
Bunge la Katiba limeibua mjadala mkali na kugawa wajumbe kwa wale
wanaotaka kura ya wazi na wale wanaotaka kura ya siri.
Dodoma. Kwa muda wa takriban siku 16
sasa, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamekuwa katika njiapanda
kuhusu kupiga kura ya siri au ya wazi katika kupitisha vifungu vya
Rasimu ya Katiba.
Kiini cha mvutano huu ni hatua ya
wajumbe wengi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutetea kwa nguvu
zote, kura ya wazi huku makundi mengine yakitetea mfumo wa kura ya
siri.
Wajumbe wengi wa CCM wanadai kuwa
hakuna sababu ya kuwa na usiri katika upigaji kura huo na kwamba itakuwa
demokrasia zaidi kwa kupiga kura ya wazi ili kila mwananchi ajue nani
kapiga kura gani.
Wanachokitaka CCM sasa hakina tofauti
na kile alichokifanya Rais Daniel Arap Moi mwaka 1988 alipoamua
kuanzisha kura iliyojulikana kama 'Mlolongo Voting' au 'Mlolongo
System'.
Chini ya utaratibu huo, wapiga kura
walipanga foleni nyuma ya picha ya mgombea wanayemtaka na baadaye mtu
alikwenda na kuhesabu idadi ya watu waliosimama nyuma ya picha na
kuandika matokeo.
Utaratibu huo ulilaaniwa duniani kote
kwamba ulikuwa una lengo la kuwatisha wapigakura na ulikuwa ukibana
demokrasia katika taifa hilo ambalo wakati huo lilikuwa na watu milioni
20.
Kutokana na mfumo huo ambao uliwafunga
wapigakura kutokutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi
wanayemtaka kwa siri, ni asilimia 32 tu ya Wakenya waliojitokeza kupiga
kura.
Leo miaka 26 baadaye, CCM inatumia nguvu kubwa kutaka mfumo kama huo.
CCM wameanzisha jambo hili kwa staili tofauti, tena katika jambo zito na la maridhiano kama la kupata Katiba Mpya.
Kwa akili ya kawaida kabisa ambayo
haihitaji kuwa na Shahada ya Chuo Kikuu, mpango huo wa CCM, ni dalili za
woga na vitisho ili wajumbe wake wenye mtazamo tofauti, wafyate mkia
wasikiuke msimamo wa chama hicho.
Kwa wiki ya pili, imekuwa shida
kuuelewa msimamo huo wa CCM, ambao unaweza kuufananisha na kinyonga
ambaye hubadilikabadilika rangi kulingana na mazingira alipo.
Miaka 50 tangu Tanzania ijipatie uhuru
wake, nathubutu kusema Serikali ya CCM imeendesha mambo yake kwa usiri
mkubwa, lakini ghafla leo imebadilika inataka uwazi. Ina hofu gani?.
Nasema imeendesha mambo yake kwa usiri
mkubwa kwa sababu mikataba yote iliyoiletea nchi hii matatizo ikiwamo
ya rasilimali ya madini, imeingiwa kwa usiri mkubwa tena mingine nje ya
nchi.
Hata hivyo, leo linapokuja suala la
upigaji wa kura kupitisha katiba yetu, CCM 'wameokoka'; hawataki tena
usiri bali uwazi. Waswahili wanasema: "Fumbo mfumbie mjinga mwerevu
atagundua."
Tusidanganyane katika hili, CCM
wanataka kuwashughulikia wajumbe wao ambao watakwenda kinyume na
misimamo ya chama hicho ambayo tayari inafahamika kwa Watanzania wote.
Nani asiyejua kuwa viongozi wa CCM
wanatoka hata 'mapovu' midomoni kupinga kwa nguvu zote muundo wa
Serikali tatu, ambayo ndiyo mapendekezo ya Watanzania wengi.
Upo ushahidi wa wanachama
'walioshughulikiwa' na chama hicho kwa kile kinachodaiwa kutumia uhuru
wao kuweka wazi misimamo yao ya kukataa kuburuzwa na CCM katika suala
hilo.
Sawa, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ya mwaka 2013 pamoja na kanuni zinazopendekezwa zinatoa kinga kwa mjumbe
kwa kile atakachokisema ama kukifanya ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.
Ukweli ulio wazi ni kuwa CCM wana mbinu nyingi za kuwashughulikia wale wanatofautiana nao kimtizamo.
Kubwa linalofanyika ni kukata jina lake anapogombea urais, ubunge na hata udiwani.
CCM wanalazimisha kwa nguvu zote
utaratibu wa kura za wazi kwa kuwa ndani ya chama hicho, tayari kuna
mgawanyiko mkubwa kuhusu muundo wa Muungano.
Baadhi ya wajumbe tayari wameonyesha
misimamo ya kwenda kinyume na misimamo hiyo ya CCM. Walioamua kukitosa
chama hicho wana sababu moja tu; wanataka kusimama na wananchi wao.
CCM wafahamu kuwa hata wakitumia wingi wao ndani ya bunge hili.
Kama ni chama kinachojiamini kwamba
msimamo wake unakubalika ndani na nje ya Bunge hilo, kinahofia nini
ikitumika kura za siri? Kwa nini inageuka kinyonga katika baadhi ya
mambo?
Kama CCM wanaona wengi wanataka kura
ya wazi, basi ushauri wa Anne Kilango Malecela wa kupiga kura za siri
ili kuamua kama itumike kura za siri ama za wazi, ulikuwa mwafaka.
Kwa mwenendo huu wa CCM, nina mashaka
kama chama hicho kina dhamira ya dhati ya kuwapatia Watanzania, Katiba
bora na kwa wakati kwa sababu mvutano huu ukiendelea, Bunge linaweza
kuvunjika.
Sitashangaa, kama CCM watafurahia
kuvunjika kwa Bunge hili ili turudi kwenye muundo wa Serikali mbili
ambao wao ndio wanautaka kwa sababu tu ya masilahi yao na si masilahi ya
wananchi.
Hata hivyo, ikishindikana, wajumbe wa
CCM wafanye uamuzi mgumu hata kama ni kura ya wazi. Wapige kura ya wazi
kwa masilahi ya Watanzania kwa sababu wataingia kwenye vitabu vya
kumbukumbu.
CCM inaweza kufutika katika historia ya nchi hii, lakini Utanzania utadumu milele na milele.
Chanzo, mwananchi
No comments:
Post a Comment