WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 19, 2014

Kanuni zizingatiwe kulinda ustawi wa Bunge la Katiba

Katuni
Bunge  Maalum la Katiba lilikumbwa na dhoruba kali juzi. Hiyo ni baada ya kuibuka kwa mvutano mkali kuhusiana na utekelezaji wa kanuni inayoelezea uwasilishwaji wa rasimu ya katiba hiyo.
Baadhi ya wajumbe, hasa wasiokuwa wafuasi wa chama tawala walikuwa wakipinga vikali uamuzi wa kutaka kuwasilishwa kwa rasimu hiyo kabla ya uzinduzi wa Bunge uliotakiwa kufanywa na mgeni rasmi, Rais Jakaya Kikwete.

Hali haikuwa shwari hata kidogo. Kuna wajumbe walizomea vikali. Wengine walipiga meza. Na baadhi yao wakagumia huku wakionyesha wazi kuwa hawaridishwi na mwenendo wa Mwenyekiti wa Bunge katika kushughulikia suala hilo.

Tukio hilo lililjiri wakati Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipopewa fursa ya kuwasilisha rasimu ya katiba mpya mbele ya wajumbe.

Kinyume cha matarajio ya Watanzania wengi waliokuwa wakifuatilia shughuli za Bunge hilo, kazi hiyo ilishindwa kufanyika. Jaji Warioba pia akaonekana kupigwa butwaa, asiamini kile kilichokuwa kikitokea.

Akaishia kusimama tu kwa dakika takriban tano, mwishowe akalazimika kwenda kuketi baada ya Mwenyekiti wa Bunge kubaini kuwa hali iliyokuwapo isingeruhusu kuendelea kwa hatua hiyo ya uwasilishaji wa rasimu.

Wajumbe waliokuwa wakipinga, wengi wao wakiwa ni wale watokao katika vyama vya upinzani, walikuwa wakipaza sauti zao kwa nguvu, wakimtaka mwenyekiti wa Bunge kuzingatia kanuni.

Nguvu ya wapingaji ikashinda. Hatimaye kikao kikaahirishwa na rasimu ikalazimika kusomwa bungeni jana asubuhi, hiyo ikiwa ni baada ya kuafikiana kwa pande zilizokuwa zikisuguana juzi.

Chanzo cha malumbano ya juzi kilifahamika. Baadhi ya wajumbe walikuwa wakipinga kile walichoeleza kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa kanuni za Bunge, wakimshutumu mwenyekiti kuwa anawaburuza ili akidhi matakwa ya chama tawala.

Waliopinga uwasilishwaji juzi walidai kuwa hawako tayari kuona kanuni ya 7 (1) h ikivunjwa. Hii ni ile  inayoeleza namna ya uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba na kwa mujibu wa kanuni hiyo, hotuba ya ufunguzi ya mgeni rasmi inatakiwa ianze kabla ya uwasilishaji wa rasimu.

Kanuni hiyo ilitenguliwa kutokana na ombi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetumia kanuni nyingine ya 85, fasiri ya 4 (d), ili kumruhusu Jaji Warioba awasilishe rasimu kabla ya hotuba ya mgeni rasmi.

Ni hapo ndipo msuguano ulipoanza. Waliokuwa wakipinga, walisisitiza kuwa kanuni lazima ziheshimiwe. Jitihada za Mwenyekiti kuwazima ili kumpa nafasi Jaji Warioba ziligonga mwamba na ndipo kikao kikaahirishwa hadi jana asubuhi.

Siyo nia yetu kutaka kueleza ni upande gani ulio sahihi. Bali, NIPASHE tunadhani kwamba malumbano kama ya juzi, yenye mwelekeo wa hisia za vyama na makundi hayana tija kwa mustakabali wa taifa letu.

Kama kweli tunataka ndoto ya kupata katiba mpya inayokidhi matakwa ya Watanzania wengi iwe ya kweli, ni lazima wajumbe wa Bunge la Katiba wakazingatioa kanuni.

Kamwe, hatuamini hata kidogo kuwa maamuzi ya wajumbe katika kukamilisha mchakato huu wa kihistoria yataegemea misimamo ya vyama, makundi au utashi binafsi.

Isipokuwa, kama ilivyowahi kusisitizwa mara kadhaa na Rais Kikwete, wajumbe wataendelea kuweka mbele maslahi ya taifa.

Tukio kama la juzi halipaswi kupewa nafasi katika kipindi hiki ambacho Watanzania wengi wanatarajia kuona wawakilishi wao wakibishana kwa hoja ili kupata katiba.

Aidha, wajumbe watambue kuwa mafanikio ya mchakato huu yanategemea utayari wao katika kuzingatia kanuni. Kuzikiuka kwa namna yoyote ile kunahatarisha uhai wa Bunge.

Mwenyekiti na viongozi wengine wa Bunge Maalum la Katiba wanapaswa kutanguliza busara zaidi katika kila jambo ili kuepuka uwezekano wa kuwapo kwa baadhi ya wajumbe watakaojihisi kupuuzwa.

Wajumbe wakumbuike kuwa hatua waliyofikia sasa ni muhimu zaidi. Ni vyema wakazingatia kanuni walizojiwekea wenyewe ili kulinda uhai wa Bunge.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment