Rais Jakaya Kikwete jana alibadili upepo wa
mchakato mzima wa Katiba baada ya kutoa maoni yake binafsi, akitaka
muundo wa Serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ufunguzi wa Bunge Maalumu la
Katiba mjini Dodoma, Rais Kikwete alipangua hoja moja baada ya nyingine
zilizotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba wakati
akiwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni Machi 18, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo ya saa 2:49 iliyokuwa na
maneno ya ‘kuuma na kupuliza’ kuhusu yaliyomo katika Rasimu ya Katiba,
Rais Kikwete alisema suala la muundo wa Muungano ndiyo ajenda mama
katika Rasimu ya Katiba na kwamba iwapo wajumbe watatoa uamuzi usio
sahihi, nchi inaweza kujaa migogoro ambayo haikuwapo.
Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo,
Kikwete alisema kuwa wanaotaka Serikali tatu waangalie changamoto zake
na kuzitafutia majibu, kwa maelezo kuwa muundo huo unaweza kuvunjika
kirahisi.
Alisema ingawa Jaji Warioba aliwatoa hofu wananchi
kuwa Serikali tatu hazitakuwa na gharama kubwa, ukweli ni kwamba muundo
huo una gharama na utekelezaji wake ni mgumu na kusisitiza kuwa CCM
inaweza kuzimaliza kero za Muungano bila kuhitaji uwapo wa Serikali ya
tatu.
Huku akichambua kile kilichoelezwa na Jaji Warioba
sambamba na kuwapiga vijembe wenyeviti wa vyama vya upinzani akiwamo
Christopher Mtikila (DP) na Freeman Mbowe (Chadema), Rais Kikwete
alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa sababu mbili kubwa za
kupendekeza muundo wa Serikali tatu;
“Sababu ya kwanza ni kwamba muundo huo ndiyo
matakwa ya Watanzania wengi Bara na Zanzibar. Sababu ya pili muundo huo
unatoa majibu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa
wa Serikali mbili zinazolalamikiwa na pande zote mbili.”
Aliongeza, “Wapo wanaokubaliana na tume na kwamba
muundo wa Serikali tatu ni matakwa ya wengi na hauepukiki na kwa msemo
wa Kiswahili wengi wape. Lakini wapo wanaopingana na takwimu za tume
kwamba hazionyeshi ukweli huo. Mimi nasema maneno yanayosemwa na watu
siyo yangu.” Huku akishangiliwa na wajumbe wa Bunge hilo alisema, “Watu
wanasema Watanzania waliotoa maoni kwa tume ni 351,664, kati yao 47,820
sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano. Watu
303,844 sawa na asilimia 86.4 hawakuwa na tatizo na muundo wa Muungano
na wala hawakuuzungumzia wakati wa kutoa maoni.”
Alisema hivi sasa watu wanahoji iweje asilimia
13.6 ndiyo wageuke Watanzania walio wengi ambao wametoa maoni ya kutaka
Serikali tatu.
“Watu wanahoji mbona taarifa ya tume inayohusu
takwimu (ukurasa 66,67), inaonyesha kati ya watu 47,820 waliotoa maoni
kuhusu muungano watu 17,280 ndiyo waliotaka Serikali tatu ambao ni sawa
na asilimia 37.2 na waliotaka muundo wa Serikali mbili ni asilimia 29.8,
Serikali ya mkataba asilimia 25.3 na Serikali moja asilimia 7.7”
alisema. Alisema taarifa ya tume inaonyesha kuwa watu 772,211 waliotoa
maoni ni asilimia 10.4 ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na
asilimia 88.6 hawakuzungumzia Muungano, bali mambo mengine.
“Watu wanahoji kama Muungano ni jambo linalowakera
sana Watanzania ingethibitika kwenye wingi wa wale waliotoa hoja.
Usahihi wa hoja hii ni upi, nawaachie nyie (wajumbe) mjadili” alisema
huku akishangiliwa kwa nguvu.
Akizungumzia sababu ya pili ya tume kwamba muundo
wa Serikali tatu unajibu changamoto za muundo wa Serikali mbili, huku
akifafanua kero zinazotolewa na kila upande wa Muungano alisema; “Nyinyi
ndiyo waamuzi, sikilizeni vizuri hoja hizi mtafakari na kuamua. Tume
yenyewe imekiri kuwa muundo wa Serikali wa Serikali tatu una changamoto
zake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa shughuli za
umma.”
Alisema wajumbe wa Bunge hilo wanatakiwa kutafuta majibu mwafaka
kuhusu changamoto za muundo wa Serikali tatu kwa sababu maelezo ya tume
kuhusu muundo huo hayana majibu.
Aliongeza, “Kupanga ni kuchagua. Wanaounga mkono
Serikali mbili wanasema mlolongo wa changamoto ulioanishwa na tume
kuhusu Serikali tatu hautapunguza matatizo bali utayaongeza kuliko
ilivyo sasa na wanasema changamoto hizo zinatatulika bila kuwepo
Serikali ya tatu.”
Alisema kama mfumo wa Serikali tatu ukipita ni
lazima Serikali ya tatu ijengewe msingi imara kwa sababu haitakuwa na
chanzo cha uhakika cha mapato yake yatakayoiwezesha kusimama yenyewe na
haitakuwa na chombo cha kukusanya mapato zaidi ya kutegemea kukusanyiwa
mapato na nchi washirika.
“Kama tunataka Serikali ya tatu lazima
tuitengenezee misingi ya uhakika. Hivi nani atakudhamini kwa virungu,
pingu, magari ya kuwasha, majeshi au bunduki. Serikali hii ya tatu
haidhaminiki wala kukopesheka,” alisema huku akitolea mfano jinsi
mataifa kama Urusi yalivyoanguka baada ya kujitenga.
Huku akifafanua jinsi kero za muungano
zilivyotatuliwa na kamati na tume mbalimbali mpaka kubaki kero sita,
Rais Kikwete alisema Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar zimeamua
kutumia mchakato wa Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa
kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana
kulikuwa na mambo 11 ya muungano, baadaye kuongezeka hadi mambo 22 na
kusisitiza kuwa mambo mengi yaliibuka baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki mwaka 1977.
Alisema jambo ambalo Serikali hizo mbili walikubaliana kuliondoa katika mambo ya Muungano ni suala la gesi asilia na mafuta.
Ammwagia sifa Warioba
Alisema Jaji Warioba wa wajumbe wenzake wa Tume ya
Katiba wameandika Rasimu ya Katiba vizuri na kwa weledi wa hali ya juu,
na kwamba wametoa maoni ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na
kuboresha Katiba tuliyonayo sasa.
“Katiba inayopendekezwa imejumuisha dhana na mambo
kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tuliokuwa nao na kuweka
misingi mizuri kwa huko mbele tuendako,” alisema.
Alisema Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa
kilichosheheni mambo mengi kina kurasa 106, sura 17, hivyo wajumbe wa
Bunge la Katiba wanapaswa kusoma kila kitu na kuelewa na kuamua kwa
utashi wao.
“Uamuzi wako siyo uamuzi wa kuambiwa na mwenzako,
unaulizwa na wenzako kwenye hilo tusemeje unasema na mimi nimeambiwa,
ebo! Umeambiwa, umefundishwa na mimi nasema akili za kuambiwa…” alisema
Rais Kikwete.
Mambo mengine
Pia Rais Kikwete aligusia suala la mbunge kupoteza
ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi kwa miezi sita mfululizo, kutokana
na maradhi au kizuizi ndani ya gereza.
Alisema anaungana na wote wanasema jambo hilo liangaliwe vizuri na kwamba anashauri kama akiwa kizuizi amepatikana na makosa apelekwe mahakamani.
“Kwa mazoea ya duania ukomo unawekwa kwa wakuu wa nchi, hawaweki ukomo kwa wabunge, Tanzania wanataka kuwa wa kwanza,” alisema Kikwete.
Kuhusu suala la ugonjwa alisema mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wake, hivyo siyo sahihi kumwekea mgonjwa muda maalumu wa kuugua kwake.
Huku akicheka, Rais Kikwete alisema kitendo hicho
kitawafanya wabunge kuanza kutembea na dripu katika majimbo yao kabla
hawajapona vizuri.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment