Dodoma. Waziri wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta amechaguliwa kwa kishindo kuliongoza Bunge Maalumu la
Katiba, huku akisema kuchaguliwa kwake ni sawa na kumrudisha chura
kwenye dimbwi la maji.
Jana, Sitta ambaye pia ni Mbunge wa
Jimbo la Urambo Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata
kura 487 na kumbwaga mpinzani wake, Hashimu Rungwe wa Chama cha Ukombozi
wa Umma aliyepata kura 69.
Wajumbe wengine, Dk. Terezya Huvisa
pia wa CCM na John Chipaka wa Tadea, walijitoa katika kinyang'anyiro
hicho ambacho tangu awali Sitta alionyesha kujiandaa kwa kutengeneza
vipeperushi alivyovisambaza kwa wajumbe kama sehemu ya kujinadi.
Akizungumza na wajumbe ambao muda
mwingi walikuwa wakimshangilia, Sitta alionekana kujiamini kabla na
baada ya uchaguzi. Pia alitumia misemo lugha ya picha ikiwamo ya chura
kuishi majini, akimaanisha kuwa wajumbe wamemchagua mtu mwenye uwezo,
uzoefu na weledi wa kuongoza shughuli za Bunge.
"Jamani kunichagua mimi ni kama
kumrejesha chura kwenye dimbwi la maji alilolizoea. Msiwe na wasiwasi
ataogelea tu na ninawaahidi kuwa ikiwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu,
mtanichagua nitawatumikia kwa uaminifu, sitakubali upendeleo wa aina
yoyote, nitasimamia kanuni tulizozipitisha hapa," alisema.
Aliongeza kusema: "Nitawaongoza kwa
utumishi uliotukuka na uadilifu ili tupate Katiba bora, yenye viwango na
kwa wakati. Nina hulka ya kuwapenda wale ninaowaongoza, kwa hiyo
nitakuwa mtetezi wa shughuli mbalimbali...Ninawaahidi Watanzania kutenda
haki na kuwapatia Katiba yenye viwango na kwa wakati.
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, Sitta
alikuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akiongozwa na falsafa yake ya Bunge la kasi na viwango. Pia anatajwa
kufanikiwa kuliongoza Bunge hilo kwa weledi wa hali ya juu.
Kwa sababu ya mafanikio hayo, alipokuwa akiomba kura za wajumbe wa Bunge hilo, hakusita kujifananisha na chura kurudi majini.
Aidha, alisisitiza kuwa ataliongoza
Bunge kwa kutumia falsafa yake ya kasi na viwango, huku akiahidi
kulisimamia Bunge kwa haki na bila upendeleo kwa kundi lolote.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo, Msimamizi wa
Uchaguzi, Dk. Thomas Kashillilah, alisema Sitta alipata kura hizo 487
ambazo ni sawa na asimilia 86.5, kati ya kura 563 zilizopigwa.
Dk Kashillilah alisema kwamba mpinzani
wa Sittta, Hashim Rungwe ambaye jana tulimwandika kimakosa kuwa anatoka
NCCR- Mageuzi alipata kura 69, sawa na asilimia 12.3 ya kura zote.
Alisema kura saba ziliharibika.
Moja ya mambo yaliyovuta hisia za
wajumbe wengi ni hatua ya Sitta kushikana mikono ya kupongezana na
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya kumaliza kuomba kura
kutoka kwa wajumbe.
Sitta na Chenge
Akitoa shukurani zake baada ya
kuchaguliwa, Sitta alisema hana uhasama wowote na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge ambaye naye awali alikuwa na nia ya kuwania
nafasi hiyo kabla ya kujitoa.
"Namshukuru pia ndugu yangu Andrew
Chenge ambaye watu walivumisha kwamba tulikuwa na mchuano wa uhasama
ndani ya chama, jambo ambalo siyo kweli, "alisema na kuongeza;
"Mheshimiwa Andrew Chenge tuna
historia ndefu sana, nikiwa Waziri wa Katiba na Sheria mwaka 1993, mimi
ndiye niliyependekeza jina kwa Rais wa Awamu ya Pili, Rais Ali Hassan
Mwinyi ili ateuliwe kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali." alisema.
Kwa upande wake, Chenge alisema:
"Mambo yote yaliyozungumzwa na Sitta ni mambo yaliyopita, kilichopo ni
kutazama kazi iliyo mbele yetu.''
Nyongeza na Beatrice Moses, Dar es Salaam
chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment