WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 12, 2014

Kanuni zapita kwa kauli moja

 
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Rasimu ya Kanuni za Bunge, Profesa Costa Mahalu, akiwasilisha kanuni mbele ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kuzipitisha jana.PICHA: SELEMANI MPOCHI
Baada ya mvutano wa takribani wiki tatu, hatimaye Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, wameridhia Rasimu za Bunge hilo na sasa zinaanza kutumika rasmi kujadili Rasimu ya Katiba, lakini vifungu vya jinsi ya upigaji kura kwa ajili ya kupata uamuzi vitaamuliwa baadaye na wajumbe.
Akiwasilisha azimio la kutunga na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum bungeni jana, Mwenyetiki wa Kamati ya Muda ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni za Bunge Maalum, Profesa Costa Mahalu, alisema suala la aina ya upigaji wa kura kwa ajili ya kupata uamuzi bado linaendelea kushughulikiwa.

Alisema suala hilo litawekwa katika kanuni husika baada ya kuamuliwa, kama ambavyo bunge hilo litakavyoona inafaa.

Kanuni hizo zimetungwa chini ya kifungu cha 26(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, ambacho kinaelekeza Bunge Maalum litatunga kanuni kwa ajili ya kuendesha shughuli za Bunge Maalum.

Mvutano ulikuwa kwenye kanuni za 37 na 38 zinazozungumzia upigaji kura. Wakati  awali kanuni ya 37 inazungumzia utaratibu wa kufanya uamuzi kuwa ni kura, ile ya 38 inazungumzia namna ya kupiga kura ikisema wakati wa kupiga kura, kila mjumbe atapiga kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana’.

Fasili ya pili ya kanuni hiyo inasema utaratibu wa kupiga kura utakubaliwa na Bunge Maalum baada ya kupitishwa kwa kanuni hizo.

Baada ya kuwasilishwa kwa azimio hilo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Pandu Ameir Kificho, aliwapa nafasi wajumbe kadhaa kutoa kauli zao za kuunga mkono.

PROF. LIPUMBA

Profesa Ibrahimu Lipumba alisema wajumbe wengi baada ya kuvipitia vifungu vya kanuni hiyo wameridhika kuwa Kanuni za Bunge Maalum za 2014, ni nzuri.

Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa hata katika  utaratibu wa aina ya kupiga kura watakaoamua baadaye uzingatie kifungu cha 4(1) kinachosema, “takuwa na uhuru wa mawazo na maoni katika mijadala ya Bunge Maalum na maoni ya mjumbe hayatahojiwa mahakamani au sehemu yoyote nje ya Bunge Maalum.”

Akiunga mkono azimio hilo aliwataka wajumbe wenzake kuridhia kanuni hizo ili waweze kufanya kazi muhimu ya kujadili na hatimaye kuwapatia Watanzania katiba bora itakayowafaa kwa vizazi vingi vijavyo.

DK. MICHAEL
Dk. Francis Michael, ambaye ni mwenyekiti wa wajumbe 201 walioteuliwa, aliipongeza Kamati ya Profesa Mahalu kwa kazi nzuri waliyoifanya.

“Tunaunga mkono kanuni hizi kwa sababu wananchi wanatutegemea kuwapelekea katiba nzuri,” alisema.

MHAGAMA

Naye Jenista Mhagama alisema: “Kanuni zimeandaliwa kwa weledi wa hali ya juu kwa kuzingatia maslahi ya taifa letu.”

Alisema baada ya kuridhiwa kwa kanuni hizo, wajumbe wanaanza safari yao kwa umoja na maridhiano ya hali ya juu.

MUSTAPHA
 Idrisa Kitwana Mustapha alisema: “Watanzania wanategemea tuwafanyie mambo makubwa. Katiba hii siyo yetu peke yetu ni ya Watanzania zaidi ya milioni 45. Kwa hiyo, maamuzi yetu yatawapa Watanzania moyo na matumaini wanayotarajia, niko chini ya miguu yao naomba wajumbe tuiunge mkono Kanuni hii,” alisema.

MBATIA
James Mbatia alisema hatua iliyofikiwa ni kubwa kwa taifa na Tanzania imeingia katika historia ya ulimwengu kwa kutumia wiki tatu tu kutunga kanuni ikilinganishwa na mataifa mengine.

“Tumeonyesha mshikamano na umoja tulionao… ni kweli hatuwezi kuridhiana wote, lakini katika hili tumeonyesha umoja wetu umeimarika,” alisema.
 
PANYA ALLY ABDALLAH

Panya Ally Abdallah aliishukuru Kamati ya Profesa Mahalu kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya na kwamba hiyo inatokana na mapenzi mazuri waliyonayo ya kuwaletea Watanzania katiba nzuri.

 FREDERICK MSIGALA

 “Kazi za Kamati ya Profesa Mahalu imekuwa nzuri sana na mambo mengi tuliyowapa wamezingatia,” alisema.

VUAI ALLY VUAI

“Naona wajumbe wote walioitwa kuzungumza wameunga mkono hoja hii na wameongea mambo mazuri, nami sina zaidi naunga mkono hoja iliyoletwa mbele yetu,” alisema.

ANNA ABDALLAH
Alitumia methali: “Usione vyaelea vimeundwa.”“Naomba niwathibitishie baadhi ya Watanzania wenzangu waliokukwa wakituona tupo hapa tunapoteza muda tu na kula posho. Tulikuwa tunaunda chombo hiki (Kanuni) ya namna ya kuendesha Bunge Maalum la Katiba, litakalotupatia Katiba ya mwisho ambayo itapelekwa kwa wananchi kupigiwa kura,” alisema.

SHEIKH KUNDECHA
Alisema anaamini tofauti kati ya binadamu haziwezi kukosekana, lakini jambo la msingi hapo ni kuwa na busara ya kuona watu wanaungana na kuafikiana kwa mwafaka.

MBOWE

Alisema jana ilikuwa siku ya majadiliano mengi yaliyoonyesha uvumilivu mkubwa.

Alisema awali ukumbi huo wa bunge ulikuwa umejaa mapepo, lakini akamshukuru mjumbe Joseph Selasini kwa kuwasilisha ombi la kuanza vikao vya bunge hilo kwa sala.
Alisema kutokana na maombi ya sala za viongozi hao wajumbe wenye mapepo wameshindwa na kulegea na sasa wanaendelea kuvumiliana.
JUSSA
Alizungumzia kazi ya kuandaa kanuni hizo kwa niaba ya wajumbe wa kamati ya kuandaa kanuni na kusisitiza kuwa haikuwa kazi nyepesi na kwamba kuna wakati walikuwa wakimuonea huruma Kificho.

“Profesa Mahalu ametuongoza vema, haikuwa kazi nyepesi hata kidogo kukubaliana kwenye kamati kama ambavyo watu wengi wanavyofikiri…wakati fulani ilikuwa ngumu sana kuvumiliana,” alisema.

Alipongeza pia mjumbe mwenzake wa kamati hiyo, Tundu Lissu kwa ‘utundu’ mkubwa alionao wa kusoma na kutumia yale aliyoyasoma katika utekelezaji.
Aidha aliwatoa hofu Wazanzibari kuwa kanuni hizo zimehakikisha katika kila hatua ya maamuzi theluthi mbili zinazingatiwa na hawatafanya chochote katika bunge hilo bila kuzingatia maslahi ya Zanzibar.
ASKOFU MHAGACHI

Alisema Kanuni hizo zitawasaidia wajumbe na Watanzania kupata katiba nzuri wanayoitaka.

Akinukuu msemo wa mwanafalsafa mmoja, ambaye alisema, ‘Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako’ na kwamba maridhiano waliyofikia yanaonyesha wana nia ya kwenda mbali na siyo haraka.

Baada ya wajumbe hao  kumaliza kuunga mkono hoja hiyo, Mwenyekiti wa Muda Kificho aliwauliza kwa sauti wajumbe kwa kutaka wajibu ‘ndiyo’ au ‘hapana’ iwapo wanaridhia Kanuni za Bunge Maalum za mwaka 2014, na walipojibu, alisema, ‘sauti za waliosema ndiyo wameshinda.’

MTIKILA, MKOSAMALI WAZUA MAPYA

Hata hivyo, wajumbe wawili, Mchungaji Christopher Mtikila, na Felix Mkosamali, kwa nyakati tofauti walitaka kuchafua hali ya hewa, baada ya kusimama bila kufuata utaratibu bungeni na kuanza kumkaripia Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho, wakilalamika kunyimwa nafasi ya kuzungumza na Bunge kupitisha kwa hila azimio la kuridhia kanuni mbovu.

 Bila kuruhusiwa na kiti, Mtikila alisimama na kuwasha kipaza sauti na kuanza kuhoji sababu za kuzuiwa kuzungumza bungeni na kama hana haki ya kuzungumza au la. Alitaka ajibiwe na Kificho kama mambo anayotaka kuzungumza hayawezi kuibariki nchi.

Mtikila alisema kuzungumza bungeni ni haki yake na siyo kwa mapenzi ya Kificho.

Alimtaka Kificho aeleze kama anamheshimu Mungu kwa kuwa neno “haki” ni msamiati, ambao umekuwa ukizungumzwa mara nyingi bungeni na kwamba, katika msahafu limeelezewa kuwa ni sehemu ya ufalme wa Mungu.

Wakati wote Mtikila alipokuwa akizungumza Kificho alibaki akiwa ameduwaa, huku ukumbi mzima wa Bunge ukiwa kimya wakimsikiliza.

Mtikila alitoa malalamiko hayo muda mfupi, baada ya Kificho kumkaribisha Profesa Mahalu, kutoa hoja ya kuwasilisha azimio hilo bungeni.

“Kwanini mheshimiwa mwenyekiti unanizuia mimi kuzungumza hapa? Kwa nini? Sina haki? Sina haki ya kuzungumza hapa? Niliyonayo hayawezi kuibariki nchi? Kwa nini? Kwa nini unanizuia kuzungumza?” alihoji Mtikila.

 “Unataka nikuheshimu wakati wewe heshima yangu unaivunja? Nataka kujua. Ni haki yangu. Ni haki yangu, nataka unijibu. “Nataka kujua kwa nini hutaki nizungumze hapa ndani? Nataka uniambie. Unachagua watu wanaozungumza kile unachofurahia wewe haki ya kuzungumza hapa ndani?”

“Nataka kuzungumza. Ni haki yangu. Siyo kwa kupenda wewe. Ni haki.” “Neno la haki limenenwa mara nyingi sana hapa ndani. Na haki msahafu unasema ni sehemu ya ufalme wa Mungu. Wewe humheshimu Mungu? Nataka kusema. Ninalo la kusema.”

MTIKILA NJE YA BUNGE

Baada ya Bunge kuahirishwa, Mtikila alitoka nje ya ukumbi wa Bunge na kuzungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge na kusema azimio hilo limepitishwa kwa hila.

 “Kanuni si halali kwa sababu haijakamilika. Katiba halali haiwezi kufanywa kwa hila na uhuni,” alisema Mtikila.

MKOSAMALI

Baada ya Mtikila kuzungumza hayo, Mkosamali naye alisimama na kuwasha kipaza sauti na kuanza kudai kuwa mara zote amekuwa akiomba kuchangia bungeni, lakini ananyimwa.

Alisema amekuwa akizuiwa kuzungumza kwa vile tu hakubaliani na maoni ya baadhi ya wajumbe, ambayo yametumiwa kupitisha kanuni mbovu. “Mwenyekiti, na mimi nasikitika, kila nikiomba kuchangia unaninyima,” alisema Mkosamali.

 “Na unawapa watu, ambao umekubaliana nao. Unawapa watu, ambao mnakubaliana na kupitisha kanuni mbovu. Wale, ambao hatukubaliani unatunyima haki ya kusema. Hiyo si haki katika kutengeneza katiba. Siyo haki.”

Akijibu madai hayo, Kificho alisema hakuweza kuwaruhusu Mtikila, Mkosamali na wengine, kwa kuwa aliona kwamba waliokwisha kuomba kusema wametosha.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment