- Kifungu cha (57) kimependekeza vikao vya Kamati za Bunge hilo vifanyike kwa faragha wakati wa majadiliano ya kupitisha hoja na masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara.
Dar es Salaam. Bunge Maalumu la Katiba limekuwa likiendelea mjini Dodoma ambako hakuna shaka moto umewaka.
Vikao vya Bunge hilo katika baadhi ya nyakati vimewaka moto, hatua inayotafsiriwa kuwa ni afya au kukomaa kwa demokrasia nchini.
Ushindani wa hoja ambao umejitokeza katika mjadala wa kanuni zitakazotumika kuongoza Bunge hilo pia ni ushahidi kwamba ipo kazi.
Katika vikao hivyo, hoja mbalimbali zimeibuliwa na
kuwekwa sawa au kupatiwa ufumbuzi kwenye vifungu vyenye utata katika
rasimu hiyo ya kanuni.
Hata hivyo, vile vyenye utata vimepelekwa kwenye
kamati ya watu makini, wenye busara ambayo imeundwa na mwenyekti wa
muda, Pandu Ameir Kificho.
Baadhi ya vifungu vilivyoteka hisia katika mjadala
huo ni pamoja na kifungu cha (57) kinachopendekeza vikao vya Kamati za
Bunge hilo vifanyike kwa faragha wakati wa majadiliano ya kupitisha hoja
na masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara.
Mvutano mwingine uliojitokeza kwa wajumbe hao,
ulitokana na kifungu kingine kinachopendekeza kuwepo kwa kura ya uwazi
wakati wa kupiga kura ya kuamua hoja mbalimbali za rasimu hiyo ya Katiba
Mpya.
Hata hivyo, wachambuzi mbalimbali wa masuala ya
siasa na utawala nchini wanasema vifungu hivyo vimeonekana kuwa mfano
wa sura mbili zinazojifitini kutokana na ukinzani uliopo kwa waumini
hao hao wa hoja ya uwazi.
Wanapendekeza kuwepo kwa vikao vya faragha wakati wa majadiliano ya kamati.
Katika mahojiano maalumu na wanasheria, wanahabari
na wasomi mbalimbali nchini ili kupata ufafanuzi wa hoja hizo na
tafsiri zinazoendelea kujitokeza.Wengi wanatoa hoja zinazokinzana.
Vikao vya faragha ni usaliti?
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Ruzuku kwa Vyombo vya
habari Tanzania(TMF), Ernest Sungura anasema Bunge hilo limeanza kujenga
kutokana na hatua ya kupitishwa kwa kifungu hicho cha faragha.
Aidha, anaongeza akisema pia kuwa pamoja na msingi wa uhuru wa
habari kutambuliwa na Katiba iliyopo, ni dalili mbaya inayojitokeza
katika kuandaa Katiba Mpya.
“Wanachojadili kilitakiwa kuripotiwa kwa kila
hatua kwa kuweka utaratibu mzuri ambao ungetoa nafasi kwa waandishi
kwani wao ndiyo wana uwezo wa kuchuja habari zinazostahili kwa jamii.
Kinachoripotiwa ni kwa manufaa ya Watanzania. Kwa hivyo ningeomba Bunge
litafakari kwa busara jinsi ya kuruhusu waandishi kushiriki vikao
hivyo,” anasema Sungura.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la
Habari (MCT), Kajubi Mukajanga ambaye ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba anasema walipendekeza waandishi wa habari washiriki vikao hivyo,
lakini maombi yao yamekwama.
“Sikuona sababu za Bunge kufikia hatua hiyo. Bunge
la Jamhuri ya Muungano wao wamekuwa wakiripoti bila masharti kwa nini
Bunge hili? Tuliopinga hatua hiyo wengi hatukupewa nafasi hata ya
kuzungumza kwenye vikao na badala yake wanasiasa wakateka mjadala,”
anasema Kajubi.
Anaongeza kuwa hoja ya waandishi kuwa na tabia za
upotoshaji katika kuripoti, haikuwa kigezo cha kuwafungia wasishiriki
vikao hivyo.
“Ni kweli kuna matatizo katika vyombo vyetu vya
habari katika kuripoti na binafsi sioni sababu ya kuingizwa kwenye
kanuni kwani hatua hiyo imekaa kiutendaji,” anasema na kuongeza:
“Hata hivyo, nimezungumza na Ofisi ya Bunge
inayohusika na habari ili kuona ni jinsi gani wanaweza kuandaa semina
kwa waandishi wote wa habari, kuwapatia maarifa, utaratibu ili waweze
kushiriki katika vikao hivyo.
Msomi mmoja kutoka moja ya vyuo vikuu nchini
anasema baadhi ya wajumbe walioshiriki kupitisha hoja ya vikao vya
faragha ni mafanikio ya kukwepa aibu ambazo zingibuliwa na waandishi.
“Its not fair (si halali) kwa kweli na
inasikitisha, hoja ya waandishi kupotosha haina mashiko. Kuna ushahidi
gani wa habari za kupotoshwa na zisizopotoshwa?
Je, kama hizo zinazoonekana kupotosha kwao ndiyo
zikawa na ukweli kwa Watanzania? Waache habari za kuchezea akili za watu
kwa propaganda chafu,” anasema msomi huyo.
Uwazi ni upotoshaji
Kupenyezwa kwa kifungu cha kura ya wazi ni moja kati ya siri
kubwa inayopigiwa chapuo na wajumbe mbalimbali hususan kutoka ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu(LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anasema pamoja na kukubaliana
na mfumo wa kura ya wazi, anapinga uamuzi wa kura hiyo kutumika katika
muundo wa Bunge hilo huku akibainisha kuwa ni upotoshaji.
Anatofautisha msingi wa kura hizo akisema: “Kuhusu
kura ya wazi yenyewe hutumika katika majadala isiyokuwa na athari au
mivutano ya kimasilahi. Kwa mfano katika kupitisha bajeti ndiyo kura
inaweza kupigwa ya wazi ili kuona ni watu gani wanakubaliana kwa wakati
huo, hatua hiyo haina sababu. Anaongeza: “Lakini kura ya siri hutumika
kwenye mazingira yenye utata na ukinzani wa kimitazamo ili kuepuka
ushawishi unaoweza kutolewa na kundi fulani lenye nguvu katika mazingira
ya kifedha au kichama.”
Bisimba anasema mapendekezo ya kanuni hiyo
yanatakiwa kupitisha kifungu cha kura ya siri ili kuepusha ushawishi
kutoka ndani ya vyama na makundi mbalimbali yenye masilahi binafsi.
Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea kutoka
Kampuni ya Sengalawe(Sengalawe Advocates), Sengalawe Charles anasema
duniani kote demokrasia hukosa nguvu katika harakati za kufanya
mabadiliko ya mfumo wa serikali iliyopo madarakani.
“Kuna Mtanzania gani ambaye mpaka sasa hajafahamu
mbinu zinazoandaliwa na CCM katika mchakato huo? Ni vigumu kusimamia
misingi ya demokrasia kwa sababu ni tofauti na mfumo wanaoutumia ambao
unalalamikiwa muda mrefu, kwa hivyo tusitegemee mabadiliko yoyote,”
anasema Sengalawe.
Msingi wa kura ya siri
Kutokana na mazingira hayo, Profesa Chris Maina
Peter kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anafafanua msingi wa
kura ya siri akisema kuna mataifa duniani yaliyoibua mjadala wa kura
ipi iweze kutumika katika wakati wa chaguzi.
“Nchi hizo ni Ugiriki na Roma katika miaka ya BC
(Kabla ya Kuzaliwa Kristo), lakini baada ya mvutano mkali kura ya siri
ikapitishwa na mataifa mengine yakaanza kuitumia ikiwamo Ufaransa
(1795), Uholanzi (1849), Australia(1856) na Uingereza (1872) ambayo
tunaifuata,” anasema na kuongeza:
“Kwa upande wa Marekani ubishi uliendelea mpaka
ilipofika mwaka 1891 jimbo la mwisho kukubaliana na utumiaji wa kura ya
siri lilikuwa ni Kentucky.
Kule Uingereza, mfumo wa kura ya siri bado
unapingwa kwa sababu unatumia namba za kuwatambua wapigakura, kitu
ambacho bado haiwezi kuwa na azimio la kura ya siri.
Aidha, msomi huyo anasema endapo wajumbe hao
watapisha kipengele hicho kutambua kura ya wazi, watakuwa wamevunja
Katiba na Mikataba ya Umoja wa Kimataifa(International Covenant on Civil
and Political Rights) ya mwaka 1966 inayofafanuliwa katika ibara ya
25(b) kifungu kinachosema:
“Kila raia atakuwa na uhuru na haki ya kupiga au kupigiwa kura katika mazingira ya usiri bila kubugudhiwa, bila kuathiri uhuru wake wa kujieleza kupitia utaratibu wa kumchagua mgombea ili kuepuka ushawishi na matakwa ya kisiasa.”
source: mwananchi
“Kila raia atakuwa na uhuru na haki ya kupiga au kupigiwa kura katika mazingira ya usiri bila kubugudhiwa, bila kuathiri uhuru wake wa kujieleza kupitia utaratibu wa kumchagua mgombea ili kuepuka ushawishi na matakwa ya kisiasa.”
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment