Dar es Salaam. Azam imezidi kunyemelea ubingwa
wa Ligi Kuu msimu huu baada ya kuichapa Simba 2-1, huku mabingwa
watetezi Yanga wakichapwa 2-1 na wachezaji 10 wa Mgambo Shooting kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mabao ya Hamisi Mcha na John Bocco yalitosha kuipa
Azam pointi tatu muhimu na kuongoza ligi kwa pointi 53, huku beki
Joseph Owino akifunga bao la kufutia machozi kwa Simba.
Nayo Mgambo wakicheza zaidi ya dakika 60 wakiwa
pungufu waliwaduwaza Yanga kwa kuwachapa 2-1. Mgambo walikuwa pungufu
baada ya beki wao Mohamed Netto kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika
ya 30 na mwamuzi Alex Mahaji aliyehisi mchezaji huyo amevaa hirizi
katika nguo yake ya ndani, lakini alipokaguliwa haikuonekana. Mabao ya
Mgambo yalifungwa na Fully Maganga na Malima Busungu.
Wakati Yanga wakisuasusa na pointi 46, Mbeya City
imejiimarisha katika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 45, baada ya
kuwafunga ndugu zao Prisons kwa bao 1-0.
Katika Uwanja wa Taifa; Mcha aliwainua mashabiki
wa Azam dakika ya 16 akiunganisha krosi kutoka upande wa kushoto baada
ya wachezaji wa Simba, Donald Musoti na Amis Tambwe kugongana walipokuwa
wakijaribu kumzuia Tchetche na kutoa mwanya kwa mfungaji kupiga shuti
lililomwacha kipa Mapunda asijue la kufanya.
Simba walisawazisha bao hilo dakika ya 45 baada ya
mpira wa adhabu uliopigwa na William Lucian kutua kichwani kwa Joseph
Owino na kuifungia Simba bao hivyo timu hizo kwenda mapumziko zikiwa 1-1
huku mashabiki wa Yanga waliojitokeza uwanjani wakiishangilia Simba kwa
nguvu.
Kipindi cha pili, Azam walimtoa Mcha na kumwingiza
Kelvin Friday dakika ya 52, mabadiliko yaliyokuwa na faida kubwa kwao
kwani dakika mbili baadaye Bocco aliifungia bao la pili akiunganisha
mpira uliopigwa na Tchetche na kugonga mwamba na kurudi uwanjani.
Mjini Tanga mshambuliaji Fully Maganga aliifungia
Mgambo Shooting bao la kuongoza dakika ya kwanza kwa kichwa akiunganisha
mpira uliokuwa umepigwa na kipa Juma Kaseja kwenda kwa Kelvin Yondani.
Hata hivyo, katika mechi hiyo, Mgambo walipata
pigo baada ya Mohamed Netto kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 30 na
mwamuzi Alex Mahaji aliyehisi mchezaji huyo amevaa hirizi katika nguo
yake ya ndani, lakini haikuonekana.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub aliifungia timu
yake bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti dakika ya 51 baada ya beki
wa Mgambo, Novart Lufunga kumchezea vibaya mshambuliaji wa Yanga kwenye
eneo la hatari. Hii ni mara ya tatu kwa Yanga kushindwa kupata ushindi
inapocheza dhidi ya timu pungufu, walitoka 0-0 na Mtibwa na sare 1-1 na
Azam. Busungu aliipatia Mgambo bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika
ya 66 baada ya Kelvin Yondani kumwangusha kwenye eneo la hatari.
Katika Uwanja wa Sokoine Mbeya mshambuliaji Paul
Nonga aliipatia Mbeya City bao la kuongoza dakika ya pili baada ya
kuwazidi mbio mabeki wote wa Prisons na kufunga bao hilo lililoamsha
shangwe.
Morogoro; Katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja
wa Manungu, wenyeji Mtibwa Sugar walienda mapumziko wakiwa mbele kwa
mabao 3-1, shukrani kwa mabao ya Jamal Mnyate dakika ya 14, Mussa
Hassan Mgosi (30), na Mohamed Mkopi (81), huku Behewa Behewa akiifungia
Coastal Union dakika ya 16
Imeandaliwa na Sosthenes Nyoni (Dar), Yakubu Burhani (Tanga) Godfrey Kahango (Mbeya), Juma Mtanda (Morogoro).
source: Mjengwa blog
Imeandaliwa na Sosthenes Nyoni (Dar), Yakubu Burhani (Tanga) Godfrey Kahango (Mbeya), Juma Mtanda (Morogoro).
source: Mjengwa blog
No comments:
Post a Comment