Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
jana alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni baada ya kutoa
mapendekezo yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa zinavutana kuhusu
kupitisha baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la Katiba.
Katika mapendekezo yake yaliyoungwa
mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Pinda alisema: "Nataka kuwaomba wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye
malumbano) tukiwa tunayapitia kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na
kumwomba Mwenyekiti aunde timu ya watu wazima na wenye busara wajaribu
kuyatazama. "Tujadiliane, tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha
inayoweza kukasirisha. Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema..."
Waziri Mkuu, aliwataka wajumbe wajiepushe na lugha za kuudhi ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya.
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga mkono ushauri huo, Mbowe
alisema Bunge limejaa hisia za hofu ndani na nje, jambo ambalo linatia
wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Alisema iwapo wajumbe
watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama, idadi yao katika
makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai alionya kuhusu matumizi ya lugha
za kuudhi huku Profesa Lipumba akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya
Taifa kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya
Watanzania wote bila ya kujali masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali, mjadala wa utaratibu wa upigaji
kura katika Bunge hilo ulichukua sura mpya baada ya kudaiwa kuwapo
ushawishi unaohusisha utoaji wa bahasha ili kutaka kuungwa mkono katika
misimamo inayokinzana.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa
watuhumiwa katika sakata hilo ni baadhi ya wajumbe ambao ni mawaziri na
mbunge mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa kuwashawishi wajumbe ambao
hawatokani na vyama vya siasa ili kupitisha agenda ya kura ya wazi
kirahisi.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa
Facebook, Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, alisema: "Jaribio la kuzuia kura ya siri limechukua
njia za aibu, baada ya CCM kutumia fedha kushawishi wajumbe."
Katika ujumbe huo ambao alikiri
kuuandika, Mtatiro aliwataja wajumbe watatu ambao ni mawaziri kuwa
waliwakaribisha wajumbe kwenye makazi yao na "kuwaandalia chakula cha
kutosha, vinywaji vya kutosha na viburudisho vingine, huku wakipewa
bahasha za nauli baada ya vikao hivyo vya siri." Mmoja wa waliotajwa ni
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyedaiwa kuwaalika
wawakilishi wa wafugaji na kuwapa chakuka na bahasha.
Akijibu tuhuma hizo, pamoja na kukiri
kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula nao chakula, alikana tuhuma za
kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa chama hicho. Alisema Mtatiro
amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na mwanasheria wake ili kumfikisha
mahakamani.
"Siwezi kumuacha hivihivi Mtatiro,
lazima nichukue hatua. Hawa niliwaalika kama marafiki tu, tukala wote
chakula. Mbona hata kesho nimealikwa na Kajubi Mukajanga (Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania), hivi nikienda kukutana naye
ndiyo atakuwa amenipa rushwa?"
Waziri mwingine ambaye jina lake
linahifadhiwa kwa sababu hakupatikana kujibu tuhuma zake anadaiwa
kuwaalika wawakilishi wa vyuo vya elimu ya juu, huku mbunge mmoja pia
akidaiwa kuwaita wafugaji.
Kulikuwa na mgawanyiko wa wazi katika
kanuni hiyo ya upigaji kura, CCM kikitaka kuungwa mkono kwa utaratibu wa
kupiga kura za wazi huku wapinzani wakitaka za siri kama zilivyokuwa
zimependekezwa na Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda kuhusu Kanuni.
Akizungumzia suala hilo, Mjumbe wa
Bunge hilo, Makersia Jibubu alisema: "Sikutarajia haya. Nilichojua,
tungefika wiki ya kwanza tukapitisha kanuni na baada ya hapo tukaendelea
na mijadala. Lakini kinachoonekana ni mivutano ya wanasiasa na kibaya
zaidi wote wanalenga kundi la wajumbe wateule wa Rais."
Alisema alianza kuwa na wasiwasi
kuhusu Bunge hilo, mara tu alipofika na kundi lake kuitwa na moja ya
vyama vya siasa kufanya mazungumzo kwa lengo la kutaka ushawishi wao.
"Makundi yote yaliyoteuliwa na Rais
yaliitwa na vyama vya siasa. Wakaandaa mikutano kwa chakula na vinywaji,
halafu wakaanza kueleza sera zao. Nikasema sasa hii ni kwa faida ya
nani?"
Mkutano wa CCM
CCM kilifanya mkutano wa wajumbe wake
juzi usiku chini ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif
Idd. Pamoja na mambo mengine, kinadaiwa kutoa msimamo kuwalazimisha
wajumbe wake kuunga mkono kura ya wazi.
Chama hicho kilitumia takriban muda wa
saa tatu kuwafunda wajumbe hao ili kuhakikisha kuwa wanatetea utaratibu
huo. Mkutano huo ulianza saa 2:15 hadi saa 5:00 usiku.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidokeza kuwa ajenda kuu ilikuwa ni kupitia rasimu ya kanuni.
Mjumbe mmoja alisema: "Inavyoonekana
sasa suala la kupiga kura ya wazi ni amri na halina tena mjadala, lakini
litaleta matatizo makubwa mbele ya safari... yetu macho.
"Mle ndani sisi wengine tuliamua kunyamaza kimya, maana hata unaposimama na kuchangia bado watu wanakuona kama ni msaliti."
Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment