Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa gazeti hili, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana.
Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Mjadala wa Mabadiliko
ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba
alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza
kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye
mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo
ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya
Profesa Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano
la Vijana lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza
Muungano Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya
Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano
hilo, Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana
budi kuzingatia mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye
Rasimu kuwa ni Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina
mamlaka katika pande hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa
viongozi halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa
Zanzibar, Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi
wa Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa
Shivji, ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania
kwa kuangalia sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya
Jaji Warioba walikuwa na nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa
kusema "the road to hell is paved in good intention," akimaanisha kuwa
njia ya kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba
alisema Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea
utaifa wa Zanzibar na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
"Shivji ni msomi na mimi najua
anaelewa matumizi ya takwimu," alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa
Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na
gazeti hili nyumbani kwake jana jioni.
"Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi."
Jaji warioba alisema Shivji ndiye
amekuwa chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake.
Alisema waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa
wananchi wa Zanzibar.
"Shivji alikuwa anasema Tanganyika
imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe
wazi isijifiche," alisema Jaji Warioba. "Na Shivji amechochea hilo...
wote wale waliokuwa wanamnukuu walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi
yake na kwamba mpaka leo hii kuna watu wa Zanzibar wanaamini Muungano
huu si halali kisheria kutokana na Shivji ambaye alisema Baraza la
Mapinduzi halikuridhia articles (ibara) za Muungano."
Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma
hizo za uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na
Utanganyika, Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa
hajamsikia Jaji Warioba akizungumzia hilo.
"Hey, amezungumza lini?" alihoji. "Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe."
Lakini Jaji Warioba alisema watu
walitumia msingi huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji
amesababisha hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa
yanatokana uchochezi huo.
"Hata kabla ya sisi kuanza mchakato
huu, Shivji alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na
akawaambia issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa
leo anaona kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea
nationalism (utaifa)," alisema Jaji Warioba.
Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema
mara ya kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu
muundo wa Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa
47,000, huku watu 27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka
Zanzibar.
"Safari hii ametaja zile za Tanzania
Bara na kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu
300,000 waliotoa maoni," alisema Warioba.
Alisema Tume ilitumia takwimu
zinatokana na watu waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na
si kwa ujumla na ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa
makusudi.
Warioba alimuelezea Profesa Shivji
kuwa sasa ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda
Rasimu ya Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio
unaoifaa Tanzani kwa sasa.
Aidha, Warioba alisema msimamo wa Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010.
" Nimeshangazwa na Shivji kusema
kwamba kitendo cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa 'Zanzibar ni Nchi'
halikuwa jambo la ajabu," alisema Warioba.
Alisema Shivji ni msomi ambaye anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika muundo wa Muungano.
"Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi,
alijibu kuwa Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka," alisema.
Alisema lakini msomi kama Shivji haoni
kama suala hilo la 'Zanzibar ni nchi' lina madhara makubwa katika
mstakabali wa taifa letu.
Jaji Warioba alisema kama serikali
tatu hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili
Katiba yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo
haiwezekani.
"Maana kama ni kusahihisha, ni lazima
kwanza Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba
ya Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,"
alisema.
"Zanzibar wakubali Rais wa Muungano
ana madaraka nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa
Jamhuri ya Muungano madaraka yake."
Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro,
Christopher Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu
hazionyeshi uhalisia wa maoni ya wananchi.
"Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro
linakuwa na watu 100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu
20,000 na waliopiga kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake
utakuwa katika watu waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,"
alisema Warioba.
Chanzo, mwananchi
No comments:
Post a Comment