Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la
Katiba, Pandu Ameir Kificho, akizungumza na mjumbe wa Bunge hilo,
SamuelSitta (kushoto), ndani ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma jana. Picha na
Emmanuel Herman.
Dodoma. Siku moja baada ya kuteuliwa
na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa
Ushirikiano wa AfrikaMashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia
sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki
kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta
alisema: "Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi
kuwa nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba."
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya
uteuzi huo ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza
bunge hilo na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji
kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani
ya chama hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, AndrewChenge alisema: "Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu
ndani ya CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta
msuguano, basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua
majina mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa
kuniteua na kwa sasa najiandaa na uchaguzi."
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo
aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu
Hassanaliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa
kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri
ambayo haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa
nafasi hiyo.
"Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote," alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira
na Wanawake na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa
Rais.
Kinana na mchakato.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema
ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa
hiari yake kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi
wa chama kwa ushauri. Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma,
Kinana alisema: "Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la
Katiba, angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili
walionyesha nia; Sitta na Chenge.
"Wote hawa wana sifa kwa historia za
maisha yao. Chenge aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sitta,
Waziri wa Sheria na Katiba, halafu wote ni wanasheria. Hawa wote
wakaanza kutafuta maoni kwa wenzao na kila mmoja akitafuta wenzake wa
kumuunga mkono. Kwa sababu wote ni wanaCCM na kwa kuogopa makundi,
tukaona tuwaite na kuwaambia jamani nyie wote ni wetu, tusingependa
mkalumbane.
"Tukawaambia washauriane na kufikia
mwafaka. Chenge akajitoa mwenyewe na jana (juzi), kwenye mkutano,
WanaCCM wote wakaamua kumuunga mkono Sitta."
Mjadala moto bungeni.
Wakati huohuo; mjadala wa kanuni za
Bunge la Katiba umeendelea kuwa moto baada ya baadhi ya wajumbe kutaka
kanuni zitambue haki ya mwanamke katika nafasi hiyo ya juu ya uongozi.
Malumbano hayo yalizuka wakati wajumbe
hao walipokuwa wakijadili kanuni ya saba inayohusu uchaguzi wa
mwenyekiti na makamu wake. Mjumbe wa bunge hilo, Christine Mzava
alishauri kuwa endapo mwenyekiti atakuwa mwanamume, makamu wake awe
mwanamke.
Akijibu hoja hiyo, Mjumbe wa Kamati ya
Kanuni, Magdalena Rwebangila alisema kwa kuwa sheria imetamka kuwa
mwenyekiti akitoka Tanzania Bara, makamu atatoka Zanzibar, itakuwa
vigumu kuweka uwiano mwingine wa kijinsia.
Baada ya ufafanuzi huo, Lediana
Mng'ong'o alisimama na kusema: "Kwani mnaona ugumu gani wa kuongeza
hicho kipengele? Mbona Rais katika uteuzi wa wajumbe 201 alizingatia
uwiano wa kijinsia?"
Mjumbe mwingine wa Kamati ya Kanuni,
George Simbachawene alisema haiwezekani kuwa na aina mbili za uwiano.
Hali hiyo ilimfanya mjumbe mwingine, Dk Ave-Maria Semakafu kusimama na
kuomba busara itumike na kutengua kanuni kwa kuweka nafasi sawa.
Hata hivyo, Mjumbe Ezikiah Wenje alisema itakuwa ajabu kumchagua mtu katika nafasi hizo kwa sababu tu ni mwanamke.
"Demokrasia inahitaji ushindani sawa
na hao kinamama wanaamini tuko sawa. Mimi naomba kama kuna mtu ana sifa
za kuwa mwenyekiti au makamu, wagombee washindane," alisema.
Maelezo hayo yaliwafanya wajumbe
wanawake kusimama na kuanza kuimba: "Tunataka haki zetu, tunataka haki
zetu." Kuona hivyo, Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, Anna Abdallah alisimama
na kuwataka wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waliopitisha sheria
hiyo kujilaumu kwa sababu walipaswa kuliangalia hilo.
Chanzo, mwananchi
No comments:
Post a Comment