WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 28, 2014

Bunge machafuko

  Ni matumizi ya kura zote, wazi na siri
  Mwigulu achafua hali ya hewa
  Ezekiel Wenje awavuruga Mawaziri,Wajumbe

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuani na haki za Bunge Maalum la Katiba, Pandu ZAmeir Kificho (Kushoto), akiwasilisha mapendekezo ya kamati kuhusu butaratibu wa upigaji kura bungeni mjini Dodoma jana,kulia Mjumbe John Mnyika akichangia pia.(Picha na Khalfan Said)
Kitendawili cha kura ya wazi au ya siri limeemdelea kuliandama Bunge Maalum la Katiba kwa kuzua mvutano mkali jana jioni baada ya Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge kuwasilisha azimio la kupendekeza utaratibu wa kura ya siri na ya wazi kutumika kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba.
Jana jioni yalizuka malumbano baada ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Pandu Ameir Kificho, kuwasilisha mapendekezo ya azimio la utaratibu wa wajumbe kupiga kura kwa kutumia njia mbili za kura ya wazi na siri kwa kadri kila mjumbe atakavyoona inafaa.

Baada ya kamati hiyo kuwasilisha mapendekezo yake, baadhi ya wajumbe walitoa maoni wengine wakipendekeza kutumika kwa kura ya kielektroniki na wengine wakipinga vikali kwa madai kuwa itakuwa na uchakachuaji.

MAKONDA

Paul Makonda alipendekeza kutumika kwa kura ya kielektroniki ambayo itaokoa muda wa upigaji kura na kila mmoja kufanya kwa uhuru zaidi.

Alisema mvutano uko baina ya wajumbe waliowafuasi wa vyama vya siasa huku 201 wakiwa njiapanda.

PAMELA
Mjumbe Pamela Maasai alisema kura ya elektroniki ni rahisi kuchakachuliwa hivyo siyo vyema Bunge hilo kukubali utaratibu huo na badala yake kura ya siri ambayo itatoa uhuru kwa kila mjumbe kufanya kwa uhuru.

NASSARI
Joshua Nassari aliwataka wajumbe kuacha unafiki na kila mmoja auzungumze kama haifahamu kesho, Katiba iwe neema kwa makundi yote kwa miaka ijayo.

“Bunge moja, taifa moja, katiba moja, nchi moja halafu upigaji kura uwe tofauti, wenzetu wanatengeneza ndege zinaruka bila rubani unasema tumebuni kupiga kura kwa kila kundi kupiga watakavyo…wengi wa wabunge wa CCM wanataka serikali tatu, ila wanashindwa kusema, njia pekee ya kuwasaidia ni kura ya siri,” alisema.

Alisema uchaguzi wa viongozi mbalimbali kura ni ya siri, wajumbe wa Bunge hilo nao wameteuliwa na Rais ambaye alijifungia na kuwateua kwa siri,” alisema na kuongeza kuwa siyo ajabu kwa Bunge hilo kupiga kura ya siri.

OLUOCH
Ezekiel Oluoch alisema kura ya siri ndiyo itasaidia kuiwafanya watu kuwa huru kwa kuwa ndani ya katiba hiyo kuna masuala ya kidini yanayopaswa kuamuliwa kwa usiri.

Alisema kura ya siri inatumika kuamua mambo yenye imani na utata mkubwa kwa kuwa inamsaidia mtu kuwa huru katika kuamua.

LAIZER
Mjumbe Michael Laizer alisema Kamati hiyo imepeleka pendekezo la kutoa suluhisho la utaratibu wa upigaji kura na kama haukubaliki ni wakati wa Mwenyekiti kuwuandikia Rais avunje Bunge ili wajumbe watawanyike na kuondoka Dodoma.

MBOWE

Freeman Mbowe, alisema ni lazima wafike hatua wafanye uamuzi kuliko kuendelea kujadili huku akisema Machi 11, mwaka huu walipitisha kanuni bila kifungu cha 37 na 38 vinavyozungumzia utaratibu wa kura ya wazi na siri.

Alisema utaalamu wa kurushiana maneno na vijembe hausaidii lolote na kwamba ni dhahiri kuwa kwa mazingira ya jana hakuna utaalamu wa kufikia mwafaha kwenye ukumbi kwa kila mmoja kuzungumza kwa kadri utaalamu wake unavyomruhusu.

“Pamoja na utaalamu wetu wa kufanya maamuzi hatuwezi kuliamua suala hili, itakuwa ni aibu tutajikuta kwenye mazingira ya kulazimisha na kuvunja Bunge, hakuna atakayetakoka mshindi si aliyesababisha na ambaye hakusababishiwa,” alisema

Alishauri viongozi wenye busara kukutana na kuzungumza na kuja na uamuzi sahihi kwa kuwa jambo la Katiba ni jambo la maridhiano, hivyo ni lazima kuwe na makubaliano ya kusonga mbele.

MWANGUNGA
Shamsha Mwangunga, alisema wanaotaka kura ya siri ni wanafiki, hawajiamini na wawajui walifanyalo na kwamba ni vyema likafanyika kwa uwazi.

“Tunashindwa kupiga hatua ya mbele kwa kuvutana, hivyo ni vyema kukubali ushauri wa kamati wa kila mmoja kupiga kura anayoona inafaa,” alisema.

RAZA
Mohamed Raza, alisema kura ya wazi ndiyo inayofaa na kwamba kuendelea kulumbana ni kutumia vibaya fedha za Watanzania.

MAKAIDI
Dk. Emmanuel Makaidi alisema kura ya siri itatoa nafasi kwa kila mjumbe kuonyeshana dhamira yake pasipo woga.

“Kura ya elektroniki haifai kuamua, tukubali kura ya siri kama ndiyo msingi wa maamuzi yetu,” alisema.

LEMA
Godbless Lema alisema kura ya siri itawaingiza baadhi ya wajumbe kwenye matatizo kwa kuwa kwa sasa kuna matamko mbalimbali yamesambaa kwenye mitanda ya jamii, vitisho vingi, ikiwamo Zanzibar inasema atakayerudi bila Zanzibar huru kichwa chake kitakuwa halali yao.

Alisema Waziri Mkuu ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya wabunge wa CCM akiamua kupiga kura ya siria haamini kama yupo anayeweza kwenda kinyume cha kiongozi wake ambaye amepinga kura ya wazi.

BULAYA
Esther Bulaya alisema msimamo wake ni kura ya siri, lakini amefurahia mapendekezo ya kamati ya kila mmoja kupiga kura kwa nutaratibu anaupenda, hivyo ni vyema wajumbe hao wakakubaliana na kamati.

MWIGULU
Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, alichafua hali ya hewa baada ya kuwatuhumu Freeman Mbowe na Ismail Jussa Ladhu kuwa wanataka kura ya siri kwa kuwa wanalengo la kuingiza ushoga.

Baada ya kauli ya Nchemba, Profesa Ibrahim Lipumba aliomba mwongozo wa Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan, akisema Bunge linaangaliwa na watu wa rika tofauti wakiwamo watoto na kwamba Nchemba ametumia lugha isiyo na staha.

Samia alimtaka Nchemba kufuta kauli yake na kuwaomba radhi Mbowe na Jussa, lakini aliendelea kutetea hoja yake akidai kuwa baadhi ya vyama (bila kuvitaja) vinafadhiliwa na nchi zinazokubali ushoga na kwamba ataondoa majina ya Mbowe na Jussa, lakini neno ushoga litabaki pale pale.

Kufuatia kauli za Nchemba, wajumbe waliendelea kupiga kelele na kutaka afute kauli na kuomba radhi, huku Samia akitumia dakika kadhaa kuwatuliza wajumbe na kumtaka Nchemba kufuta kauli na kuomba radhi.

Hata hivyo, baadaye Nchemba alifuta kauli hiyo na kuwaomba radhi Mbowe na Jussa.

MAPENDEKEZO YA KIFICHO

Akiwasilisha Azimio la kufanya marekebisho ya Kanuni za Bunge la Maalum jana, Kificho alisema kuwa marekebisho yanayofanywa ni kanuni za Bunge Maalumu kwenye kanuni ya 37 kwa kuongeza mwishoni mwa fasiri ya (3) maneno “ya siri kwa mjumbe anayetaka kupiga kura ya siri au kura ya wazi kwa mjumbe anayetaka kupiga kura ya wazi kwa kuzingatia utaratibu ulioanishwa katika kanuni ya 38.

WENJE AWASHA MOTO
Kauli ya Ezekiel Wenje kuwa baadhi ya mawaziri wamewahonga baadhi ya wabunge wa makundi ya wabunge 201 ilisababisha vurugu kubwa kwa mawaziri tajwa kutaka waombwe radhi, akiwamo, Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi).

Mbali na mawaziri hao pia wajumbe kutoka kundi hilo walitaka kuombwa radhi.

Awali Makamu Mwenyekiti aliyekuwa anaongoza kikao, Samia Suluhu Hassan,  alimtaka Wenje kuomba radhi, lakini alisema mawaziri hao wamethibitisha wenyewe kuwaalika watu hao na kuongeza orodha ya mawaziri kuwa ni pamoja na Gaudensia Kabaka (Kazi na Ajira) na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba walihusika kuwakirimu wajumbe hao na kuwapa msimamo wa serikali mbili.

Wakati vurugu za kelele na kurushiana maneno zikielendelea, Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta, alirejea kwenye kiti chake na kumtaka Wenje amjibu kama kweli haoni kuwa kauli yake imewaudhi wajumbe wengine.

Wenje alisema kuwa inawezekana kuwa kuna watu wameudhika, lakini kwa kuwa alichosema ni ukweli na kwa kuwa anaomba radhi tu, lakini ukweli anausimamia.

Kwa kauli hiyo, Sitta alisema kwa kuwa Wenje amekataa kuomba radhi, basi suala hilo ameamua kulipeleka kwenye kamati ya Kanuni na Haki za Bunge la Bunge Maalum.

Baada ya uamuzi wa Sitta wajumbe walishangilia na Wenje alionekana alishangilia uamuzi huo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment