HATIMAYE
Bunge Maalumu la Katiba, limepitisha rasimu ya Kanuni zitakazotumika
kuongoza majadiliano, pamoja na vifungu ambavyo havikutaja aina ya
upigaji kura kama utakuwa wa wazi au wa siri. Hata hivyo, wakati Bunge
likipitisha azimio hilo, baadhi ya wajumbe wamelaani kitendo cha
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, kuridhia
kupitishwa kwa ‘kanuni nusu’ za Bunge kwa maelezo kuwa jambo hilo
halitaleta muafaka.
Wajumbe
hao pia wameonya kuwa Bunge Maalumu la Katiba, linaweza kushindwa kupata
muafaka wa njia ya kufanya uamuzi iwapo wajumbe ndani ya Bunge hilo
watang’ang’ania ushabiki na itikadi za vyama vyao.
Azimio la
Kutunga na Kupitishwa kwa Kanuni hizo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu ambaye alitaka kanuni zipitishwe
pamoja na aina ya upigaji kura kwa ajili ya kupata uamuzi wa Bunge
Maalumu unaendelea kushughulikiwa.
“Suala la
upigaji kura, litawekwa katika kanuni husika baada ya kuamuliwa kama
ambavyo Bunge hili maalum litaona inafaa,” alisema Profesa Mahalu
akizungumzia vifungu vya 37 na 38 vinavyoelezea namna ya upigaji kura
ambapo kanuni hizo zimeelezea uamuzi utakaopitishwa kwa upigaji wa kura.
Wakichangia
wakati wa kupitishwa kwa kanuni hizo, Profesa Ibrahim Lipumba alisema:
“Kanuni nzuri zinakidhi mahitaji ya kuendesha vizuri Bunge la Katiba.
Kanuni zimetuhakikishia haki na kinga za kila mjumbe na kutakuwa na
uhuru bila kushurutishwa au kupokea maelekezo kutoka kwa yeyote au
chombo chochote, naomba tuzipitishe.”
Naye
James Mbatia aliomba vifungu vya 37 na 38 ambavyo havijakamilishwa
vichukue muda mfupi vikamilishwe. Kwa upande wa Idrisa Kitwana Mustafa
alisema:
“Mshikamano
wetu ndiyo utakaowapa moyo wananchi walio nje ya Bunge hili. Tukubali
kuwa hakuna kazi ya mwanadamu itakayoridhisha kila mtu na tuchukulie
upungufu uliojitokeza kama ni mambo madogo kwani tuna kazi kubwa mbele
yetu”. Panya Ali Abdallah alisema anaamini tunu ya hekima na busara
itatumika katika kupata Katiba. Shehe Mussa Kundecha alisema:
“Hakuna kazi ya mwanadamu ikakosa kasoro…ni busara kuona watu wakikubaliana kwa yale waliyotofautiana , tuliombee Bunge hili”.
Kwa upande wa Freeman Mbowe wakati anaunga mkono azimio hilo, aliwataka wajumbe washirikiane, kuheshimiana na kuvumiliana.
Mbunge wa
Mwibara, Kangi Lugola alilaani hatua ya Mwenyekiti wa Muda wa Bunge
Maalumu, Pandu Ameir Kificho, kukubali kanuni kupitishwa ‘nusu’ kwa
sababu ya kuzidiwa nguvu na vyama vya siasa ambavyo vimesimamia itikadi
zao na vinatoa vitisho kwa wabunge wake wakubaliane na misimamo ya
vyama.
“Hii
Katiba tunayoenda kuitunga hapa ni Katiba ya vyama vya siasa na sio
Katiba ya wananchi, maana vyama vya siasa vyote vina misimamo kwenye
kuandika Katiba hiyo na ndicho kinafanya tushindwe hadi kuafikiana ndani
ya Bunge hili,” alisema.
Mbunge
huyo ambaye jana alisimama ukumbini kutaka kuzungumza lakini hakupewa
nafasi, alidai iwapo jambo hilo litakwama hapo baadaye, Kificho ndiye wa
kulaumiwa maana wiki ijayo ni wiki ya kufanya uamuzi lakini Kanuni
zimekaa kimya.
Alisema
kwa mara ya kwanza Tanzania itapata Katiba ya vitisho kutokana na vyama
vikubwa vya CCM, Chadema na CUF kuwalazimisha wabunge wake kuwa na
msimamo katika suala ambalo linahusu masuala ya wananchi na sio ya vyama
hivyo.
“Watanzania
wapo wengi hawana vyama, lakini hivi vyama vya siasa vimeng’ang’ana
kuwatisha wajumbe wake wasiende kinyume na misimamo ya vyama hivyo, hii
sio haki hata kidogo, tunachoandika hapa ni Katiba ya wananchi sio ya
vyama,” alisema mbunge huyo.
Alionya
kuwa wabunge wengi kwenye vyama vya siasa ni waoga hasa wa viti maalumu,
maana wanaamini kuwa wakienda nje ya misimamo ya vyama vyao,
watafukuzwa na hawatapata ubunge tofauti na wabunge wa majimbo.
Mbunge wa
Muhambwe Felix Mkosamali, alisema hata wajumbe ambao wamepitisha Kanuni
hizo watajilaumu kwa vile vikao vya Bunge haviwezi kuanza bila
kuafikiana namna ya kufanya uamuzi.
Mkosamali
ambaye awali alimlalamikia Kificho kwa kutompa nafasi ya kuzungumza,
licha ya kusimama mara nyingi, badala yake Mwenyekiti huyo wa muda
alikuwa anaruhusu wajumbe aliowataka.
“Toka
nimefika hapa sijapewa nafasi ya kuzungumza, nimesimama mara kwa mara;
lakini Mwenyekiti haniruhusu kwa vile tu anafahamu msimamo wangu ni
kupinga kanuni hizi kupitishwa nusu,” alisema Mkosamali.
Alipoulizwa
iweje apinge suala hilo wakati Mwenyekiti wake wa NCCR-Mageuzi Taifa,
James Mbatia alisimama kuunga mkono na kuwasihi wajumbe wote kuunga
mkono suala hilo, alisema Mbatia ana uamuzi wake katika Bunge la Katiba.
“Kwa
maoni yangu, Mbatia amekosea kuunga mkono suala hilo, huo ni mtazamo
wangu maana hapa hakuna mbunge wa chama bali sote sisi ni wajumbe,
hakuna mnadhimu wa chama hapa,” alisema Mkosamali.
Alisema
katika Bunge Maalumu la Katiba, mambo yote yanahitaji maridhiano hivyo
haipendezi Mwenyekiti kupendelea baadhi ya watu. Alisema anamsubiri
Mwenyekiti atakayechaguliwa ili awasilishe maoni yake.
Mchungaji
Christopher Mtikila kwa upande wake alisema alipinga kupitishwa kwa
azimio hilo la kuazimia Kanuni za Bunge Maalumu kwa vile limepitishwa
kwa hila na akashangaa wajumbe wengine kutoka kwenye Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kwa kuunga mkono kanuni hizo.
Mtikila
alisema suala la kanuni hizo kutokuwa na namna ya kupiga kura,
linaonesha dhahiri kuwa wajumbe hawana nia ya dhati ya kutunga Katiba
mpya kwa vile suala hilo litarudishwa kwa wajumbe hao lipate uamuzi.
Alisema
kuliahirisha ni kutoa fursa kwa baadhi ya watu kuwarubuni baadhi ya
wajumbe ili waweze kubadilisha misimamo yao na wanapoenda kupiga kuwa
wapigie kundi ambalo linang’ang’ania kura ya wazi.
“Ndio
maana wameliweka kiporo suala hili wanataka tukirudi hapa tuwe tumepowa
na watunywe vizuri kama uji wa ulevi,” alisema Mtikila.
Mbatia
kwa upande wake alisema wiki tatu zilikuwa ngumu kwa wajumbe, lakini
akasema kwenye Katiba ili jambo lipite ni lazima lipate maridhiano hivyo
kitendo cha kupitisha kanuni hizo kunatoa fursa ya mambo mengine
kuendelea na baadaye warudi kufanya uamuzi.
“Dola
linaundwa kwa njia ya maridhiano na ndio hatua tuliyofikia sasa, wahenga
wanatuasa pambana wakati mnazungumza, kisheria kanuni hizi ziko
sahihi,” alisema Mbatia.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment