Godfrey Mgimwa na Robby Mgimwa wakionesha hati yao ya ubunge baada ya kukabidhiwa leo |
Sehemu ya msafara wake |
Boda boda nao walikuwepo |
AKIWA ameambatana na mkewe, Robby
Mgimwa, Godfrey Mgimwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jana alitangazwa
mshindi wa ubunge katika uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga baada ya
kuvibwaga kwa kura za kishindo vyama vingine viwili vilivyoshiriki
uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika
Jumapili ya Machi 16, mwaka huu, Mgimwa alizoa kura 22, 962 ambazo ni
sawa na asilimia 79.32 dhidi ya kura 5,853 sawa na asilimia 20 alizopata
Grace Tendega wa Chadema na kura 150 sawa na asilimia 0.52 alizopata
Richard Minja wa Chausta.
Msimamizi wa uchaguzi huo Pudenciana
Kisaka ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa jana
alimkabidhi Mgimwa hati yake ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Godfrey Mgimwa
Akizungumza na wanahabari baadaye
Mgimwa alisema anazikumbuka ahadi zote alizotoa kwa wananchi wa jimbo
hilo wakati wa kampeni zake na anajipanga kutekeleza moja baada ya
nyingine.
“Kama mnavyojua nyingi ya ahadi hizo
zitatekelezwa kupitia Ilani yetu ya CCM; nachowahakikishia wananchi
wangu wawe na imani kwani mambo yatatekelezwa,” alisema huku
akiwashukuru wapiga kura wa jimbo hilo kwa kumpa ushindi wa kishindo
dhidi ya wapinzani wake.
Pamoja na Chadema kuleta wabunge
wake wote siku tatu kabla ya uchaguzi huo na kutumia chopa kwenye
kampeni zake kabla ya kuitumia kulinda kura siku ya uchaguzi, Mgimwa
alimgaragaza mgombea wa Chadema hata katika kata zilizokuwa zikielezwa
kuwa ni ngome ya chama hicho.
Kata hizo ni pamoja na Ifunda ambayo
Mgimwa alipata jumla ya kura 1,627 dhidi ya 601 alizopata mgombea wa
CCM na 13 za mgombea wa Chausta.
Nyingine ni Nzihi ambayo CCM ilipataa kura 1,793 dhidi ya 606 za Chadema na saba za Chausta.
Katika kata ya Magulilwa ambako
mgombea wa Chadema ndiko anakotokea, Mgimwa alifanya vizuri zaidi kwa
kupata kura 2,065 dhidi ya kura 549 za Chadema.
Matokeo ynayofana na hayo yalitokea
pia katika kata zingine zote za jimbo hilo; wakati Mgimwa akipata kati
ya kura 1,500 na 3,000, mgombea wa Chadema alipata kati ya kura 200 na
700 tu.
Grace Tendega
Tendega akizungumza na wanahabari |
Akizungumza na wanahabari nje ya
iliyokuwa kambi ya Chadema mjini Iringa ya CK Lodge, Tendega alianza kwa
kumshukuru Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine wote
walioshiriki kampeni za chama hicho.
Huku baadhi ya wafuasi wa chama
hicho wakiangua kilio alisema; “Ninawashukuru makamanda wenzangu na
wanaharakati waliokuwa wanapigania haki Kalenga, wafuasi na wanachama wa
Chadema wote, nawapa pole na hongera kwa kuanza na kumaliza uchaguzi
huu uliokuwa na dosari nyingi,” alisema.
Alisema maapambano ya ukombozi yana
changamoto nyingi na kwamba huo ni mwanzo wa safari ya mabadiliko
makubwa nchini, pale walipokesea mbele ya safari watajipanga upya.
Benson Kigaila
Kigaila akisisitiza kuyakataa matokeo |
Katika mkutano huo na wanahabaari,
Mkurugenzi wa Oparesheni wa Chadema, Benson Kigaila alisema Chadema
haiyakubali matokeo hayo japokuwa haitakakata rufaa mahakamani
kuyapinga.
Alisema daftari la wapiga kura
lililotumika katika uchaguzi huo sio la mwaka 2010 bali ni lile
walilolilalamikia awali kufanyiwa marekebisho mwaka huu.
“Kuna wapiga kura wengi waliondolewa
katika daftari hilo lakini wengine wengi wapya waliingizwa, tunao
ushahidi tuliouwasilisha kwenye kikao tulichofanya na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi,” alisema.
Alisema “ni mwendawazimu pekee ndiye
anayeweza kusema kwamba uchaguzi huu wa Kalenga ulikuwa huru na wa
haki, vinginevyo haki ya watanzania inaendelea kuporwa kwa njia ya
masunduku ya kura.”
Alisema yako mambo ya kisheria
yaliyojitokeza wakati wa zoezi la upigaji kura ambayo watataka ufafanuzi
wake kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa.
“Kuna gari na watu wetu hawajulikani
walipo mpaka sasa, kuna wafuasi wetu walikamatwa wakapigwa na kuteswa
baada ya kukamatwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM, tunataka
kujua wahusika wamechukuliwa hatua gani kwasababu wanafahamika,”
alisema.
Alisema yeye na baadhi yaa viongozi wa chama hicho hawataondoka mjini Iringa mpaka watakapopata majibu ya mambo wanayolalamikia.
Jimbo la Chalinze
Kigaila alisema wakimaliza
kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo,
mapambano yao watayaelekeza katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze.
“Kule Chalinze kampeni
zimekwishaanza; tukitoka Iringa breki yetu ni Chalinze; tutapita kijiji
kwa kijiji kuwaeleza watanzania umuhimu wa kuichagua Chadema,” alisema.
Alisema katika kampeni hiyo wimbo
wao mkubwa utakuwa ni fursa sawa kwa watanzania wote ili kuondokana na
tabia inayojengekea ya watoto kurithi nafasi za uongozi za wazazi wao.
“Wote tuna haki sawa, Chadema
tunataka kuona wakulima, walimu na watu wengine wa kawaida wanapata
fursa katika nchi hii badala ya kuendelea kutoa madaraka kwa watoto wa
wakubwa,” alisema.
CHANZO:FRANCI GODWIN
No comments:
Post a Comment