Dodoma. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Dodoma, Godfrey Mdimi Mhogolo amefariki dunia akiwa kwenye matibabu
nchini Afrika ya Kusini.
Katibu wa Dayosisi ya Dodoma, Luteni Mstaafu Daudi Kandila alithibitisha jana kutokea kwa kifo hicho na kusema kimeacha pengo kwa dayosisi na Kanisa la Anglikana kwa jumla.
Kandila alisema Askofu Mhogolo alifikwa na umauti katika Hospitali ya Mil Park iliyoko Afrika Kusini ambako alipelekwa Machi 19.
“Ni kweli Baba Askofu amefariki jana saa 6:00 mchana. Siwezi kuzungumzia suala hili zaidi kwani katibu mkuu wa jimbo ndiye atakayetoa taarifa kwa undani,” alisema Kandila.
Alisema mtumishi huyo alianza kuugua mapema mwezi Februari na ilipofika Machi Mosi, alipelekwa Hospitali ya African Medical ya Dar es Salaam ambako alitibiwa kwa siku 18 kabla ya kupelekwa Afrika Kusini.
Ugonjwa uliosababisha kifo chake Mhogolo
haujajulikana kutokana na maelezo kuwa hadi watakapopata ripoti za
madaktari juu ya nini kilikuwa kikimsumbua marehemu kabla ya uhai wake.
Mhogolo amekuwa Askofu wa Dayosisi ya Kati ya Tanganyika tangu mwaka 1999 kipindi kifupi baada ya kifo cha aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Marehemu Yohana Madinda. Katika uchaguzi uliomwingiza madarakani, alimshinda aliyekuwa Askofu Msaidizi wa wakati huo, Donald Mtetemela na kufanya aende kuwa Askofu wa Ruaha (Iringa).
Mhogolo pia aliwahi kuwa katibu wa dayosisi hiyo kabla ya kushika wadhifa huo na alifanya kazi ya kufundisha katika Chuo cha Theolojia cha Kongwa.
Katika uongozi wake, alifanikiwa kuigawa dayosisi
yake ambapo Dayosisi za Mpwapwa na Kondoa zilianzishwa. Mpwapwa akawekwa
Simon Chiwanga kuwa Askofu na Kondoa akapewa Askofu Yohana Mkavu.
Hadi mauti yanamkuta, alibakiza miezi kadhaa astaafu kwani ratiba ya kanisa inaonyesha Desemba mwaka huu ingekuwa na uchaguzi.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment