Dar es Salaam. Wakati mjadala wa
Katiba Mpya hususani muundo wa Muungano ukipamba moto, imebainika kuwa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kupendekeza kuanzishwa
Serikali ya Tanganyika, kama sharti la kuingia kwenye Shirikisho la
Afrika Mashariki.
Maelezo hayo ya Mwalimu Nyerere yapo
kwenye kitabu chake cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania
kilichoandikwa mwaka 1994 na kutolewa 1995
.
"Wakati Mwalimu anaandika kitabu hiki
mwaka 1994 taifa letu lilikuwa linakabiliwa na changamoto kadhaa za
kihistoria ambazo ndizo zilimfanya kuingilia kati na kuandika kijitabu
hiki ambacho kilikuwa kama nasaha, onyo, na usia kwa Watanzania,"
inasema sehemu ya utangulizi wa kitabu hicho.
Katika sura ya nne ya kitabu hicho,
pamoja na mambo mengine Mwalimu Nyerere alizungumzia suala la Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar ambapo alieleza sababu zilizofanya muungano wa
serikali mbili ukaanzishwa.
"Labda ni vizuri kukumbuka kwamba
shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki
ziwe nchi moja," alisema katika kitabu chake hicho.
Alieleza kuwa, wakati Zanzibar na
Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katika
mazungumzo ya kutafuta uwezekano wa kuungana.
"Kama jambo hilo lingetokea, nina
hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa
shirikisho; ama shirikisho la nchi tatu zenye serikali nne, au
shirikisho la nchi nne zenye serikali tano.
"Kwa kweli hata kesho nchi za Afrika
Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa
ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye serikali mbili ya Zanzibar
na ya Tanganyika kuliko Tanzania yenye serikali mbili, ya Tanzania na
Zanzibar," alisema.
Alisema kwa kufanya hivyo, wapendao
Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti,
wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa nchi moja, kuliko
Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.
Baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, wakizungumzia suala hilo, walisema kuwa ni vyema
kuangalia zaidi matakwa ya wananchi kuliko kujali tu mfumo.
Mmoja wa wahadhiri hao, Faraja
Christoms alisema wakati Mwalimu Nyerere akiandika kitabu cha Uongozi
Wetu Na Hatima ya Tanzania, alikuwa na hofu ya kumeguka kwa muungano.
"Wakati ule kulikuwa na wale wabunge
wa G55 jina walilobatizwa na Profesa Issa Shivji, hawa wabunge walikuwa
wanaona kama Zanzibar inapendelewa sana, walikuwa wanaona kama
wanalalamika tu kama watoto
"Lakini ukiwasikiliza na wenyewe
Wazanzibari walikuwa na hoja, waliona kama Serikali ya Muungano ndiyo
imekuwa ya Tanganyika kwa hiyo vitu vya Muungano vilikuwa vinainufaisha
zaidi Tanganyika," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo Mwalimu Nyerere alipoamua kuandika kitabu hicho.
Christoms alisema kwa mfumo wa sasa
ulivyo ni vyema maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yakaheshimiwa,
kwani hayatofautiani sana na yale ya tume nyingine zilizowahi kuundwa
kuangalia suala la Muungano.
Alisema kwa kuwa tayari Zanzibar ina katiba yake ambayo imetambua visiwa hivyo kama nchi, siyo rahisi kubadilisha hali hiyo.
"Ukisema tuendelee na serikali mbili,
kero za Wazanzibari hazitatatulika, ukitaka kulitatua hili kwanza useme
haya mambo yasiyo ya Muungano nani ayashughulikie na yale ya Tanganyika
pia yatashughulikiwa na nani?
"Mimi mwenyewe sioni kwa nini watu
waseme tukiwa na serikali tatu muungano utavunjika kwa sababu muungano
ni ridhaa ya watu, kwa sababu tayari Zanzibar ilishasema kuwa yenyewe ni
nchi, Tume ya Warioba imebeba mawazo ya watu kwa hiyo ni vyema
tukayaheshimu," alisema Christoms.
Kwa upande wake Dk Aldin Mutembi
alisema, "Mimi sijaingia ndani sana kwenye suala la serikali tatu ama
mbili, lakini naungana na maoni ya Tume ya Warioba."
Tume ya Warioba ilipendekeza kuwapo kwa serikali tatu.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk
Wetengere Kitojo alisema kuwa, mawazo ya mwalimu yalikuwa serikali mbili
kwa kuwa lengo lilikuwa katika kuelekea kwenye muungano wa serikali
moja.
Alisema kwa sasa baadhi ya watu
wanapiga kelele kutaka uwepo wa serikali mbili na wengine serikali tatu,
ingawa ndani yake wapo ambao hawautaki kabisa muungano.
"Serikali mbili ni muungano bora
zaidi, tumekuwa na mfumo huu kwa muda mrefu, lakini hatuoni kama kuna
mwelekeo wa serikali moja, ndiyo maana watu wengine wameona bora tuwe na
serikali tatu ili tupunguze kero ambazo zimeshindwa kutatuliwa kwa muda
mrefu ndani ya mfumo wa serikali mbili.
"Mimi naona cha msingi ni nia ya
dhati, wapo wanaotaka serikali mbili lakini hawana nia ya dhati ya
muungano, wapo wengine serikali tatu lakini pia hawautaki muungano.
Lengo ni muungano kamili, serikali tatu ni kurudi nyuma, ila sasa kama
kwa miaka yote tumeshindwa kufikia lengo la serikali moja wengine
wanaona bora turudi kwenye serikali tatu
Alisema kuwa, kwa mtazamo wake
serikali mbili ni bora zaidi ili baadaye iwepo moja lakini kama suala
hilo limeshindikana ni bora kuwepo na mfumo wa serikali tatu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania, Emanuel Muya alisema mazingira yaliyomfanya Mwalimu Nyerere
kuandika kitabu cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania, ni tofauti na
haya yaliyopo leo.
"Pamoja na yote bado kuna umuhimu wa
kuungana Tanganyika na Zanzibar, hakuna anayetaka kuuvunja muungano,
hata mwalimu alikuwa anataka muungano imara, alivyoondoka muungano
ulikuwa imara.
"Uwe unakubalika pande zote, kwa sasa
una matatizo pande zote, lazima tukubali kupata mazingira aliyokuwa
akiyataka Mwalimu," alisema.(E.L)
source: Fredy Azzah, Mwananchi
No comments:
Post a Comment