Dodoma. Huwezi kuzungumzia
mafanikio ya Bunge Maalumu la Katiba bila kumtaja aliyekuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Kupitia Kanuni za Uendeshaji wake, Profesa Costa Mahalu.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya gazeti hili na profesa huyo.
Mwananchi: Nini siri ya mafanikio yako katika kuiongoza Kamati ya Kanuni tena kwenye kipindi cha misukosuko mingi ya kikanuni?
Profesa Mahalu: Siri ya
mafanikio yangu ni Mungu. Nilimwomba Mungu ili aniwezeshe kuongoza
kamati yenye mchanganyiko wa wajumbe kutoka makundi mbalimbali. Pia siri
yetu ya mafanikio ni ‘teamwork’(kufanya kazi kwa pamoja) tumefanya kazi
kama timu. Baadhi ya wajumbe ninawafahamu vizuri na wengine siwafahamu
lakini Mungu mwema, tumekuwa kitu kimoja.
Tuliazimia wote kuwa kitu kimoja na kiukweli
tumeweka rekodi kubwa duniani ya kumaliza kazi ya kutayarisha kanuni za
Bunge la Katiba kwa majuma matatu. Nchi nyingine zilitumia mpaka miaka
kutengeneza kanuni tu.
Nafurahia umoja wetu na ninaamini hautaishia kwenye mchakato wa Katiba pekee.
Mwananchi: Kitu gani kilikukera zaidi wakati wa mchakato huo wa kutengeneza kanuni?
Profesa Mahalu: Mimi ni mfuasi
wa dhana ya saba mara sabini. Inawezekana kabisa lugha zilipishana
lakini tayari nimesamehe na naamini hata wajumbe wameisamehe kamati
yangu.
Mwananchi: Kipi ulikipenda sana katika kazi ile ya kutengeneza kanuni?
Profesa Mahalu: Nilipenda sana
ushirikiano niliupata kutoka kwa wajumbe wenzangu wa kamati. Mwanzoni
niliogopa kufanya kazi na watu ambao nilijua wana masilahi tofauti.
Lakini kadiri muda ulivyosonga, nikagundua kuwa wote ni wamoja, labda ni
kwa sababu wote tumetoka kwenye taaluma moja ya sheria.
Mwananchi: Nini maoni yako kuhusu kanuni
ya 37 na 38 zinazozungumzia aina ya kura ambazo kamati yako ilishindwa
kufikia mwafaka?
Profesa Mahalu: Ukiangalia kwa
jicho la sheria hakuna utata wa ufafanuzi. Kura ya siri au ya wazi zote
ni kura katika mchakato wa kidemokrasia. Lakini hilo ni suala ambalo
kamati haiwezi kufanyia uamuzi kwa kuwa bado watu wanavutana. Natoa wito
kwa wajumbe wa kamati, kuliangalia suala hilo kwa makini ili
lisitupotezee muda.
Mwananchi: Unakumbuka kusukumwa na kikundi chochote
ambacho labda kilitaka masilahi yake yaingizwe kwenye kanuni wakati wa
kuandaa kanuni hizo?
Profesa Mahalu: Hakuna kikundi
kilichotushawishi kwa namna yoyote ile. Tulifanya kazi yetu kwa uhuru,
weledi na amani kubwa. Nina hakika tumevunja rekodi ya dunia katika
kutengeneza Rasimu ya Kanuni kwa muda mfupi.
Mwananchi: Una maoni gani kuhusu tofauti za kimtazamo zinazojitokeza kwenye mchakato huo wa Bunge la Katiba?
Profesa Mahalu: Tofauti za
kimtazamo ni msingi wa demokrasia na sheria inatambua hilo. Ila katika
mchakato muhimu kama huu wa kutengeneza Katiba, lazima wanaopingana
kimtazamo wafikie mwafaka.
Mwananchi: Unatoa wito gani kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba?
Profesa Mahalu: Wito wangu ni
kuwataka tushirikiane katika kazi hii ya kihistoria. Tuache tofauti zetu
za kiitikadi tumwangalie Mungu na waja wake, raia wa Tanzania.
Nawakumbusha wenzangu kwamba Katiba
tunayoitengeneza siyo mali yetu, ni mali ya watoto na wajukuu wetu.
Mungu aliondolee Taifa letu ubinafsi, ili tuwe pamoja katika mchakato
huu wa kihistoria.
Historia yake
Profesa Mahalu alizaliwa Julai 9, 1948 katika Kijiji Cha Katunguru wilayani Sengerema katika Mkoa wa Geita.
Zamani eneo hilo lilikuwa likijulikana kama Wilaya ya Geita.
Baada ya kumaliza elimu ya msingi katika Shule ya
Msingi Geita, Profesa Mahalu alijiunga na masomo ya sekondari katika
Shule ya Sekondari Kibaha, mkoani Pwani ambako alimaliza kidato cha
nne, kabla ya kujiunga na masomo ya kidato cha tano katika Shule ya
Sekondari ya Mkwawa.
Mwaka 1971 alijiunga na mafunzo ya jeshi katika
Kambi ya Makutupora, mkoani Dodoma na baadaye mwaka 1974 alijiiunga na
masomo ya Shahada ya Kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Mwaka 1975, aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama
Mkufunzi Msaidizi katika Kitengo cha Sheria kabla hajaanza masomo yake
ya Shahada ya pili ya sheria kati ya mwaka 1976 na 1978 huku akiendelea
kufundisha.
Mwaka 1979 alikwenda Hamburg, Ujerumani Magharibi ambako alisomea na kuhitimu udaktari wa sheria mwaka 1983.
Alirudi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuendelea na kazi yake kama Mhadhiri Mwandamizi.
“Baadaye nikawa Mkuu wa Kitivo cha Sheria wakati
tayari nikiwa Profesa mshiriki. Mwaka 1990, nilikwenda Ujerumani
kufundisha na mwaka 1991 nilirudi tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama
Profesa wa Sheria, nikafanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu,
kabla sijateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu mwaka 1992 hadi 1996,”
alisema Profesa Mahalu na kuongeza;
“Mwezi Oktoba, mwaka huo huo 1996, nilihamishiwa
katika Wizara ya Mambo ya Nje na baadaye nikapelekwa Ujerumani kuwa
msaidizi wa balozi mwaka 1997. Mwaka 1999 niliteuliwa kuwa Balozi wa
Tanzania nchini Italia, kazi ambayo niliifanya kuanzia mwaka 2000 hadi
2006.”
Kwa sasa Profesa Mahalu ni Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine mkoani Mwanza.
Katika maisha anaamini katika kumcha Mungu na kuwa muwazi.
source: mwananchi
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment