Kumbukumbu za majadiliano ya Bunge
(Hansard), za Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Aprili 25-28, 1977, Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Moringe Sokoine,
ameelezea vizuri dhana na mamlaka ya Bunge Maalum la Katiba.
Kwa kuwa taifa letu kwa mara nyingine
liko kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya, na kwa kuwa Bunge Maalum tayari
limeanza vikao vyake vya kutunga Katiba Mpya hiyo mjini Dodoma, ni muhimu
tukumbushane kile alichokisema Sokoine wakati ule wa mchakato wa kutunga Katiba
hii ya sasa ya mwaka 1977.
Sokoine anasema: “Katiba ya nchi ndiyo
Sheria ya msingi kabisa kwa taifa lolote, na chombo kinachotunga Sheria hiyo,
ni lazima kiwe chombo chenye madaraka makubwa kabisa. Kwa hiyo, Bunge hili
Maalum lina madaraka kuliko Bunge la kawaida. Bunge hili linaweza kukataa au
kukubali mapendekezo haya.
“Lakini Ndugu Spika, katika kutumia
madaraka yetu, ni lazima tujue mipaka ya madaraka hayo. Mapendekezo
tutakayofikiria hivi sasa yametokana na maagizo ya Chama. Kwa busara yetu,
tumeamua, na bila kusita, kwamba Chama kitashika hatamu za uongozi wa nchi. Kwa
hiyo, Bunge hili linaweza kabisa kuyakataa ama kuyabadilisha mapendekezo ya
Serikali iwapo litaona kuwa yanapinga maagizo ya Chama. Na iwapo mapendekezo
yote yanayopendekezwa yanatekeleza maagizo ya Chama, naomba Bunge lisione uzito
wa kuyapokea na kuyapitisha bila kusita (Makofi).”
Kwetu sisi katika maneno haya ya
Sokoine tunaziona hoja kuu mbili. Kwanza ni madaraka ya Bunge Maalum la Katiba,
na pili ni mipaka ya madaraka hayo. Kwamba Bunge Maalum hili lina madaraka
kuliko Bunge la kawaida, kwa maana ya Bunge la Muungano na Baraza la
Wawakilishi. Kwamba pamoja na madaraka makubwa hayo, bado Bunge hili linahitaji
kuongozwa na busara ya kujua mipaka yake.
Bunge Maalum la mwaka 1977, mipaka yake
ilikomea kwenye mamlaka ya Chama kwa sababu wakati huo Chama, kwa maana ya CCM,
kilikuwa kimeshika hatamu za uongozi. Bunge Maalum la sasa, 2014, mipaka yake
inakomea kwenye mamlaka ya wananchi kwa sababu wananchi ndio wenye Katiba na
ndio wametoa maelekezo kwa Bunge Maalum hilo juu ya Katiba waitakayo.
Pamoja na ukweli huo, tunasikitika
kusema hapa kwamba vyama vya CCM na CHADEMA, tayari vinakwenda kinyume na
mantiki hiyo ya Sokoine. CCM imeweka msimamo kwa wajumbe wake kung’ang’ania
muundo wa Mungano wa Serikali mbili. CHADEMA nao wameweka msimamo na wabunge
wake wa kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Vyama hivyo vinataka kujipa madaraka
makubwa kuliko madaraka waliyonayo wananchi wao. Badala ya kung’ang’ania mambo
ya msingi ambayo wananchi wao wanataka yawemo kwenye Katiba Mpya yao, wao
wameng’ang’ania muundo wa Muungano wa Serikali mbili au tatu.
Linapokuja suala la kulipana posho za
vikao, vyama hivyo havionyeshi tofauti yoyote, vimeungana na kuwa wamoja. Hapo
ndipo wananchi wenye nchi yao na Katiba yao wanapovishangaa vyama viwili hivi
viwili na vingine vinavyounga misimamo hiyo, wakati kuna mambo mengi ya msingi
ndani ya Rasimu hiyo ya Katiba.
Hivi kweli wajumbe wao na vyama vyao,
wanaelewa ni nini maana ya Bunge Maalum la Katiba? Wanaelewa jukumu la Bunge
hilo? Wanaelewa Bunge hilo linawajibika kwa nani? Tunadhani, misimamo hiyo ya
CCM na CHADEMA, inalidhalilisha taifa hili.
Source:
www.raiamwema.co.tz -Godfrey Dilunga
No comments:
Post a Comment