BUNGE Maalumu la Katiba ndio limeanza
na kwa karibu miezi mitatu hivi tutashuhudia malumbano, mabishano, michango na
mijadala motomoto na mingine iliyopoa wakati wajumbe wa Bunge hilo watakapokuwa
wanapitia ibara na vifungu mbalimbali vya rasimu ya Katiba Mpya. Mwishowe,
watawaletea Watanzania Katiba inayopendekezwa ili wao wachukue uamuzi wa
kuikubali au kuikataa. Na endapo wataikubali basi Tanzania itakuwa na Katiba
Mpya miezi michache tu ijayo. Endapo hata hivyo Watanzania wataamua kuikataa
basi Katiba ya sasa itaendelea kutumika.
Katika mchakato mzima hakuna mtu ambaye
ameweka hadhi, heshima, jina, ujiko na sifa yake rehani kama Rais Kikwete.
Vyovyote utakavyokwisha mchakato huu, Rais Kikwete ama atakumbukwa kwa
kuwaachia Watanzania Katiba Mpya ambayo itadumisha taifa au anaweza kujikuta
jina lake linatajwa katika historia kama kiongozi ambaye kutokana na uamuzi
wake alisababisha taifa la Tanzania kufa.
Kikwete kama Gorbachev?
Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za
Kisovieti za Urusi (USSR) ulipata Rais wake wa mwisho chini ya Muungano huo,
ambaye kutokana na uamuzi wake alisababisha (au alichangia kwa kiasi kikubwa)
kuvunjika kwa Muungano huo. Huyo si mwingine bali ni Mikhail Gorbachev (83).
Kuna watu wanamuona Gorbachev kama shujaa na wengine wanaona kama mtu
aliyevunja sifa na taifa la Urusi kwa kuleta yale mabadiliko makubwa ya
kimfumo, utawala, kisiasa na kiuchumi.
Lakini kubwa zaidi ni kuwa ilikuwa
chini yake Urusi iliyokuwa taifa kubwa na lenye nguvu duniani ilivunjika na
kusababisha kuzaliwa kwa mataifa mengine madogo na pia kusababisha mivurugano
na hata vita katika zilizokuwa jamhuri za kisovieti. Kile kilichokuwa nia
“njema” ya kuleta mabadiliko ili kuwaingiza Warusi katika ulimwengu wa kisasa
wa demokrasia kilienda na uzuri wake na ubaya wake.
Kikwete asipoangalia – na sijui kama
kuna namna ya kubadili – kuna uwezekano kabisa kuwa mwisho wa mchakato huu wa
Katiba ama Tanzania itakuwepo au atajikuta amesababisha mvurugano mkubwa sana
baina ya watoto wa taifa hili na yeye kama Gorbachev akijikuta anabakia kupewa
tuzo, kusifiwa duniani na kuishia kualikwa kutoa hotuba za kuelezea “mafanikio”
yake.
Mchakato huu ni uamuzi wa Kikwete
Ni vizuri kukumbuka kuwa mchakato huu
wa Katiba ulianzishwa na Rais Kikwete peke yake; hakukuwa na kikao chochote cha
kiserikali au chama ambacho kilipitisha uamuzi huu. Yawezekana alishauriana na
watu wachache lakini hakuna ushahidi wowote kuwa ulikuwa ni uamuzi wa kisera wa
chama chake au serikali yake. Ni kana kwamba aliamka usiku mmoja na kuamua kuwa
ni bora awapatie wananchi Katiba Mpya kabla ya kuondoka. Uamuzi huu unaweza
ukaandikwa kama uamuzi wa kijasiri zaidi au mojawapo ya uamuzi wa kibabe
uliowahi kuchukuliwa na viongozi wetu.
Kikwete hakuwa na madaraka ya kuanzisha
mchakato wa Katiba Mpya, mojawapo ya mambo ambayo labda wanafunzi wetu wa
sheria itabidi waje kujifunza ni kuhusu madaraka ya Rais (Presidential Powers)
na mambo yale ambayo Rais pekee anaweza kuyafanya (Presidential prerogatives).
Matokeo yake ni kuwa mchakato mzima
ulikuwa umeandaliwa na kumzunguka Rais mwenyewe na sitoshangaa siku chache
zijazo mambo yakiwa magumu Dodoma, utasikia watu wanamuita Rais “aingilie
kati”!
Kuelekea Tanganyika
Sina uhakika kama Rais Kikwete alikuwa
miongoni mwa wabunge wa kundi la wabunge 55, maarufu kama G55 ambao
walijiandikisha na kuweka majina yao wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Chunya
(kabla haijagawanywa), Njelu Kasaka.
Vyovyote vile ilivyokuwa mchakato huu
umewarudisha katika kurasa za siasa za nchi yetu watu ambao walipoteza nafasi
ya kuirudisha Tanganyika kwa mbinde, mwaka 1993.
Kwa vile mchakato huu ulibuniwa vibaya
na umeendeshwa vibaya na una kila dalili ya kuleta mijadala mikali kuna
uwezekano kuwa Bunge la Katiba linaweza kujikuta linakwama na kugawanyika kwa
namna ambayo ‘magenius’ wetu hawakufikiria mwanzoni.
Sijui ni kwa kiasi gani Rais Kikwete
ataweza kuokoa hasa ukizingatia kuwa hivi sasa hakuna namna yoyote ya Rais
kuingilia mchakato huu; hawezi kuuzuia, hawezi kuwaita wajumbe na hawawezi
kuuahirisha zaidi ya kuuacha ufuate mkondo wake.
Ni kwa sababu hiyo, kama nchi na
serikali ya Tanganyika vitarudi suala kubwa litakuwa ni kwa namna gani hivyo
viwili vitaweza kuwa ndani ya Muungano na jinsi gani Watanganyika watataka
kuendelea kuwa ndani ya Muungano na Zanzibar. Kwa vile mchakato huu kuna
uwezekano utasababisha kurudi kwa Tanganyika – kama baadhi ya watu
wanavyotamani – Rais Kikwete ama atakuwa shujaa au historia itamhukumu vibaya.
Ni vizuri kukumbuka kuwa hata Urusi
ilivyogawanyika mojawapo ya matokeo yake wanasiasa wake wakajikuta wanatafuta
wapi wakagombee uongozi na wengine kweli wakapata sifa zaidi katika nchi mpya
ujiko (sifa) ambazo wasingeweza kupata ndani ya Urusi.
Hili litatokea baadaye kwani licha ya
kuwa mfumo huu utatengeneza nafasi kwa utumishi wa Serikali ya Muungano, lakini
naamini ujiko mkubwa na nguvu kubwa katika hilo Shirikisho linalopendekezwa
itakuwa ni kwa Tanganyika. Sijui ni kwa kiasi wanasiasa waliojazana bungeni
watakapokuwa wanazungumza watakuwa wanazungumza kwa ajili ya uzalendo hasa au
wakipigia hesabu ulaji mpya ambao wanajiandaa kujitengenezea!?
Vyovyote vile ilivyo, kufanikiwa kwa
mchakato huu au kuharibika kwake kutaamua kwa kiasi gani historia itamhukumu
Rais Kikwete. Anaweza akasifiwa kwa mengi katika uchumi, jamii na mengine
lakini ni hili la Katiba Mpya litaamua kwa vizazi vijavyo ni kwa kiasi gani
alikuwa kiongozi mwenye maono, mwenye kulinda taifa na ambaye aliweka maslahi
ya taifa mbele kuliko kitu kingine chochote. Kinyume cha hapo, historia
haitakuwa na huruma.
Source:
Lula wa Ndali Mwananzela
No comments:
Post a Comment