Ndugu zangu,
Jana katika nyakati tofauti nimefuatilia mjadala wa rasimu ya kanuni za Bunge hilo.
Kuna wakati nimejiuliza; hivi wote mle ndani wanajua maana ya dhamana kubwa waliyobeba kwa ajili ya nchi hii, leo na kesho?
Kwamba hawapaswi kuonyesha aibu ile ya
kujikita kwenye kujadili mustakabali wa taifa kwa kuvaa miwani ya
makundi na vyama vyao vya siasa. Kuingia kwenye ushabiki kama wa Simba
na Yanga. Maana, inahusua masuala ya msingi yaliyo mbele ya uhai wa
vyama vya siasa.
Katiba ni dira ya nchi. Ni ramani ya kutuongoza Watanzania wa leo na wajao, bila kujali makundi na vyama vya siasa.
Kwa WaTanzania, madai ya kupata Katiba
mpya ni madai halali yanayotokana pia na kukosekana kwa Haki, Uwazi na
Uwajibikaji, hususan kutoka kwa baadhi ya wenye kupewa dhamana za
uongozi.
Watanzania ni kama kisa cha wanakijiji
waliokuwa kwenye shida ya njaa ya miaka hamsini. Na katika kuhangaika
kwao,na kwa risasi yao ya mwisho waliyobaki nayo kwenye gobore moja na
la pekee kijiji kizima, wamekaa kikao na kujadili wafanyeje ili wampate
mwenzao atakayekwenda mbugani kuwinda mnyama ili aokoe njaa yao.
Na Jemedari wao, baada ya kutafakari,
amewateulia mwenzao anayedhaniwa kuwa makini na mahiri kwa uwindaji.
Mwenye uwezo wa kulenga shabaha, na hivyo, kuitumia vema risasi hiyo
moja iliyobaki kwenye kumlenga nyati na kumwangusha. Kwamba abebe gobore
lenye risasi moja, na aingie nalo msituni kuifanya kazi hiyo.
Aliyekwenda mbugani nyuma amewaacha
wengi wenye matumaini ya kuusikia mlio wa gobore utakaoshiria mnyama
mkubwa ameangushwa mbugani.
Na hakuna habari mbaya, kama
wanakijiji wale watakapousikia mlio huo na kukimbilia mbugani kujionea.
Na huko wamkute mwenzao ameitumia risasi ile ya mwisho kwa kumlenga na
kumwangusha nyani badala ya nyati waliyemtarajia!
Na kwa mila za wanakijiji wale, nyani haliwi,na ni mwiko.
Na Bunge la Katiba lijione kuwa lina
fursa adhimu ya kutimiza ndoto ya Watanzania ya kupata Katiba Bora yenye
kukidhi mahitaji ya sasa na hata miaka mia moja ijayo.
Kwa Wabunge wa Bunge la Katiba kwenda
Dodoma na kurudi na nyani badala ya nyati, sio tu kutawakatisha tamaa
Watanzania, bali, kutawafanya Watanzania wawadharau Wabunge hao na hata
kuhoji uzalendo wao kwa nchi yao waliyozaliwa.
Ni Neno Fupi La Leo.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)
Dar es Salaam.
0754 678 252(P.T)
No comments:
Post a Comment