Dar es Salaam. Wakati maombi ya baadhi
ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ya kuongezewa posho yakipingwa
kila kona, uongozi wa muda wa Bunge hilo umeunda kamati kuchunguza
uhalali wa maombi hayo.
Juzi, ndani ya kikao cha Bunge hilo,
baadhi ya wajumbe walieleza mahitaji yao ya posho kuongezwa wakisema
kiwango cha Sh300,000 (Sh80,000 za kujikimu na Sh220,000 kwa kikao),
hakitoshi
.
Baada ya maombi hayo, Mwenyekiti wa
Muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho aliahidi kuliwasilisha suala hilo
serikalini ili lifanyiwe kazi, lakini jana aliamua kuunda timu ya
wajumbe sita kuchunguza uhalali wa posho hizo.
Posho kupingwa
Baadhi ya vyama vya siasa,
wanaharakati na wananchi wa kawaida wameshangazwa na maombi hayo ya
posho, wakisema wajumbe wamesahau kilichowapeleka bungeni na kukimbilia
kutetea masilahi yao.
Vyama vya Chadema na CUF kwa nyakati
tofauti, vilisema kuwa vitaanzisha juhudi za kuwataka wabunge wao ambao
ni wajumbe wasusie agenda yoyote inayotaka kuongezwa kwa posho hizo.
Tamko la vyama hivyo limetolewa huku
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho wajumbe wake ndio wanaodaiwa kupigia
debe mpango huo, kikisema kitatoa ufafanuzi juu ya hoja hizo baada ya
kupata 'taarifa rasmi'.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa alisema jana kuwa wajumbe hao hawakupaswa kudai nyongeza ya posho
kwa vile hawakutumwa kwenda Dodoma kudai marupurupu ya fedha.
Alisema kuanza kujadili suala la
nyongeza ya posho badala ya kuzungumzia hoja za msingi zilizopo kwenye
Rasimu ya Katiba, ni sawa na kuwapuuza wananchi ambao wanasubiri kupata
Katiba Mpya.
"Wametoka kwenye hoja na kutupeleka
kwenye mambo mengine ambayo hayana msingi wowote. Sisi kama Chadema
tunapinga na tunataka wabunge wetu watambue hilo," alisema.
Alisema wale wanaolalamika kwamba
Sh300, 000 hazitoshi wanajaribu kupindisha ukweli, kwani kuna baadhi ya
watumishi wa Serikali wanalipwa kiasi hicho ikiwa ni mshahara wao wa
kila mwezi.
Alisema Chadema kimewataka wabunge
wake kutojiingiza kwenye malalamiko hayo badala yake wazingatie kile
walichotumwa na wananchi kwenda Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius
Mtatiro alisema amesikitishwa na maombi hayo ya posho na kuahidi
kuanzisha kampeni ya kuyakwamisha kwa sababu hayana tija kwa wananchi.
"Tunafahamu kuwa kuna njama zinapangwa
ili wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waongezewe fedha zaidi, binafsi
na wenzangu wengi tumepanga kutumia kila uwezo kuzuia nia hiyo ovu.
Ifikie wakati tuambiane ukweli, vinginevyo nchi hii watu watakufa
maskini," alisema Mtatiro ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo.
"Sh300,000 tunazopewa kwa siku
zinatosha kabisa, ambaye hazimtoshi aongeze za kwake na ambaye anaona
hawezi kuongeza fedha zake aondoke Dodoma ili kupisha wanaoweza kutunga
Katiba waendelee." Alipotakiwa kutoa msimamo wa CCM kuhusiana na hatua
hiyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema:
"Sina chochote cha kuzungumza sasa hadi pale nitakapoletewa taarifa
rasmi kwani siwezi kufanya kazi kupitia magazeti."
Akizungumzia posho hizo, Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipinga madai kwamba
viwango vilivyotangazwa vya wajumbe wa Bunge la Katiba (Sh300, 000) kwa
siku ni pungufu kwa vilivyotolewa kwa wajumbe wa Tume.
Bila ya kutaja kiwango alisema: "Ninachofahamu, posho ya wajumbe wetu ilikuwa chini ya hiyo."
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya tume hiyo, zinaeleza kuwa wajumbe hao walikuwa wakipokea Sh200,000 kwa siku.
Kuhusu madai kwamba kazi inayofanywa
na Bunge Maalumu la Katiba ni nzito kuliko iliyofanywa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Warioba alisema hawezi kupima uzito wa kazi ya
Tume kwa kuilinganisha na inayofanywa na Bunge la Katiba na hafahamu
waliotoa madai hayo wametumia utaalamu gani
Kamati yaundwa
Kutokana na kupanda kwa joto la posho
hiyo, jana asubuhi, Kificho alitoa maelezo kwa wajumbe kuwa uongozi
unatafakari namna bora ya kuwafanya wajumbe waishi kwa amani mjini
Dodoma.
"Kwanza tulikubaliana kuwa kikao
kianze leo (jana) saa nne asubuhi, lakini tumechelewa kwa sababu muhimu,
kwani lazima mtambue kuwa kila jambo mnalozungumza hapa halitupwi kama
jiwe," alisema Kificho na kuongeza:
"Mlinituma tuzingatie namna gani
tutakaa Dodoma kwa amani, ili tuweze kumudu na kuishi vizuri katika kazi
hii nzito iliyoko mbele yetu."
Alisema kuwa walikuwa wameshauriana na
wataalamu wake ambao ni makatibu na kukubaliana kuunda timu ya
kufuatilia na kuishauri Serikali jinsi ya kuongeza posho hizo
Aliwataja walioteuliwa kuunda timu
hiyo kuwa ni, William Lukuvi, Mohamed Aboud Mohamed, Freeman Mbowe, Paul
Kimiti, Asha Bakari na Jenister Mhagama.
Wakati akiitangaza timu hiyo
iliyopaswa kuanza kazi yake jana, jina la Lukuvi ambaye pia ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) lilizua kelele
kutoka miongoni mwa wajumbe wakipinga uteuzi wake.
"Hatufai huyo, hatufai huyo, hilo jina
liondoeni na kulitupa kapuni kwani mbona wapo wengine, kwa nini
mkaingiza jina la Lukuvi?" zilisikika sauti za juu kutoka ndani ya
ukumbi, lakini lilipotajwa jina la Mhagama wajumbe wengi walishangilia.
Imeandikwa na George Njogopa, Editha Majura na Habel Chidawali
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment