Yakimbilia Bagamoyo kuiwinda Mbeya City, Kiiza arejea
Yanga
Kikosi cha Yanga juzi kilijikuta kikipata sare ya tatu msimu huu baada ya kutoka suluhu na mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuuachia uongozi wa ligi kwa 'Wanalambalamba' Azam FC ambao juzi walichomoza na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers.
Mara nyingi Yanga huweka kambi yake Bagamoyo kila inapokabiliwa na mechi dhidi ya watani zao Simba lakini wakati huu sare dhidi ya Coastal na ugumu wa Mbeya City ambayo hadi sasa haijapoteza mechi hata moja, imeonekana kuichanganya.
Yanga ilirejea jijini Dar es Salaam jana mchana ikitokea Tanga na kuingia kambini moja kwa moja kujiandaa na mechi hiyo ya Jumapili.
Hata hivyo, faraja kubwa kwa Yanga ni kupona kwa mshambuliaji wao Mganda Hamis Kiiza ambaye aliikosa mechi dhidi ya Coastal juzi.
"Kwa sasa timu iko kambini Bagamoyo kwa kujiweka sawa kabla ya mchezo wetu unaofuata dhidi ya Mbeya City. Ni mechi nyingine ngumu kwetu ndiyo maana tumeona ni vyema tuweke kambi kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili," alisema ofisa mmoja wa Yanga huku akiomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa klabu hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Daktari wa Yanga, Juma Sufiani, alisema Kiiza ambaye alikuwa anasumbuliwa na malaria ameshapona na wakati kikosi cha timu hiyo kikiwaTanga alikuwa ameanza kufanya mazoezi mepesi.
Daktari huyo aliwataja wachezaji wengine waliokuwa majeruhi lakini sasa wamepona ni pamoja na Hassan Dilunga, Salum Telela na Shaaban Kondo.
"Wagonjwa wote wamepona na naamini wataweza kucheza mechi inayofuata endapo kocha ataamua kuwapanga," alisema daktari huyo wa Yanga.
Mabingwa hao watetezi wa ligi pamoja na Mbeya City wote watashuka dimbani Jumapili wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare katika mechi zao zilizopita.
Mbeya City yenye rekodi ya kutofungwa tangu ilipopanda daraja msimu huu, juzi ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya 'Maafande' wa Ruvu Shooting katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Baada ya mechi ya Jumapili, ligi itasimama kwa wiki moja kwa ajili ya kuwapisha wawakilishi wa Bara, Yanga na Azam wanaoshiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF)
Yanga itawakaribisha Komorozine ya Comoro katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika Jumamosi Februari 8 na Azam watakuwa wenyeji wa klabu ya Fereviario de Beira ya Msumbuji kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho siku inayofuata.
Wakati huo huo Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema macho yake sasa anayaelekeza katika mchezo huo dhidi ya Mbeya City.
Pluijm aliliambia NIPASHE jijini Tanga juzi, kuwa amewasihi wachezaji wake wasahau yaliyotokea Tanga ili waelekeze akili na nguvu zao katika mechi inayofuata.
“Tulipoteza mechi kipindi cha kwanza tuliposhindwa kupata bao licha ya kutengeneza nafasi nyingi. Kipindi cha pili tulishindwa kucheza mpira mzuri kutokana na upepo mkali,”alisema.
"Hatuna budi kusahau yaliyotokea hapa (Tanga) ili mipango yetu ijikite katika mchezo wetu unaofuata. Nimeambiwa tutacheza dhidi ya timu nzuri ambayo haijapoteza mechi," alisema zaidi raia huyo wa Uholanzi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment