KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), inatarajiwa kukutana mjini Dodoma Jumapili wiki hii, huku Baraza
la Ushauri linaloundwa na marais wastaafu, likitarajiwa kuwasilisha
taarifa ya hali ya chama hicho. (HM)
Habari za kuaminika zilizopatikana
kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya CCM, zinasema Baraza la Ushauri,
linaloundwa na marais wastaafu, linatarajia kutoa tamko zito kutokana na
mwenendo unaoonyeshwa na makada wake.
Baraza hilo, linaundwa na wenyeviti na
makamu wastaafu wa chama, likiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais mstaafu
Ali Hassan Mwinyi na Katibu wake ni Pius Msekwa.
Wengine ni Rais mstaafu Benjamin
Mkapa, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid
Karume na Waziri Mkuu mstaafu, John Malicela.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada
ya kuibuka malumbano yanayowahusisha makada wa chama hicho wanaotajwa
kuwania mbio za urais mwaka 2015 kuanza harakati mapema.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika
kutoka CCM, kiliiambia MTANZANIA kuwa kikao cha CC, pamoja na mengine,
kitatoa dira ya chama na kuweka mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015.
"CC itakutana Februari 9, mwaka huu
kati ya mjini Dodoma au Dar es Salaam, lakini katika kikao hicho wajumbe
wa Baraza la Ushauri la chama watakuwepo.
"Sijui watazungumza nini katika kikao
hicho, huenda ikawa haya mambo yanayoendelea ndani ya chama hivi sasa,
kwani tambua wajumbe wa baraza wanaweza kuomba kukutana na CC au NEC
wakati wowote pale wanapoona inafaa," kilisema chanzo hicho.
Katika siku za hivi karibuni, makada
wa CCM wameibuka na kuunga mkono hatua ya Katibu wa Uhamasishaji wa
Chipukizi, Paul Makonda, ambaye alimtuhumu Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, kuwa ameanza harakati za kuwania urais.
Baada ya kauli hiyo, Malecela naye aliibuka na kuutaka uongozi wa CCM kumchukulia hatua Lowassa.
Malecela alidai, Lowassa anakiyumbisha chama hicho kutokana na kampeni za kutaka kuwania urais wa 2015.
Alisema Sekretarieti ya CCM inapaswa
kuwachukulia hatua kali makada wanaojipitisha maeneo mbalimbali nchini
kwa nia ya kusaka urais, kabla ya chama hicho kupanga muda.
Chanzo:
mtanzania
No comments:
Post a Comment