MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemjibu Rais Jakaya Kikwete kwamba
asiingize utani katika masuala mazito ya taifa. (HM)
Mbowe alisema Katiba ya Tanzania,
itaamuriwa na wananchi wenyewe na si Chama Cha Mapinduzi (CM) ambacho
kimekuwa na mkakati mkali wa kutaka kuua maoni ya wananchi.
Mbowe ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku
moja tu baada ya Rais Kikwete kudai amesikia kiongozi huyo wa upinzani
akitangaza kutumia nguvu kupata Katiba mpya.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi
kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, wakati akihutubia sherehe za
miaka 37 ya kuzaliwa CCM. Alisema amesikitishwa na kauli hiyo na
kuwataka Watanzania kutobabaishwa.
Kikwete alisema Katiba mpya itapatikana kwa hoja za kila upande kulingana na mapendekezo yake.
Akizungumza jana, Mbowe alisema Rais Kikwete hapaswi kuchukulia utani katika mambo mazito ya taifa.
"Namuomba Rais Kikwete asichukulie
utani mambo ya taifa suala la Katiba mpya. Anapaswa kuzungumza mambo ya
msingi ambayo yanaleta tija.
"Siku zote Katiba ya nchi inapatikana kwa dhamira nzuri lakini tumebaini wenzetu hawa CCM hawaheshimu hoja za wananchi.
"Hebu tujiulize jinsi Jaji Joseph
Warioba alivyotumia fedha nyingi kukusanya maoni ya Watanzania, leo CCM
hao hao wanayakataa tuwaeleweje?" alihoji Mbowe.
Alisema Jaji Warioba ametoa hoja za msingi lakini kwa sababu ya uoga wa CCM wanataka kupindisha ukweli wa mambo.
"Mzee wa watu huyu amezunguka taifa
zima kwa fedha za walipa kodi wa nchi hii, sasa wanataka watumie wabunge
wao kukwamisha mchakato huu,"alisema Mbowe.
Alisema kama utawala wa Rais Kikwete
utashindwa kuleta Katiba mpya ambayo inakidhi matakwa ya Watanzania, wao
wataendelea kudai utawala mpya utakapoingia madarakani uwe ni wa
Chadema au CCM.
"Nawahakikisha Watanzania, ikija
Katiba mbaya tutaendelea kuidai kwa nguvu zote iwe CCM imeingia
madarakani au sisi, Kikwete awe madarakani au asiwepo hatulali kamwe.
"Katiba ni maridhiano ambayo yanabeba maoni ya Watanzania sasa kwa nini CCM hawataki kuyafuata?" alihoji Mbowe.
Alisema CCM haina hatimiliki ya Katiba mpya na kwamba wakati wa kufanya uamuzi mgumu wa kupindisha maoni ya Watanzania umefika.
"Hawa watu hawana hatimiliki ya Katiba
mpya, kwa nini wanajawa uoga kiasi hiki? Wanaogopa serikali tatu,
nakwambia sitaki utani kwenye ya msingi,"alisema Mbowe.
NJE YA BUNGE
Mbowe alisema atahakikisha wanajadiliana vya kutosha ndani ya Bunge kuona haki inatendeka.
"Tutabishana kwa kila namna ndani ya
Bunge,wakituzidi kete kwa rafu zao bungeni tutarudi kwa wananchi
kuwashitaki maana hawa ndiyo walengwa... hatutaki kufika huko kama kila
mtu ataweka busara zake chini.
"Dhamira ya CCM ndiyo inatufanya tutoe
kauli hizi lakini nakwambia hapa hakuna mcheza ngumi... hoja ndiyo
jambo la msingi tu,tutatumia maandamano nchi nzima maana haya ni haki ya
msingi ya kila mtu,"alisema Mbowe.
Chanzo: mtanzania
No comments:
Post a Comment