WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, February 13, 2014

Kingunge:Ushabiki uachwe suala la Katiba mpya

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru
Jumatano iliyopita mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru ktika mahojiano maalum na NIPASHE kupitia safu ya makala alizungumzia umuhimu wa mwanachama yoyote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anayetaka kugombea urais  kujitokeza mapema ili watu wamjue na kwamba kwa kufanya hivyo sio kosa.
Kauli hiyo inaweza isieleweke sana kwa viongozi wa juu wa CCM, ambao mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza kwamba hakuna mwanachama yoyote anayeruhusiwa kujitokeza kwa sasa kutangaza kugombea urais ifikapo mwakani.

Leo Kingunge anazungumzia umuhimu wa Tanzania kupata Katiba mpya iliyo bora ambayo itasaidia kutatua kero ambazo zimekuwa zikilikumba taifa kwa miaka zaidi ya 50 tangu upatikane Uhuru.

Mkongwe huyo wa sisasa hapa nchini anasema yapo mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuwamo kwenye katiba mpya ijayo.

Mchakato wa kupata Katiba mpya unaendelea na wiki ijayo rasimu ya pili itaanza kujadiliwa na Bunge maalum la Katiba mjini Dodoma.

Kingunge anasema kunahitajika busara, weredi na uvumilivu katika kuijadili rasimu ili wabunge waweze  kuipatia Tanzania Katiba iliyo bora itakayosaidia kizazi cha sasa na kijacho.

Anasema anasema mjadala juu ya Katiba mpya haupaswi kufanywa kwa jazba, ushabiki wa kisiasa, kidini au ukabila badala yake ufanywe kwa umakini mkubwa ili kusaidia kupatikana kwa majawabu ya yale ambayo yamekuwa au yanaonekana ni mapungufu ndani ya Katiba iliyopo sasa.

"Kubwa ipatikane Katiba  mpaya iliyo bora  itakayoimarisha na itakayosaidia kuujenga umoja, amani, utulivu, mshikamano na udugu wetu ambao kwa takribani miaka  50 tangu Tanzania kuwa Jamhuri ya Muungano umekuwa ukizingatiwa," anasema.

Anasema hakuna ubishi kwamba kuna mapungufu makubwa katika  Muungano uliopo na ndani ya Katiba ya sasa, hivyo ni vyema mapungufu hayo yakarekebishwa pamoja na kuyapa uhai mapendekezo mapya kwa manufaa ya taifa.

Kingunge anasema mawazo mapya yaliyosahaulika katika Katiba ya sasa ni muhimu yazingatiwe ili mradi yana manufaa kwa taifa.

"Matatizo ya msingi yapo na kama Katiba itakuwa kimya katika mambo hayo haiwezi kuwa bora, mfano makundi yasiyo na uhakika kuwamo kwenye mkondo wa maendeleo kama Wafugaj na Wahamaji, inayowahusisha Wamasai, Wabarbaig, Wasukuma na hata Wanyamwezi wanaohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta chakula cha mifugo yao.

Anasema kundi hili limekuwa wahanga na kutengwa badala ya kusaidiwa kuwawekea miundo mbinu itakayowafanya wafanye shughuli zao kwa ufanisi na kupata maendeleo na kuwaepusha kuingia kwenye mizozo ya mara kwa mara dhidi ya wakulima.

"Rasimu ya Katiba ya sasa haielezi namna ya kutatua migogoro na mauaji ya wafugaji na wakulima badala yake imejikita kwenye masuala ya vyeo na mgawanyo wa madaraka tu, yaani ulaji wakati mambo kama haya yanapaswa kuainishwa mapema, suala la wavuvi wadogo au wakulima wadogo. Tunakimbilia wakulima wakubwa kupitia Kilimo Kwanza, wakati watu wanaolisha taifa kwa kutumia jembe la mkono wamesahauliwa," anasema Kingunge

Anasema tangu uhuru vita vya wakulima na wafugaji imekuwa ikitokea, lakini utatuzi wake umekuwa wa kisiasa na kushindwa kumalizika, kitu anachotaka katiba mpya ijayo iweke bayana hilo ili kufanya makundi hayo kufanya shughuli zao na kujiletea maendeleo huku watoto wa jamii ya wafugaji wahamaji wanapata nafasi ya kusoma na kinamama kupata haki zao za ndoa.

"Katiba ikiwa wazi katika suala la makundi kama hayo hata suala la uharibifu wa mazingira utapatiwa ufumbuzi kwa sababu mfugaji anapohama na mifugo yake anasababisha uharibifu mkubwa wa ardhi, je wafanyeje na wakati ni lazima wawapatie mifugo yao vitu hivyo ili wasife....ni Katiba pekee yenye majiu hayo," anasema.

Kingunge anasema ni lazima mjadala wa Katiba mpya upewe nafasi pana na kuwaachia wananchi kujiamulia mambo yao na hasa kwenye suala la mfumo wa serikali tatu, badala ya Tume na wanasiasa kuanza kuwajibia wananchi.

"Tume imefanya kazi kubwa katika kukusanya maoni na mapendekezo yaliyozalisha rasimu mbili tofauti za katiba, lakini bado haiwezi kuwa kama kipaza sauti cha kuwasemea wananchi juu ya mfumo gani wa Muungano wanaoutaka katika Katiba hiyo," anasema.

Anaongeza kuwa hakubaliani na mfumo uliopendekezwa ndani ya rasimu ya Katiba serikali tatu kwa maana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar.

Anasema watanzania wanapaswa kujifunza kwa mataifa kama Marekani, India, China na kwingine yenye kuundwa na mfumo wa muungano jinsi yanavyokuwa wazalendo katika utaifa wao kuliko umajimbo au nchi zilizochangia kuunda mataifa hayo.

Anasema matatizo ya Muungano yaliyopo sasa yanachangiwa na uzembe wa viongozi wenyewe kwa kunyamazia izkiwamo baadhi ya kero zinazopigiwa kelele huku akihoji kwa mfano serikali ya Jamhuri ilikuwa wapi wakati Zanzibar wakipitisha katiba yao inayokinzana na ile yao na kuja kuibuka sasa baadhi ya wanasiasa kuliona hilo.

Kingunge anasema anaamini watanzania wakikaa chini na kujadili kwa kina mambo yao wanaweza kupata Katiba mpya itakayowapa nafasi kuendelea kufurahia amani, utulivu na undugu wao vinginevyo watu wakiendesha mambo kwa ushabiki na tamaa ya maslahi yao taifa la Tanzania litaangamia na kuja kujuta baadaye.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment