WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, February 3, 2014

Ngumi hazitatoa katiba mpya, asema Kikwete

  Wajumbe Bunge la Katiba leo au kesho
  Bunge kuanza wiki ya tatu mwezi huu

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiinua juu mfano wa Jembe na Nyundo alama inayotumiwa na chama hicho katika kilele cha sherehe zake za kutimiza miaka 37 iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Mbeya jana.
Rais Jakaya Kikwete amasema Katiba mpya haitapatikana kwa kupigana ngumi bali kwa wajumbe wa Bunge la Katiba kujenga hoja zitakazowezesha Taifa kupata Katiba nzuri.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati akihutumia mamia ya wanachana na wananchi katika maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Alisema anashangazwa na kauli za baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaowaeleza wananchi kuwa watatumia ngumi, mieleka na virungu iwapo baadhi ya vifungu vitaondolewa kwenye rasimu ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Wapo wanaosema hakuna mazungumzo mkibadili tutapigana, kazi ya Bunge hili ni kujadili kipengele kwa kipengele, watabadili wanalotaka libadilike, wataongeza ambalo Tume hawakuweka, kinachotakiwa ni maridhiano ya wabunge na si kupigana ngumi bali ni kura za kuongeza na kupunguza vifungu,” alisema na kuongeza:

“Tusiwatishe watu, tusiwazuie watu kusema Bunge lile kazi yake si kupiga kura ya ndiyo bali mjadala na ndiyo maana zimewekwa siku 90 za majadiliano kwa kujadilina na kukubaliana kwa kuwa wao ndiyo kikao cha mwisho.”

Rais Kikwete alisema ni vyema kila upande utumie hoja zenye nguvu, ushawishi na mashiko ili kufanikiwa kuungwa mkono na upande wa pili na sikutukanana.

Alisema amesikitishwa na kauli ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuwa watatumia hata ngumi ili kupatikana kwa serikali tatu.

Alisema jambo la wengi haliwezi kwisha kwa ngumi na kwamba hakuna refarii wa ngumi na kwamba Bungeni mwamuzi ni kura pekee kwa kujenga hoja zenye ushawishi kwa kuongeza umahiri wa kushawishi watu.

Alisema kutumia nguvu hakutasaidia na hakuna Katiba iliyotungwa kwa mtu kumshinda mwezake kwa ngumi.

Rais Kikwete alimtaka Mbowe atambue kuwa ugomvi ukitokea bungeni wakati wa mjadala wa katiba hautaleta
jawabu, bali utavuruga mambo na chama chake pia kitaathirika kwa kuwa katiba ya sasa ndiyo itaendelea kutumika pamoja na magumu yake.
Alifurahi kutokana na makubaliano ya vyama vya  siasa kwamba Alhamisi wiki hii watakutana kuweka mambo sawa kabla ya Bunge la katiba kuanza.

BUNGE LA KATIBA WIKI YA TATU FEBRUARI
Katika hotuba hiyo ambayo alitumia kuhutubia Taifa, alisema Bunge la Katiba linatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi huu, kwani  maandalizi ya ukumbi yatakamilika Jumatatu ijayo na ameongeza kati ya siku tano hadi saba ili kujihakikishia kila kitu kiko sawa kabla Bunge kukutana Dodoma.
Alisema bunge hilo litakaa siku 90 kujadiliana na kukubaliana, kubadili au kuongeza kifungu chochote hata kama tume haikukukiweka kwenye rasimu.
WAJUMBE KUJULIKANA LEO AU KESHO

Katika hotuba hiyo alisema kazi ya kuteua wajumbe 201 imekamilika na kilichobakia ni kuhariri majina leo na ikiwezekana leo au kesho atayatangaza.
Hata hivyo, alisema haikuwa kazi rahisi kwani majina yalikuwa ni mengi na nafasi chache.

“Watu walinitumia meseji Mzee usiniache Bunge la katiba. Kama huko haiwezekani basi hata nafasi mbili zilizobaki Bunge la kawaida,” alisema Rais Kikwete.
Alisema watafuata ushauri wa wanasheria ili wafanye marekebisho na kutangaza siku ya Bunge hilo kuanza na kwamba kati ya leo au kesho atatangaza siku ya Bunge la Katiba.
“Tunataka tupate Katiba inayoiimarisha Muungano badala ya kuudhoofisha au kuubomoa, amani na utulivu wa nchi, mazingira mazuri ya kuongeza zaidi kasi ya kujiletea maendeleo kwa Tanzania,”alisema.

MUUNGANO

Alihadharisha kuwa muundo wa Muungano utaleta mvutano katika Bunge hilo na kuwa kutakuwa na mjadala mkali juu ya mfumo upi ulio bora kati ya serikali mbili au tatu.

Alisema wapo wanaoilaumu CCM kwa sera yake ya mfumo wa serikali mbili, aliwataka wasioutaka mfumo huo wasiwatukane bali wajenge hoja ili wawaunge mkono katika hoja yao ya mfumo wa serikali tatu.

“Wana- CCM wanaotaka serikali mbili wawaridhishe wanaotaka serikali tatu, wasikae na kusema hao wa Serikali tatu ni wapinzani, mawazo hayapigwi rungu bali yanashindwa kwa mawazo yaliyo bora zaidi,” alisema na kuongeza:

“CCM wanasema serikali mbili, Chadema serikali tatu na na CUF wanalaani serikali tatu na hakuna aliliye na hakika.”

“Katika mazingira hayo ndiyo mana nilipendekeza wakutane…bahati nzuri baada ya majadiliano ya vyama wamekubalina kukutana Februri 06, mwaka huu, vyama vizungumze jambo letu, tunazungumzia hatima ya nchi lazima tulimalize vizuri,” alisema.

CCM NA FEDHA CHAFU
Akizungumzia maendeleo ya CCM na maadhimisho ya miaka 37 , Kikwete alisema kukosekana kwa miradi ya maedeleo ndani ya chama hicho kumesababisha viongozi kukubali fedha chafu bila kuhoji watoaji wake.

Alisema Oktoba, mwaka 2006 walianzisha mradi wa kuimarisha chama ukiwa ni wa tatu, malengo na madhumuni yake yanatekelezwa kwa ukamilifu.
Aliwakumbusha wanachama wake kuwa uhai na maenedeleo ya CCM sasa kwa miaka mingi yametegemea ufanisi wao katika utekelezaji wa mradi wa tatu wa kuimarisha chama, kwani ndiyo utawahakikishia ushindi katika  uchaguzi wa serikali  za mitaa wa wmaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
MAWAZIRI MIZIGO

Akizungumzia kuhusu suala la mawaziri ambao waliitwa mizigo na CCM kubakia ndani ya baraza lake jipya alilolitangaza hivi karibuni, Rais Kikwete aliwakingia kifua na kushangazwa na malumbano yanayoendelea ndani ya jamii ya kutaka wafukuzwe kazi.

Alisema hatua ya kuitwa kwao katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya CCM, inatokana na hoja zilizoibuka kwa wananchi na sasa wamepewa maelekezo huku wakifuatiliwa juu ya utekelezaji wa maagizo ya chama.

Alisema mawaziri hao waliitwa na kuhojiwa kutokana na kasoro ambazo zilizobainika ndani ya Serikali na kudai kuwa CC  inaendelea kufuatilia utendaji wao na ikiwa haijaridhika itatoa mapendekezo tena kwa mamlaka ya uteuzi ili ichukue hatua.

Rais Kikwete alisema kwa kufanya hivyo Kamati Kuu imetimiza wajibu wake, hivyo Serikali ndiyo iliyobaki na wajibu wakufanyia kazi mapendekezo yote ambayo yalitolewa na chama.

Alisema kuwa Kamati Kuu haina mamlaka ya kuwafukuza mawaziri, bali wajibu wake ni kutoa mapendekezo kwa Serikali hivyo Serikali itaendelea kufanya kazi ya kutekeleza mapendekezo yake.

Alisema amewaacha mawaziri hao kwa sababu maalum na kuwa ikiwa utendaji kazi wao hautaridhisha anaweza kuchukua maamuzi mengine baadaye.  

CCM NA RUSHWA
Kwa upande mwingine Rais Kikwete alitaka kuondokana na  dhana potofu kwamba uongozi ndani ya chama chake unapatikana kwa kutoa rushwa.
“Tusiache ikajengeka dhana potofu kwamba ukitaka uongozi kupitia CCM ni lazima uwe na uwezo wa fedha, kuhonga watu ndani ya chama na nje ya chama, tusikubali kuacha chama chetu kifikishwe  hapo,” alisema Rais Kikwete.

Aligiza wanachama wanaofanya vitendo hivyo vya kutoa rushwa pamoja na mawakala wao wadhibitiwe na kamati ya maadili ili kuhakikisha chama kinafuata misingi ya maadili.

Imeandikwa na Salome Kitomari Dar; Emmanuel Lengwa na Mary Geofrey, Mbeya
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment