Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ametangaza kuwa Bunge Maalumu la Katiba litaanza Februari 18 mwaka huu huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuweka mbele masilahi ya Taifa na siyo ya vyama vyao.
Rais Kikwete alisema wajumbe 640 wa Bunge hilo
wengi ni wafuasi wa vyama vya siasa, hivyo wanatakiwa kukubaliana kwa
hoja badala ya kila upande kuvutia kwake.
Aliwaonya pia wanasiasa kutokazania suala la
muundo wa Muungano peke yake, bali waangalie na masuala mengine yaliyomo
kwenye rasimu hiyo ambayo ni muhimu kwa Taifa.
Bunge la Katiba linafanyika baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake ya miezi 20 kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya pili Katiba ambayo ilitolewa Desemba 30, mwaka jana.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa vyama hivyo jana katika mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Rais Kikwete alisema kama wanasiasa wakikubaliana, hakuna mwananchi yeyote atakayepinga uamuzi utakaopitishwa na Bunge hilo.
“Nimeshauriana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein kuwa Bunge Maalumu la Katiba lianze vikao Februari 18,
mwaka huu. Bunge hili litafanyika kwa siku 70 na kama mambo yatakuwa
hayajamalizika zinaweza kuongezwa siku 20,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: “Nyinyi ndiyo wenye jukumu la kuipatia nchi yetu katiba nzuri inayojali masilahi ya watu wake ndani ya pande zote za Muungano, kuanzia watu wanapoishi, wanapotoka na asili yao. Msije mkafanya uamuzi utakaowaingiza katika uadui na chuki.”
Katika hotuba yake ya dakika 70, Rais Kikwete
alisema yapo mambo mengi ya kujadili katika Bunge hilo, siyo muundo wa
Muungano pekee.
“Mnakwenda kuijadili Katiba kuhusu masuala mbalimbali yenye masilahi ya nchi yetu, siyo mambo ya Muungano tu. Wekeni utaratibu ili muweze kukubaliana hata katika masuala ambayo kila mmoja ana msimamo wake,” na kuongeza:
“Kuna suala la ukomo wa kugombea ubunge kuwa
vipindi vitatu. Hii maana yake ni kuwa kama
umeshakuwa mbunge kwa vipindi vitatu huwezi kugombea hata urais,” alisema na kuongeza;
umeshakuwa mbunge kwa vipindi vitatu huwezi kugombea hata urais,” alisema na kuongeza;
Kwa mujibu wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, Ibara ya
75 (e) mgombea urais alitakiwa kuwa na sifa za kugombea ubunge, ikiwamo
ya kutowahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu. Hata hivyo kwenye Rasimu ya
Pili itakayojadiliwa na Bunge hilo, ibara ya 79 inayozungumzia sifa za
kuwania urais, hailazimishi mgombea urais kuwa na sifa za kuwania
ubunge.
Rais Kikwete alisema wanasiasa wana dhamana ya
kuwapatia Watanzania Katiba itakayodumu kwa miaka 50 ijayo na kuimarisha
Muungano, umoja, amani na utulivu, siasa safi na kuongeza kasi ya
maendeleo na ustawi wa wananchi.
“Mnatakiwa kuisoma vizuri Rasimu ya Katiba na kujua yaliyopendekezwa na wananchi. Chambueni kinachofaa na kisichofaa lakini kwa kuzingatia masilahi ya Taifa na siyo na vyama vyenu,” alisisitiza Rais Kikwete.
Alisema mafaniko ya mchakato wote wa Katiba yanategemea kauli, mwenendo na matendo mema ya vyama vya siasa.
“Vyama vya siasa vinatakiwa kujenga na siyo kubomoa. Mkiamua Katiba Mpya ipatikane tutaipata, mkiamua isipatikane hatutaipata. Katiba Mpya ni kwa masilahi ya watu wote,” alisema na kuongeza;
“Siyo lazima wazo la chama fulani lipitishwe, vyama vinatakiwa kutambua kuwa wapo wenzao wenye mawazo mazuri kuliko wao. Siyo kila unachokitaka wewe na wenzako wanataka hicho hicho. Muongozwe na nguvu ya hoja siyo hoja za nguvu zilizotolewa na mjumbe wa chama chako.”
Alisema kuwa lengo lake siyo kuwazuia wajumbe kutoka vyama vya siasa kutoa maoni katika Bunge hilo. Lengo ni kuwakumbusha kuwa msimamo wa chama fulani kuhusu jambo lolote, usigeuzwe kuwa amri ndani ya Bunge hilo.
“Itakuwa aibu kwa chama kwenda katika Bunge bila kuwa na msimamo wake lakini pamoja na hali hiyo, mtakuwa tayari kusikiliza mawazo ya wenzenu?” alihoji Rais Kikwete.
Uteuzi wa wajumbe
Rais Kikwete alisema leo atatangaza majina 201 ya wajumbe wa Bunge hilo kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Akizungumzia uteuzi huo alisema, “Majina yaliyowasilishwa na makundi hayo yalikuwa 3,774. Kazi ya uteuzi imeshakamilika na kilichobaki sasa ni kuhakiki tu majina, kuangalia uwiano wa wajumbe kimkoa na jinsia.”
Alisema taasisi zisizo za kiserikali zilizoomba zilikuwa 1,647 na wameteuliwa watu 20, taasisi za dini waliomba 329 na kuteuliwa 20, vyama vya siasa waliomba 198 na kuteuliwa 42, taasisi za elimu waliomba 130 na kuteuliwa 20, makundi ya walemavu waliomba 140 na kuteuliwa 20.
Wengine ni vyama vya wafanyakazi waliomba 102 na kuteuliwa 19, vyama vya wafugaji wameomba 47 na kuteuliwa 10, vyama vya wavuvi waliomba 57 kuteuliwa 10, vyama vya wakulima waliomba 157 kuteuliwa 20 na makundi yenye mrengo unaofanana walioomba 727 na kuteuliwa 20.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Alisema jambo jingine muhimu ambalo Serikali inaendelea kulifanya kazi ni kuboresha muundo wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ili iweze kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
“Tutaangalia jinsi ya kuongeza bajeti ya ofisi hii ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake,” alisema.
Sheria ya vyama vya siasa
Akizungumzia sheria ya vyama vya siasa alisema kuwa ina adhabu moja tu ambayo ni kukifuta chama kinachofanya makosa, kusisitiza kuwa sheria hiyo haitoi nafasi ya kutosha kulea vyama, hivyo inatakiwa kutazamwa upya.
“Mchakato wa kupitia sheria hiyo na ile ya gharama za uchaguzi umeanza. Naamini marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa itasaidia kuboresha matatizo ya shughuli za kisiasa nchini,”
“Bila kuingilia uhuru wa vyama vya siasa na ile ya uchaguzi kusaidia wananchi kuchagua watu kwa ubora wao na vyama vyao.”
Kutenganisha biashara na siasa
Alisema jambo ambalo mpaka sasa halijaanza kushughulikiwa ni kutenganisha biashara na siasa, “Jambo hili limeonekana kuwa gumu kweli kushughulikiwa ndani ya mfumo wa Serikali, sijui limekwama wapi.”
Alisema lazima kuwepo na misingi ya maadili ya uongozi na kwamba mfanyabiashara anayejitosa katika siasa lazima afuate utaratibu fulani kama inavyofanyika nchi mbalimbali duniani, ikiwamo Marekani huku akimtaka msajili wa vyama vya siasa kulishughulikia suala hilo ili liweze kumalizika.
Wanasiasa wanena
Wakizungumzia hotuba ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alisema, “Rais anatakiwa kudhibiti kauli zinazotolewa na viongozi wa chama chake, ambao wanapinga masuala mbalimbali yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba ikiwamo serikali tatu.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk
Willibrod Slaa alisema, “Hakugusia kabisa wabunge wa Bunge hilo
kuzingatia maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu hiyo.”
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, “Nadhani mmesikia alichokisema Rais. Tutazingatia yote aliyoyasema kwa sababu Katiba hii ni kwa ajili ya masilahi ya Taifa.”
Wakati huo huo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Issa Salum alizua kioja wakati akijitambulisha baada ya kujipambanua kuwa ni muumini wa Muundo wa serikali mbili, kauli ambayo iliwafanya baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kumwangalia kwa mshangao
Source: mwananchi
No comments:
Post a Comment