Ndugu zangu,
Profesa Mwesiga Baregu amenukuliwa na gazeti Mwananchi akisema;
"Bila
kuweka utashi wa kujenga taifa moja, Bunge lijalo linaweza kutawaliwa
na vituko. Iwapo wajumbe watakwenda kwenye Bunge la Katiba huku wakiwa
na ushabiki wa vyama vyao mimi naona kutakuwa na vituko
vikubwa.Tunapaswa kutambua kwamba tunakwenda kutengeneza Katiba ya Taifa
na siyo kwa kuegemea masilahi ya kundi fulani" - Profesa Baregu (
Mwananchi, Februari 7, 2014)
Na kabla sijaichambua kauli ya
Profesa, ngoja hapa nimkumbushe Profesa juu ya mwanafalsafa wa Kiyunani,
Ptolemy, huyu alipata kuandika: "Ex Africa simper aliquid novi". Maana
yake: "Kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika."
Mimi nadhani Profesa amechelewa katika
kauli yake hii, maana, anachofikiri Profesa kuwa kitatokea, tayari
ishara zilishaonekana, na sasa tumeanza kukiona. Na Rais Kikwete kule
Mbeya majuzi ndiye aliyeweka bayana kabisa, kuwa tatizo naye ameliona,
kuwa kwenye Bunge la Katiba yumkini malumbano hayatakuwa ya hoja bali
hata kupimana ubavu na kwa sura za rangi za vyama.
Profesa wangu Baregu, hivyo
vitakavyotokea si vituko tu, ni vioja kama anavyosema Mwanafalsafa
Ptolemy. Na tujiandae na burudani za aibu kwa taifa.
Maana, nilishapata kuandika, kuwa
safari nyingi za Mwafrika ni za bure tu. Tusipotanguliza busara na
hekima, tutambue, kuwa kazi yote hii ya akina Jaji Warioba na wenzake
nayo itakuwa ni ya bure tu. Tutakuwa tumechoma mabilioni ya fedha kwa
jambo litakalohitimishwa na kutugawa zaidi kuliko kutujenga kama taifa.
Maana, sisi ni wabinafsi kuliko. Hatutangulizi maslahi ya nchi bali yetu
binafsi, ya makundi yetu na vyama vyetu.
Na zaidi ya miaka 15 iliyopita
niliandika, kuwa Tanzania ina vyote kasoro Watanzania. Tusipowafanya
wajumbe wengi ndani ya Bunge la Katiba wafikiri kama Watanzania, basi,
tutaishia kuipata Katiba ya Vyama Vya Siasa na si ya Watanzania.
Maana, wanachotaka Watanzania walio
wengi tayari kinafahamika kupitia rasimu ya pili ya Mabadiliko ya
Katiba. Lakini, hofu iliyopo ni kutokea kwa baadhi ya Watanzania
wenzetu, kupitia Bunge la Katiba, kuyateka matakwa ya umma na
kupandikiza matakwa ya vyama na makundi.
Maana, kupitia Tume ya Warioba
Wananchi walishausonga ugali wao na ukaiva. Lakini, kuna waliojipanga
kwa kuanika kimea cha mtama, tayari kuwakorogea Wananchi togwa ili
wanywe, walewe na kuendelea kulala usingizi. Wakiamka watayakuta yale
yale. Na yawe ni mapambano, ya uwepo wa Katiba ya Kusongwa na Wananchi,
kama ugali, na kuipinga kwa hoja, Katiba ya kukorogwa na wanasiasa, kama
togwa.
Itakumbukwa, mwanzoni kabisa mwa
mchakato wa Katiba, Profesa Kabudi alipata kusema, " What we are doing
is Constutional building and not Constutional making". Kwamba
tunachokifanya ni Ujenzi wa Katiba na si Kutengeneza Katiba.
Na katika alichokisema Profesa Kabudi
swali lilikuja,je;
" Ni kina nani wanaostahili kushirikishwa kwenye
maandalizi ya ujenzi huo? Swali lingine, ni maoni yepi yanayotakiwa
kupewa kipaumbele, ya wananchi au wanasiasa?
Nahofia, kuwa hatufikiri kuhusu nchi
yetu tuliyozaliwa na hatma yake. Tunajifikiria sisi , makundi na vyama
vyetu. Vyote vya kupita, wakati nchi itabaki.
Maana, kutengeneza Katiba ya nchi ni
sawa na kulima shamba la pamoja. Na kwanini basi wenye kulima shamba
moja wagombanie majembe? Hakika, huo utakuwa ni uwendawazimu, ni kwa
vile, watakachopanda na kuvuna ni cha faida yao wote.
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
0754 678 252
Iringa.
Maggid Mjengwa,
0754 678 252
Iringa.
No comments:
Post a Comment