Dodoma. Siku moja baada ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kusema wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba, wanaweza kubadili chochote, isipokuwa tunu za
Taifa, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba,
ameonya kuwa jambo hilo linapaswa kufanywa kwa uangalifu mkubwa.
Jaji Warioba alipingana na kauli hiyo ya Jaji
Werema na kusisitiza kuwa Katiba ni mali ya wananchi, hivyo mawazo na
mapendekezo yaliyokusanywa na tume yake kupitia Mabaraza ya Katiba
“yanapaswa kuheshimiwa”.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo alipotakiwa na
gazeti hili kufafanua kile kinachoonekana kama mkanganyiko wa kauli za
viongozi hao wakuu kuhusu majukumu ya Bunge la Mabadiliko ya Katiba.
“Katika hili mimi ndiyo msemaji wa mwisho. Kwenye
mchakato huu, sisi sote ni washauri tu, someni vizuri sheria mtajua.
Tangu mwanzo, wananchi ndio waliotoa maoni yao, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ikayakusanya na kutengeneza rasimu ya kwanza,” alisema Jaji
Warioba na kuendelea: “Baadaye tukairudisha rasimu hiyo kwa wananchi
wenyewe, baada ya kuiboresha kupitia mabaraza ya katiba ya wilaya.
Wakaibadili wenyewe, kuridhia na hatimaye tukapata Rasimu ya Pili ya
Katiba. Hivyo hata hii rasimu itakayojadiliwa bungeni, bado ni mali ya
wananchi.”
Jaji Warioba alisema tofauti na nchi nyingine
ambako Bunge la Katiba linaruhusiwa kufanya mabadiliko kwenye rasimu,
utaratibu tuliouchukua hapa nchini, ni Bunge hilo kuliondolea mamlaka
hayo.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba wenzetu Bunge
lao linakuwa na uwakilishi wa wananchi waliochaguliwa kwa ajili ya
katiba tu. Kwa maana hiyo ni wananchi wenyewe. Lakini sisi kwenye Bunge
letu tumechanganya wajumbe wa Katiba na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano na wale wa Baraza la Wawakilishi ambao kimsingi,
hawakuchaguliwa kwa kazi hiyo,” alisema. Aliongeza: “Kwa utaratibu huu
wa kwetu, wananchi wana mamlaka zaidi juu ya Katiba yao kuliko Bunge.
Bunge na sisi wengine wote tunashauri tu, ndiyo maana hata Tume
ilipotengeneza rasimu ya kwanza, ilibidi iirudishe tena kwa wananchi.
Jaji Warioba alienda mbali zaidi na kufafanua kazi ya Bunge hilo kuwa ni kuboresha Katiba.
“Ukiangalia kwa undani, huwezi kuboresha bila
kubadili, ila unaboresha kwa kiwango gani na mamlaka yako ya kuboresha
yainaishia wapi. Ndiyo maana sisi kwenye Tume tulipoboresha maoni ya
wananchi na kutengeneza Rasimu ya Kwanza ya Katiba, tukairudisha kwa
wananchi,” alisema.
Alisema kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni
kuiboresha rasimu hiyo kwa kutoa ushauri na maoni yake ambayo hata hivyo
si lazima yakubalike na wananachi ambao ndio wenye Katiba yao.
Alichosema Werema
Akijibu maswali ya wajumbe wa Bunge Maalumu juzi,
Jaji Werema alisema Bunge Maalumu linaweza kubadili vifungu mbalimbali
vilivyomo katika Rasimu ya Katiba, isipokuwa vilivyotajwa katika kifungu
cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kama kazi ya Bunge hilo ingekuwa kufanyiwa maboresho kwa
vifungu vya rasimu hiyo tu, kusingekuwa na maana ya kuwepo kwake.
“Kwanza idadi ya watu waliotoa maoni ya Katiba
Mpya ni Ndogo ikilinganishwa na idadi ya wananchi wote wa nchi hii.
Bunge hili halipitishi Katiba na ndiyo maana kuna hatua nyingine ya
wananchi kupiga kura. Kama itaonekana kuna kitu kinafaa na kinaweza
kuingizwa na kukubalika ni sawa,” alisema na kuongeza:
“Nyinyi kama mngekuwa mnafanya maboresho tu au
ukarabati sidhani kama kungekuwa na umuhimu wa kuwa na Bunge
hili.” Alisema hata mawazo mazuri ambayo yapo katika nyaraka za makundi
mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa yanaweza kujadiliwa katika Bunge
hilo.
“Kisichotakiwa ni nyaraka hizo kutoingizwa humu
bungeni. Rasimu inayojulikana na kukubalika ni hii iliyotolewa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba tu,” alisema.
Mambo yaliyomo katika kifungu hicho ambayo
hayatakiwi kubadilishwa ni uwepo wa Jamhuri ya Muungano, uwepo wa
Serikali, Bunge na Mahakama, mfumo wa kiutawala na kijamhuri na uwepo wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mengine ni umoja wa kitaifa, amani na utulivu,
uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalumu,
ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu, utu usawa mbele ya sheria na
mwenendo wa sheria na uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na
dini yoyote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.
“Fanyeni vyote lakini katika kifungu cha tisa
hamtaruhusiwa kubadili chochote labda muongeze tu baadhi ya mambo lakini
siyo kupunguza,” alisema Werema.
source:mwananchi
source:mwananchi
No comments:
Post a Comment