Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ametangaza majina 201 ya wajumbe
kutoka makundi mbalimbali nchini walioomba kuteuliwa ili waungane na
wabunge wa Bunge la Jamhuri na la Wawakilishi Zanzibar waliopo, kuingia
kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya kutangaza majina hayo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, Kaimu
Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florence Turuka, alisema kazi ya kuwapata
wajumbe wa Bunge hilo ilikuwa ngumu.
Kwa sasa Rais Kikwete amenawa mikono kama Pilato, na sasa analala
usingizi mnono, akiwatazama wajumbe aliowatupia zigo ili wajadili
mustakabali wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni wa nchi hii na ikitokea
wakaboronga ni wao wenyewe lakini yeye nadhani hahusiki tena.
Kwa msingi huo huo, hatutarajii tuone tena kuna watu wanasinzia na
kulala usingizi katika Bunge hili Maalum kama tulivyozoea kuwaona baadhi
ya wabunge wakipiga usingizi hadi wakafikia kukoroma na kutoa udenda
mdomoni.
Aidha, hatutaki kuona tena, usingizi huu na kauli ya wanaoafiki waseme
ndiyo hata kama mbunge alikuwa amelala na wala hakujua chochote
kilichokuwa kikizungumzwa.
Utaratibu wa kuafikiana ufanyike kwa kupiga kura za siri ili kila mtu
awe huru kupendekeza anachoona kinafaa badala ya kuulizwa kwa mdomo.
Pamoja na wabunge wa Bunge la Muungano na Wawakilishi kule Zanzibar,
lakini macho na masikio ya watanzania nikiwamo mimi, kwa sehemu kubwa
sana tunawaangalia na kuwategemea wajumbe 201 toka makundi mbalimbali,
walioteuliwa ili wawe mawakili.
Walioteuliwa ni kutoka taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za
kidini Tanzania Bara, kundi la vyama vya siasa, taasisi za elimu, watu
wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya
wavuvi, vyama vya wakulima na watu wenye malengo yanayofanana.
Kama kati ya watanzania zaidi ya milioni 44, wajumbe hao 201
wameteuliwa, ni matarajio yangu watathamini uteuzi huo, na hivyo katika
mjadala huo wa rasmu ya pili ya katiba, watajikiti kuangalia mustabali
na uzalendo wa taifa hili, ili waandike historia muhimu maishani mwao.
Naamini wajumbe hao watatamani kuandika historia katika maisha yao ili
wakumbukwe na vizazi vya miaka 50 ijayo ambapo vizazi hivyo vitasoma,
vitasikia, na kushuhudia katiba nzuri na kuwapongeza kuwa walifanya kazi
nzuri na kusujudu makaburi yao badala ya kuwalaumu.
Lakini kama wajumbe hao watajadili usingizi wa Itikadi zao, dini zao,
maslahi ya uongozi wa watu fulani binafsi, ukanda, ukabila bila kujali
utaifa; vizazi vijavyo vitawalaumu kwa kutengeneza katiba mbovu.
Ikiwa katiba mpya haitapatikana kutasababisha msuguano mkubwa miongoni
mwa jamii nchini Tanzania, kwa sababu iliyopo imeonesha mapungufu
makubwa ambayo kwa namna moja au nyingine, imekuwa ikiwanyima haki
wananchi na hasa wapiga kura.
Ni rai yangu wajumbe wafahamu kwamba, wanakwenda huko huku wakijua kuwa,
kama watafanya madudu yasiyotarajiwa kutupatia katiba mpya, waelewe
wananchi bado tuna nafasi ya kuipigia kura ya kuikataa ama kuikubali.
0715933308
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment