Mabingwa watetezi Yanga wametuma salama kwa Al
Ahly baada ya kuisambaratisha Ruvu Shooting kwa mabao 7-0, huku Mbeya
City wakinyukwa 2-0 na Coastal Union.
Yanga inayojiandaa na mechi ya Ligi ya Mabingwa
dhidi ya Al Ahly wiki ijayo ilipata mabao yake kupitia washambuliaji
wake Didier Kavumbagu, Simon Msuva waliofunga mabao mawili kila moja,
huku Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa na Khamisi Kiiza kila moja alifunga
bao moja.
Kwa matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 39,
wakati Mbeya City waliopokea kipigo wamebaki nafasi ya tatu na pointi
zao 35, Azam wameshuka nafasi ya pili na pointi 36 na Simba ya nne (32).
Kipigo cha Ruvu Shooting cha mabao 7-0 kimekuja
ikiwa ni siku nne tu zimepita tangu ndugu zao wa JKT Ruvu kunyukwa 6-0
na Tanzania Prisons.
Yanga ilianza mechi hiyo kwa kishindo kwa kupata
bao katika dakika ya kwanza lililofunga na Kavumbagu kwa shuti la mguu
wa kushoto akipokea pasi ya Okwi, wakati Shooting wakishangaa Msuva
aliifungia Yanga bao la pili dakika ya pili akimalizia pasi ndefu ya
Ngassa.
Shooting waliamka na kufanya shambulizi dakika ya 12, lakini mpira wa kichwa wa Michael Aidan ulidakwa na Deogratus Munishi.
Kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa aliyekuwa
Misri kuishuhudia Al Ahly aliingia uwanjani hapo dakika 15 na kwenda
moja kwa moja kwenye benchi.
Mshambuliaji Okwi aliwainua mashabiki dakika ya 28
kwa kupachika bao la tatu baada ya kumlamba chenga kipa wa Shooting,
Abdallah Ramadhani.
Ngassa aliendeleza kulizamisha jahazi la Shooting
dakika ya 34 baada ya kumzidi ujanja beki Mangasi Mbonosi na kipa wake
Ramadhani na kufunga bao la nne.
Kasi ya washambuliaji wa Yanga, Kavumbagu, Okwi, Ngassa na Msuva iliwashinda kabisa mabeki wa Shooting.
Kocha wa Shooting, Tom Olaba aliwapumzisha Juma
Nade, Hamis Ali, Shabaan Suzan na kuwaingiza Said Madega, Ayoub Kitala
na Gedion Sepo.
Wakati Hans Pluijm aliwapumzisha Mbuyu Twite, Ngassa, Kavumbagu na kuingia Juma Abdul, Kiiza na Said Bahanuzi.
Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kubwa kwa Yanga, katika dakika
ya 53, Kavumbagu alitumia vyema krosi ya Msuva kufunga bao la tano.
Kiiza alipachika bao la sita kwa kuunganisha krosi
ya Msuva bao lililomfanya kocha wa Shooting, Olaba kuondoka uwanjani
hapo na kuingia vyumbani, lakini baadaye alirejea.
Msuva alihitimisha karamu hiyo kwa kufunga bao la
saba kwa shuti kali akimalizia mpira uliorushwa na Juma Abdul katika
dakika ya 77.
Tanga, Wenyeji mabingwa wa 1988,
Coastal Union walithibitisha utu uzima dawa baada ya kuinyuka Mbeya City
mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mabao ya Coastal Union yalifungwa na Mohamed
Mtindi katika dakika ya 79 na 89 na kuzima kasi ya Mbeya City ambayo
ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini washambuliaji wake walikosa
umakini kwenye umaliziaji.
Katika mchezo mwingine Mtibwa Sugar iliichapa
Ashanti United 2-1, mabao ya Mohamed Mkopi na Abdalla Juma huku Musa
Mgosi akipewa kadi nyekundu.
Arusha JKT Oljoro ililoa 2-1 kutoka kwa Mgambo Shooting, huku Kagera Sugar wakiiadhibu Rhino Ranger 1-0 bao la Suleiman Kibuta.
Azam, Simba vitani leo
Azam FC ina shughuli pevu leo itakapokabiliana na
Prisons kwenye uwanja wake wa Azam Complex, wakati Simba itateremka
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupepetana na JKT Ruvu.
Ni wazi, Azam itaingia uwanjani ikiwa na mawazo ya
kusaka ushindi ili kujipoza na machungu ya kutupwa nje ya Michuano ya
Kombe la Shirikisho baada ya kuchapwa jumla ya mabao 2-1 na Ferroviario
ya Msumbiji.
Hata hivyo, kazi haitakuwa nyepesi kwa Azam, kwani
Prisons nayo imeingia mzunguko wa pili ikiwa na staili mpya ya kutoa
vichapo vikali bila kujali inacheza na nani. Prisons inayokamata nafasi
ya tisa ikiwa na pointi 19, haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake
tatu za mzunguko wa pili ilizokwishacheza ambapo ililazimishwa sare ya
0-0 na Coastal Union, ikaichapa Mtibwa mabao 3-1 kisha ikainyuka JKT
Ruvu mabao 6-0.
Nayo Simba baada ya ziara ngumu mikoani iliyoshuhudiwa ikikosa
ushindi hata mmoja katika mechi zake tatu, itakuwa na fikra za kusaka
ushindi ili kurejesha furaha ya mashabiki wake mbele ya JKT Ruvu.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic amewaambia wachezaji wake kwamba hataki mzaha tena anahitaji ushindi tu kuanzia mchezo wa leo.
Imeandaliwa na Sosthenes Nyoni (Dar), Burhan Yakubu (Tanga), Musa Juma (Arusha), Juma Mtanda (Moro) na Phinias Bashaya (Kagera)
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment