Rais Jakaya Kikwete amesema uteuzi wa
majina 201 ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba umekamilika na kati ya
leo na kesho, atayatangaza pamoja na tarehe ya kuanza kwa Bunge hilo.
(HM)
Bunge la Katiba litakalokuwa na
wajumbe 640, litakutana kwa siku 90 kujadili Rasimu ya Katiba
iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Desemba 30, mwaka jana.
"Bunge la Katiba litakutana katika
wiki ya tatu ya mwezi huu. Mambo yanayosubiriwa ni mawili tu, uteuzi wa
wajumbe 201 na siku ya kuanza kwa Bunge hili. Mambo haya yote
ninayesubiriwa kuyakamilisha ni mimi tu," alisema Rais Kikwete alipokuwa
akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa
CCM.
Alisema kazi ya uteuzi wa wajumbe hao
ilikamilika tangu juzi na kinachofanyika sasa ni kuhariri majina hayo na
kurekebisha mambo kadhaa.
"Jumatatu (leo) tutayapitia majina
haya ili tuone kama tunaweza kurekebisha. Baada ya hapo tutaweza
kutangaza na inaweza kuwa siku hiyohiyo au kesho yake (Jumanne),
hazitazidi siku hizi mbili," alisema.
Alisema hivi sasa ukarabati katika
Ukumbi wa Bunge, Dodoma bado unaendelea na mkandarasi ameeleza kwamba
hadi Februari 10, mwaka huu atakuwa amemaliza kazi.
"Nimewapa siku tano hadi saba za
kujaribu spika na vipaza sauti ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa,
lakini pia nitakwenda kupata ushauri wa wanasheria ili kuweza kutangaza
siku ya Bunge hili kukutana," alisema.
Amshangaa Mbowe
Katika hotuba yake Rais Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM, alimshangaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe kwa kauli yake kwamba mfumo wa Serikali tatu ukikataliwa katika
Bunge hilo, nchi haitatawalika.
"Huku ni kuwadanganya wananchi, pale
hakuna ngumi wala vurugu yoyote, kila ibara iliyopo katika rasimu
itajadiliwa ili upatikane mwafaka. Huku ni kukosa ukomavu wa kisiasa,"
alisema.
Alisema si kweli kwamba kila
mwanaChadema anataka mfumo wa Serikali tatu na kila mwanaCCM anapendelea
mfumo wa Serikali mbili akisema kinachohitajika ni ushawishi wa kujenga
hoja ili wanaopinga wakubaliane.
Chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment