Na Mwinyi Sadallah
Waziri Kiongozi mstaafu wa SMZ Shamsi
Vuai Nahodha, amesema hoja ya kuwapo au kutokuwapo kwa hati ya Muungano
kusifute azma ya kuwashughulikia viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za
matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali za umma Zanzibar .
Nahodha aliyasema hayo jana wakati
akihutubia mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye uwanja wa
Mzalendo Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani hapa.
Alisema ameshangazwa na baadhi ya
viongozi wakitunisha misuli kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar wakati baadhi yao wakikabiliwa na tuhuma za unadhirifu ikiwemo
matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema Zanzibar inakabiliwa na matatizo
makubwa ya matumizi mabaya ya ardhi kwani viongozi wengi walijimegea
kwa maslahi binafsi na wanajulikana.
Akifafanua zaidi alikiri kuwa kero za
Muungano zipo na zinaeleweka ingawa alisema baadhi ya watu wakiwamo
viongozi wanatumia mwanya huo ili kuficha tuhuma za ufisadi, uporaji na
kujipatia utajiri usioelezeka.
"Kuhoji kuwapo au kutokuwepo kwa hati ya
muungano baada ya miaka 49 kupita ni sawa na mtu kupatwa shaka kuhusu
uhalali wa cheti cha ndoa ya wazazi wake, je ikiwa kimepotea kinaweza
kubatilisha ndoa na uhalali wa mtoto,?"alihoji Nahodha
Alisema wanaotaka Muungano wa mkataba
nia na lengo lao ni kuvunja muungano uliopo ili wapate nafasi ya
kuatamia utajiri waliopata kwa kupora mali za wananchi na serikali
yakiwamo majengo ya umma kinyume na sheria.
Aidha, aliwataka viongozi wa serikali na
wanasiasa kujenga utashi na ujasiri wa kuhoji kwa nguvu ya hoja na
kukemea vitendo vya ufujaji vilivyokithiri na kusababisha uchumi wa
Zanzibar kutoimarika.
Alisema bado kuna vitendo hatarishi
katika taasisi za serikali hivyo ni jukumu la kila mwenye ujasiri
akapaza sauti yake badala ya kutumia muda mwingi kujificha kwenye kivuli
cha hati ya Muungano.
Nahodha ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa alisema Serikali ya CCM itaendelea kutetea
msimamo wake wa muundo wa Serikali mbili na kushughulikia kasoro na
utatuzi wa kero zilizopo katika Muungano bila kuyumbishwa na kundi
lolote.
Akizungumzia upotevu wa Sh. bilion 20
katika Shirika la Umeme Zanzibar(zecco), alisema fedha hizo ni nyingi na
zingeweza kutumika kusukuma maendeleo ya kisekta na badala yake akasema
zimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
"Tusijifiche chini ya kivuli cha hati ya
muungano wakati baadhi yetu mikono yetu inachuruzika michirizi ya
uporaji, wizi na ubadhirifu wa mali za umma na uvunjaji wa
sheria,"alisema Nahodha huku akishangiliwa.
Akilizungumzia suala la vijana kukosa
ajira, alisema ni hatari kulisahau kundi hilo la vijana kwa kuwa ndiyo
lenye nguvu na ushawishi.
"Chama chetu kihakikishe kinachemsha
bongo na kulishika kundi hilo, lipewe nafasi katika medani za uongozi wa
leo, kujengewa uwezo ili liwe jeshi imara litakalokabili mapambano na
kuwashinda maadui,"alisema Nahodha .
Matamshi ya Nahodha yamekuja huku
Serikali ikiwa bado haijatekeleza ripoti tatu za Baraza la Wawakilishi
za kuchunguza matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu ikiwamo uuzaji
wa ardhi kwa maslahi binafsi na majengo ya Serikali.
Ripoti ya kwanza ilihusu uuzaji wa
majengo katika hifadhi ya mji wa urithi wa dunia katika mji mkongwe aa
Zanzibar, kisiwa cha changuu kilichokodishwa kwa bei ya
kutupa,ubadhirifu katika Zecco na Baraza la Manispaa Zanzibar.
Ingawa ripoti zote zimesema kuna
viongozi na watendaji wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa
kuuza mali za serikali kwa kutozingatia sheria ya manunuzi na ugavi
lakini hadi sasa hakuna kigogo yeyeto aliyefikishwa mahakamani
Chanzo - Nipashe
No comments:
Post a Comment