Ndugu zangu,
Kwanza kabisa niwashukuru kwa dhati kabisa nyote mlionitumia salaam
za kunifariji kwa njia za simu, email, facebook, majukwaa ya
Mabadiliko, Wanabidii na JF.
Nimefarijika sana kutambua kuwa kuna wengi wenye kunifuatilia na kunijali.
Ndugu zangu,
Kama alivyowataarifu kaka yangu Nyaroonyo Kichehere, ni kuwa, jana
Jumamosi nilikuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuanzia saa tano
asubuhi ya jana mpaka saa tatu usiku. Ilihusu mahojiano ya Polisi na
mimi kuhusiana na sakata la ndugu yetu Absalom Kibanda.
Ukweli sikukamatwa mahali popote, bali niliitwa na Kamishna (
Upelelezi) Advocate Nyombi. Alhamisi nikiwa Iringa, tukakubaliana na
kiungwana na Kamishna Nyombi kuwa nifike Makao Makuu hayo ya polisi
Jumamosi saa tano. Ikawa hivyo.
Hapo nilipokelewa na Kamishna Nyombi. Baada ya mazungumzo mafupi
ndipo akawaita maofisa wengine watano wa Upepelezi kufanya mahojiano
nami.
Niliomba niwe na Mwanasheria, nikakubaliwa. Nilimpigia simu kaka
yangu Nyaroonyo, naye, kwa vile ni Wakili pia wa Kibanda akanisaidia
kuhakikisha napata wakili mwingine. Pamoja na kuwa ilikuwa ni Jumamosi,
ndugu yangu Nyaroonyo Kichehere alifanya alivyoweza.
Ndani ya dakika 40 hivi alifika chumba nr 704 ghorofa ya saba akiwa
na Wakili Jacquiline Rweyongeza na Legal Officer Dickson Mbonde.
Nilimshukuru Kaka Nyaroonyo Kichehere. Na nilimuaga kwa kumwambia; “
Nenda ukaifahamishe jamii juu ya hiki kilichonitokea”.
Nachukua fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati kabisa dada yangu Wakili
Jacquiline Rweyongeza na kaka Dickson Mbonde kwa kuacha yote ya
Jumamosi na kuwa tayari kuwa msaada kwangu. Jacquiline alimuacha
nyumbani mtoto wake wa miezi minne kwa ajili ya suala langu. Sina namna
nyingine ya kumshukuru. Na hakika, msaada wao niliuhitaji sana.
Nawashukuru pia kwa dhati kabisa, ndugu zangu Saed Kubenea, Mbaraka
Islam na wengine wote waliokuwa na utayari wa kunisaidia pale msaada
wao ulipohitajika. Kwa ufupi, nimetoa maelezo yangu bila shuruti wala
kutishwa.
Na nimeweka wazi kuwa yanaweza kutumika Mahakamani kama yatahitajika au hata kama mimi nitahitajika, kwa namna yeyote ile.
Kesho saa mbili asubuhi nitaripoti Makao Makuu ya Polisi kupewa
maelezo ya kitakachofuatia.Kwa mara nyingine tena, nawashukuru sana kwa
kuwa nami katika muda wote huu.
Maggid,
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment