Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Aprili 29,
2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid
Mwenyekiti wa kamati ya
uwasilishaji wa mapendekezo ya muundo wa mabaraza ya Katiba kwa jamii ya
watu wenye ulemavu, Bw. David Nyendo (kushoto) akiwasilisha maoni yake
ya kamati hiyo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika mkutano baina yao
uliofanyika ofisi za Tume Jijini Dar es Salaam.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema
imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa
na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya
katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013).
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh
Warioba amesema leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam
kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka
taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.
"Tume haitengenezi katiba ya vikundi
au vyama, tunaandaa katiba ya nchi," amesema Jaji Warioba katika mkutano
wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume
inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi na sio idadi ya watu
waliotoa maoni.
Jaji Warioba amewataka wananchi
kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa
kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.
Mabaraza ya Wananchi wenye ulemavu
Akizungumza kuhusu ushiriki wa
walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake
inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa
fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu
rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.
Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho
la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu
wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.
Jaji Warioba amesema Baraza moja
litaundwa Tanzania Bara na jingine Zanzibar na kwamba yatashirikisha
wananchi kutoka ngazi ya chini ya wilaya hadi Taifa.
"Tunaelewa kuwa watu wenye ulemavu ni
karibu asilimia 10 ya watanzania wote na mchakato huu hauwezi kuwatenga
katika ngazi yoyote," amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa taarifa
ambazo Tume yake inazo zinaonyesha baadhi ya watu wenye ulemavu
wamependekezwa na mitaa, vijiji, vitongoji na shehia kuwa Wajumbe wa
Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Chaguzi za Wajumbe Mabaraza ya Katiba ya Wilaya.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia
mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika
nchini kote hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba
kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini
ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika
ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa
na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na
utulivu.
"Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na
asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha
vizuri mchakato huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia
99.8 kati ya Kata 3,339 kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato
wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia
utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo," amesema Jaji Warioba.
Kuhusu hatua inayofuata baada ya
chaguzi hizo, Jaji Warioba alisema Tume inaendela kupokea majina kutoka
kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ya wananchi wote waliopendekezwa
kutoka katika Kata na Shehia na kazi hiyo inatarajia kukamilika ifikapo
tarehe 30 Aprili mwaka huu (2013).
Changamoto
Akizungumzia kuhusu changamoto
zilizojitokeza katika chaguzi hizo, Jaji Warioba amesema kuwa pamoja na
mafanikio yaliyopatikana pia kulijitokeza changamoto kadhaa ambazo
zilisabishwa na misimamo ya kisiasa na kidini
"Katika baadhi ya maeneo mikutano ya
uchaguzi ngazi za vijiji, mitaa na shehia ilishindwa kufanyika kutokana
na mivutano ya kisiasa na kidini zilizosababishwa na baadhi ya wananchi
kufangamanisha chaguzi za Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na
masuala ya kisiasa na kidini," amesema Jaji Warioba.
Jaji Warioba ametaja changamoto
nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kujiingiza katika vitendo
vya rushwa katika chaguzi hizo ili wapendekezwe kuwa wajumbe wa mabaraza
hayo ya katiba.
"Tumepokea pia malalamiko ya vitendo
vya rushwa," alisema Mwenyekiti huyo na kusema vitendo hivyo ni kinyume
cha sheria na kuongeza kuwa taasisi zenye mamlaka ya kupambana na
vitendo hivyo zinapaswa kushughulikia malalamiko hayo.
Aina na Majukumu ya Mabaraza ya Katiba
Katika mkutano huo uliofanyika katika
katika Ofisi za Tume zilizopo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti huyo pia alizungumza kuhusu aina na majukumu ya Mabaraza ya
Katiba.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imetoa fursa ya kuundwa kwa mabaraza ya
aina mbili ambayo ni Mabaraza yatakayoundwa, kusimamiwa na kuendeshwa
na Tume katika muda na tarehe itakayopangwa na Tume.
Aina ya pili, kwa mujibu wa Mwenyekiti
huyo, ni Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi mbalimbali
yenye malengo yanayofanana. Mabaraza haya yatajiunda, yatajisimamia na
kujiendesha yenyewe na kisha kuwasilisha maoni yao kuhusu rasimu ya
Katiba ndani ya muda utakaopangwa na Tume.
"Kazi kubwa ya Mabaraza ya Katiba ya
aina zote mbili ni kuipitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya
Katiba itakayokuwa imeandaliwa na Tume kutokana na maoni yaliyokusanywa
kutoka kwa wananchi," alisema Jaji Warioba na kuziomba taasisi, makundi,
asasi na vyama mbalimbali kutumia fursa hiyo ya kisheria kuunda
mabaraza na kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa.
source:Mjengwa blog
No comments:
Post a Comment