WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, April 22, 2013

Yanga pointi 1 bingwa

 
Simon Msuva wa Yanga (Mbele), akimiliki mpira mbele ya mlinzi wa Ruvu JKT, Damas Makwaya kwenye pambano la soka ligi kuu ya Tanzania bara kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam jana.
Yanga ilitoa kipigo kikali cha magoli 3-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana na kubakisha pointi moja ili kutwaa ubingwa wa 23 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ushindi uliwafanya vinara hao wa ligi kufikisha pointi 56, idadi ya juu kabisa ambayo wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Azam FC (wenye pointi 47) wanaweza kufikisha iwapo watashinda mechi zao zote tatu zilizobaki.

Yanga wanaweza kutwaa ubingwa "bila ya jasho" Jumamosi kama Azam watashindwa kupata ushindi dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 

Magoli kutoka kwa Simon Msuva, Hamis Kiiza na Nizar Khalfan yaliwaweka Yanga jirani zaidi na ubingwa wao wa 23 ambao ni rekodi wakifuatiwa na Simba iliyoutwaa mara 16.

Msuva, ambaye goli lake la dakika za lalasalama liliiokoa Yanga na kipigo katika sare ya 1-1 dhidi ya Mgambo JKT katika mechi yao iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani, aliifungia timu yake goli la kuongoza katika dakika ya 45, bao ambalo hata hivyo lilikuwa la utata.

Utata ulianzia pale Kiiza alipoutoa mpira lakini kijana muokota mipira akamkabidhi mpira beki wa Yanga, Mbuyu Twite badala ya kuwapa JKT warushe katika tukio hilo lililotokea pembeni kidogo mwa kibendera cha kona. Mbuyu akaurusha haraka kwa Msuva aliyekuwa ndani ya boksi na mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Tanzania akapiga shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha hasira za wachezaji wa JKT. Hata hivyo maamuzi ya goli hilo hayakutenguliwa.

Kiiza aliifungia Yanga goli la pili katika dakika ya 57 baada ya mabeki wa JKT kujichanganya na Nizar akapigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la 'maafande' akimalizia wavuni mpira ulirudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti ya Frank Domayo aliyetumia pasi ya Haruna Niyonzima.

Kocha msaidizi Fred Minziro ndiye aliyeliongoza benchi laYanga jana kutokana na kutokuwapo kwa kocha mkuu Mholanzi Ernie Brandts kwa kile kilichoelezwa na Katibu Mkuu, Lawrance Mwalusako, kwamba alikuwa akiugua Malaria.

Minziro alisema baada ya mechi hiyo kwamba hali nzuri ya uwanja na sapoti kubwa ya mashabiki ndiyo iliyokuwa sababu ya ushindi wao jana.

Kocha wa JKT Ruvu, Azish Kondo alisema kuwa timu yake inakabiliwa na tatizo la utawala.
Alisema baadhi ya viongozi wao wamehamishwa na wengine kubadilishwa vitengo na kwamba goli la kwanza lililotokana na makosa ya marefa, hasa refa msaidizi namba 2, Lulu Mushi wa Dar es Salaam aliyeruhusu mpira urushwe kuelekea JKT na kwamba goli hilo liliwatoa vijana wake mchezoni.

Yanga walianza mechi vizuri zaidi kwa kuliandama lango la JKT Ruvu. Shabani Dihile alidaka shuti la Msuva katika dakika ya 3 na kuikosesha Yanga goli la mapema lakini dakika tano baadaye JKT walijibu mapigo kupitia kwa Ally Mkangwa ambaye hata hivyo alipiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa Ally Mustapha 'Barthez'.

Nizar Khalifan alishindwa kulenga lango baada ya shuti lake kupaa juu katika dakika ya 9 na Dk 3 kazi nzuri ya kugongeana baina yake na Haruna Niyonzima kuanzia katikati ya uwanja.
Katika dakika ya 17 beki wa JKT, Ramadhan Madenge aliruka na kutoa kwa kichwa krosi iliyopigwa na Frank Domayo na kuwanyima Yanga nafasi ya kufunga.

Kiiza angeweza kuifungia Yanga goli katika dakika ya 51 lakini alipaisha shuti lake juu ya lango na kupoteza pasi nzuri ya mbali kutoka kwa Mbuyu Twite.

Kabla ya kuanza kwa mechi wachezaji na waamuzi walikusanyika pamoja katikati ya uwanja na mashabiki walisimama majukwaani kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka gwiji wa muziki wa taarab nchini, Fatma binti Baraka maarufu Bi. Kidude, aliyefariki dunia wiki iliyopita akikadiriwa kuwa na umri wa miaka 102.

Vikosi katika mechi hiyo vilikuwa; JKT Ruvu: Shabani Dihile, Hassan Kikutwa, Stanley Nkomola, Madenge Ramadhan, Damas Makwaya, Nashon Naftary, Amos Mgisa/ Abdallah Bunu (dk.51), Ally Mkwanga, Mussa Mgosi, Zahoro Pazi na Haruna Adolf.

Yanga: Ally Mustapha 'Barthez'/ Said Mohammed (dk.51), Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athumani Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Hamis Kiiza, Nizar Khalfani na Haruna Niyozima.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment