Na Nuzulack Dausen, Mwananchi
Dar es Salaam. Mwanadiplomasia mkongwe
nchini, Dk Salim Ahmed Salim amesema amesikitishwa na vitendo vya vurugu
za dini zinazoendelea na kuzitaka mamlaka husika kudhibiti hali hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, baada ya kumalizika Kumbukumbu za mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda miaka 19 iliyopita, Dk Salim alisema hali hiyo inatakiwa kudhibitiwa mapema kabla amani haijatoweka.
Dk Salim ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU), alisema kila Mtanzania ana wajibu kuhakikisha anadhibiti uchochezi na vurugu za kidini, ili kulinda amani ya nchi ambayo imedumu kwa muda mrefu.
“Vurugu za dini ni jambo la kusikitisha na hatari sana, nchi hii ni ya Watanzania wote bila kujali itikadi za imani, hivyo tunatakiwa kulitatua tatizo hili mara moja,” alisisitiza Dk Salim.
Alisema Serikali, viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za dini, taasisi za kiraia na wananchi hawana budi kukaa pamoja kuhakikisha wanalitatua tatizo la migogoro ya dini linalotaka kuvuruga amani ya nchi.
Alisema kuna haja ya kuendeleza jitihada za
kulitatua tatizo hilo mara nyingi zaidi ya hatua iliyofikiwa, ili
kulinda mustakabali wa nchi.
Wakati huohuo, Dk Salim alizitaka nchi za bara la Afrika kuwa chachu ya kutatua matatizo ya ndani ya bara lao, badala ya kutegemea watu kutoka nje.
Dk Salim alisema nchi za Afrika zinatakiwa
kuwajibika ipasavyo kwa matendo yao, kwa kutafuta suluhu haraka
iwezekanavyo siyo kutegemea taasisi kutoka nje ya bara.
“Lazima watafute suluhu za matatizo ambabyo yanawakabili, wahakikishe wanayadhibiti haraka ipasavyo kabla hayajafikia mahali pabaya” alisisitiza.
Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda nchini, Dk
Benjamin Rugangazi alisema maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya
halaiki ni salamu kwa ulimwengu mzima katika harakati za kudumisha amani
na upendo, ili kuzuia mauaji kama hayo yasitokee tena.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment