Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema hatoongoza serikali yake kwa shikinikizo la mtu au kiongozi yeyote.
Aidha, amewashangaa wanaohoji sababu za yeye kutowateua wakuu wa wilaya na mikoa wapya tangu achaguliwe kuwa Rais mwaka 2010.
Rais Shein aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara
uliofanyika Amani Mkoa wa Mji Unguja.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, yeye ndiye Rais baada ya
kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na ndiye aliyewateua Makamu wa
Kwanza na wa Pili wa Rais kuwa wasaidizi na washauri wake.
Aidha, alisema kutokana na nguvu za kikatiba na kisheria alizonazo,
anaweza kumuondoa yeyote katika uteuzi wake bila ya kuvunja na kikuika
sheria ikiwa hataridhishwa na utendaji wa kiongozi aliyemteua.
Kauli ya Dk. Shein, ilionekana ni kama kumpiga `kijembe' Makamu
wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye aliwahi kutamka
katika mkutano wa hadhara Fuoni katika uwanja wa Magirisi kuwa hawezi
kufukuzwa kazi na Rais.
“Mimi ndiye mshindi wa urais wa Zanzibar mwaka 2010, nimeunda
serikali na kuteua Makamu wa Kwanza na wa Pili ili kunisaidia kazi na
kunipa ushauri, nimetengeneza wizara na kuteua mawaziri na naibu
mawaziri bila ya kupangiwa na mtu na wakati wowote naweza kumuondoa
yeyote,” alisisitiza.
Tangu kuchaguliwa kwake, Dk. Shein ameendelea kubakia na wakuu wa
mikoa na wilaya wale wale aliowateua Rais wa awamu ya sita, Amani Abeid
Karume na kufanya mabadiliko madogo katika Wilaya ya Kati na Kaskazini
`B’ kati ya wilaya 10 za Unguja na Pemba.
Kutowateua wakuu wa wilaya na mikoa, kumewahi kuhojiwa mara kadhaa
na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa nyakati
tofauti wakiwa kwenye vikao vya Baraza. Rais Dk. Shein alisema ana
uzoefu na maarifa ya kutosha katika masuala ya uongozi na anapenda
kuheshimu Katiba na kufuata sheria na hapendi kukurupuka au kusema
kutokana na watu wanavyosema mitaani na kwenye majukwaa ya kisiasa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment