Viongozi
wa Taifa wakishangilia jambo siku ya kuazimisha kwa miaka 49 ya Muungano wa
Tanzania, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es
salaam
Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar ni muungano wa mfano duniani. Ni dola mbili huru zilizoungana na
kuunda nchi moja yenye serikali mbili.
Tanganyika
ilipata uhuru wake Desemba 9/1961 na ikapata kiti chake katika Umoja wa Mataifa
Desemba 14, 1961. Namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1667 (XVI).’ Zanzibar
nayo ikapata uhuru wake Desemba 10, 1963 na ikapata kiti chake katika Umoja wa
Mataifa Desemba 16, 1963; namba ya kiti hicho ni ‘GA resolution 1975 (XIII).’
Ilipofika
Aprili 26, 1964, mataifa hayo mawili huru yaliungana na hapo ndipo ilipozaliwa
nchi iliyojulikana kwa jina la Tanzania.
Novemba
2, 1964 kupitia Wizara wa Mambo ya Nchi za Nje ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, iliuandikia barua Umoja wa Mataifa na kutaka Zanzibar na
Tanganyika ziondoshwe katika orodha ya mataifa na iingizwe nchi inayojulikana
kwa jina la Tanzania.
Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar ni sawa na muungano wa Siria na Misri walioungana
mwaka 1958 na ni sawa na muungano wa Yemen ya Kaskazini na Yemen ya Kusini
walioungana mwaka 1990. Kwa bahati mbaya muungano wa Siria na Misri ulivunjwa
mwaka 1961 (ulidumu kwa miaka 3).
Kwa
sasa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umefikia hatua nzuri na ya kupigiwa
mfano duniani kwa sababu umedumu kwa miaka 49 sasa.
Hata
hivyo pamoja na kuwa muungano huu una muundo wa kipekee na kuwa umedumu kuliko
miungano mingi iliyowahi kuwapo Afrika.
Muungano
wa kwanza ulikuwa ni ule wa nchi za Afrika Magharibi, mwishoni mwa miaka ya 50
na mwanzoni mwa miaka ya 60, ulioanza na nchi mbili Ghana na Guinea na baadaye
Mali ikajiunga nao. Muungano huu ulitokana na vuguvugu la umajimui wa Afrika
(Pan Africanism), vinara wake wakiwa Kwame Nkrumah wa Ghana, Sekou Toure wa
Guinea na Modibo Keita wa Mali.
Novemba
1958 uliundwa muungano wa Ghana na Guinea mara baada ya mkutano wa watu wa
Afrika (All- African Peoples’ Conference). Ghana ilitoa fedha nyingi na kuipa
Guinea ili ijitoe haraka kutoka katika utegemezi wa Ufaransa.
Mei
1959 ikatangazwa kuwa umoja huo utatambulika kama Umoja wa Dola za Kiafrika.
Ilipofika
Aprili 1961, Mali nayo ilijiunga na umoja huo. Muungano huo ulivunjika mwaka
1962 kutokana na vita baridi, ambapo Guinea ilionekana ikiinyooshea mikono
Marekani wakati wenzake walikuwa wakifuata mrengo wa kushoto wa Karl Marx/Lenin
Muungano mwingine wa nchi za Afrika ulifanyika mwaka 1981 baina ya nchi za Senegal na Gambia, uliojulikana kama Senegambia ambao ulikufa mwaka 1989.
Muungano mwingine wa nchi za Afrika ulifanyika mwaka 1981 baina ya nchi za Senegal na Gambia, uliojulikana kama Senegambia ambao ulikufa mwaka 1989.
Pamoja
na kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa kupigiwa mfano,
lakini bado si vyema kuacha kusema kuwa una matatizo.
Tatizo
kubwa la muungano huu ni ile hali ya upande mmoja kujiona kama unabinywa na
upande mwingine wa muungano, nadharia iliyozoeleka ni ‘samaki mkubwa kummeza
mdogo.’ Tatizo hilo lilisababisha baadhi ya Wazanzibar kulalamika na kumi
katika hao walijitokeza na kwenda mahakamani kudai Hati ya Muungano. Jibu
walilopata ni kuwa hakuna Hati ya Muungano (Mkataba).
Mwanasheriaa
Mkuu wa Zanzibar alisema hakuna Mkataba wa Muungano kwa kuwa suala la muungano
ni kama ardhi kwa sababu muungano ni wa nchi na nchi ni sawa na kuunganisha
sehemu mbili za ardhi suala ambalo kisheria linaweza kuhojiwa ndani ya miaka
kumi na mbili (12), baada ya hapo huwezi kuhoji, kwa maana hiyo ni halali kwa
mujibu wa sheria ukizingatia waliohoji walifanya hivyo mwaka 2004 sawa na miaka
40 tokea nchi ziungane.
Muungano
huu wa Tanganyika na Zanzibar umekumbwa na misukosuko mingi ambayo ndiyo hii
inayoitwa kero za Muungano ambazo zinatolewa na wananchi wa pande zote mbili.
Kutokana na kelele nyingi kuhusu muungano, iliundwa kamati ya kujadili na
kujaribu kutatua kero za muungano ikiongozwa na Makamu wa Rais ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kamati
hiyo iliyo na uwiano sawa wa wajumbe kutoka pande zote mbili za Muungano
imepokea kero 11 za muungano na kwa sasa wameshazitatua tisa zimebaki tatu
ambazo ziko njiani kutatuliwa kwa hivyo kwa upande wa kero wamefikia hatua
nzuri sana.
Miungano
mingi duniani inakuwa na kero lakini hutatuliwa kwa ushirikiano kwa pande zote
zinazohusika. Kwa mantiki hiyo kero ni vitu vya kawaida katika muungano wowote
ule uwe wa nchi, mataifa au hata katika jamii. Watanzania tuna kila sababu ya
kujivunia muungano huu.
Nchi
nyingi duniani zilizoungana zimeweza kupata maendeleo ya kasi ya kiuchumi na
kiulinzi, tunaweza kuuangalia Umoja wa Nchi za Ulaya kama mfano. Vilevile Umoja
wa Falme za Kiarabu ambao msingi wake ni uamuzi wa ulinzi wa uchumi wa falme
saba ya kiarabu yanayozalisha mafuta yakiongozwa na Abudhabi.
Hivyo
muungano kimsingi pamoja na mambo ya kisiasa na kijamii unakuwa na dhamira ya
kuendeleza maendeleo ya nchi husika na kutumia rasilimali zao sambamba na
rasilimali watu kuweza kujikomboa kiuchumi na kupandisha uchumi wao.
Na
kwa Tanzania kupitia Muungano hilo kwa kiasi fulani limewezekana kwa sababu
pamoja na kelele zinazopigwa kuhusu rasilimali lakini kimsingi rasilimali zote
zinazopatikana Tanzania ni za Watanzania wote kwa sababu zinaelekezwa katika
kujenga miundombinu ya maendeleo ya nchi yetu.
Na
hata kwa upande wa ulinzi, si rahisi kuichezea Tanzania kwa sababu ina nguvu ya
pamoja ambapo pengine Zanzibar peke yake na udogo wake isingeweza kuilinda
vyema mipaka yake hasa kwa sababu ni nchi iliyozungukwa na bahari na ni visiwa
vya kinacholengwa kwa stratejia za kiuchumi na hata kiutamaduni.
Waasisi
wa Muungano huu, kwa kuamini watakuwa na taifa moja madhubuti lisiloyumba wala
kuyumbishwa ndipo kwa moyo mmoja walipokubali kuunganisha nchi mbili na kuwa na
taifa moja lenye dhamira moja na kwa pamoja kujifaharisha kuwa sisi ni
Watanzania, na Tanzania ndiyo nchi inayotambulika Umoja wa Mataifa, si
Tanganyika wala si Zanzibar.
Na
bado kama kuna nchi ambazo zinataka kuungana basi zije kusoma Tanzania na
watajua nini maana ya muungano wa dhati, nini umuhimu wa kuvumiliana,
kuaminiana na kusaidiana. Hapa hasa ndipo penye udugu wa kweli hata kama
wanagombana lakini hatimaye husuluhishana na kupatana na maisha kuendelea.
Waswahili wanasema ‘ndugu wawili wakigombana, chukua jembe ukalime….’
Rashid
Yussuf Mchenga ni mwanasiasa mkongwe/mwanaharakati aliyeko Zanzibar.
+255 773 560243 / 775-560243
SOURCE: MWANANCHI; Na Rashid Yussuf
Mchenga
No comments:
Post a Comment