Spika wa Bunge Anna Makinda akiteta jambo na Naibu wake Job Ndugai
Baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda
kutoa mwongozo na kuunga mkono uamuzi wa Naibu wake, Job Ndugai
kuwasimamisha wabunge sita wa Chadema, wasomi, wanasiasa na wanaharakati
wamesema Kiti cha Spika ndiyo chanzo cha mvutano bungeni kwa kuwa
kinapendelea wabunge wa chama tawala (CCM).
Wamesema licha ya Bunge kuongozwa na
kanuni, wakati mwingine viongozi hao wa Bunge wanatumia kanuni hizo
kuwapendelea wabunge wa CCM, huku wakieleza kuwa licha ya wabunge wa
chama hicho kutukana, hawakupewa adhabu yoyote.
Jumatano ya wiki hii, Ndugai
aliwasimamisha Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joseph Mbilinyi (Mbeya
Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela),
Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema wa Arusha Mjini kutohudhuria
Bunge kwa siku tano kutokana na alichokiita kufanya vurugu ndani ya
Bunge.
Uamuzi huo wa Spika Makinda ulikuja
baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
kumtaka Ndugai aeleze alitumia kanuni gani kuwasimamisha wabunge hao.
Licha ya wabunge hao kupewa adhabu
hiyo baada ya kuomba mwongozo wa Spika na baada ya kupinga mwenzao
kutolewa ndani ya ukumbi wa Bunge, wapo wabunge wa CCM waliotukana na
kutoa lugha za kukera lakini hawakuchukuliwa hatua yoyote.
Wabunge hao ni Peter Serukamba ambaye
alitukana tusi zito la nguoni kwa lugha ya kimombo wakati ulipozuka
mzozo wakati wa hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Profesa Kulikoyela Kahigi.
Wengine ni mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na Livingstone Lusinde (Mtera).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
Mwananchi Jumapili jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es
Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Bunge la sasa linakabiliwa
na mambo mawili makubwa; la kwanza ni udhaifu wa kiti cha Spika na pili
ni wabunge wa CCM kuamini kuwa Chadema ni maadui wakati katika hali ya
kawaida siasa ni ushindani na ndiyo demokrasia kwa kuwa sasa tuko katika
mfumo wa vyama vingi.”
Alisema kuwa Spika na Naibu wake wameshindwa kudhibiti vurugu bungeni kwa sababu ya kuendekeza itikadi za vyama.
“Kushindwa huko ndiyo kunachangia
vurugu kwa sababu wote wanaegemea upande mmoja, wabunge wengine wa
upinzani hawawezi kukubaliana na hali hiyo na huo ndiyo mwanzo wa
malumbano,” alisema Profesa Mpangala.
Alisema tatizo jingine ni kitendo cha
wabunge wa CCM na chama chao kudhani kuwa upinzani ni uadui, “Hayo ndiyo
matunda ya mfumo wa vyama vingi. Mfumo huu ni wa ushindani na kuna
mambo ya msingi yanayotolewa na wapinzani na mengine hayana ubaya
wowote.”
Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho,
Bashiru Ally alisema Spika anaongoza Bunge kwa ushabiki wa vyama;
“Hatuwezi kutenganisha tabia za wabunge ndani na nje ya Bunge, ila
pamoja na hilo bungeni sasa kuna ushabiki wa vyama.”
Alisema hali hiyo inasikitisha kwani
licha ya kuongezewa posho wabunge sasa wamegeukia malumbano badala ya
kujadili mambo ya msingi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi nchini (Tucta), Nicholas Mgaya alisema kuwa viongozi hao wa
Bunge wanafanya uamuzi bila kufuata kanuni za Bunge.
“Hatuwezi kuwalaumu wabunge kwa sababu
wanaowaongoza wameshindwa kusimamia kanuni hivyo wanajua wazi kuwa hata
wakifanya ndivyo sivyo hakuna hatua zozote watakazochukuliwa,” alisema
Mgaya.
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha
Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Bunge limekosa
usimamizi mzuri, huku akifafanua kuwa limeshindwa kuwachukulia hatua
wabunge wa CCM ambao wanatumia chombo hicho cha kutunga sheria kujizolea
umaarufu.
“Wabunge watatu wa CCM walitukana,
lakini hawakuchukuliwa hatua yoyote ila wabunge wa upinzani walioomba
miongozo wamechukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kuhudhuria
vikao vya Bunge, hii si sawa” alisema.
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen-Kijo Bisimba alisema; “Inaonekana
wabunge hawajui cha kufanya wala kilichowapeleka bungeni.”
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alisema kuwa moja ya mambo yaliyotakiwa
kujadiliwa na wabunge hao ni pamoja na madai ya walimu ya muda mrefu.
“Walimu wanaidai Serikali Sh25
bilioni, kuna suala la kutokuwapo kwa mitalaa, haya yote hawayaoni
wanaishia kutupiana vijembe tu,” alisema Oluoch.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe,
Profesa Prosper Ngowi alisema wabunge wanatakiwa kutambua kuwa wapo
bungeni kwa fedha za wananchi, hivyo wanatakiwa kulipa fadhila.
“Wananchi wanawategemea wabunge
wasimamie haki na usawa na kujenga hoja za kutetea masilahi yao, naona
2015 ndiyo uwe muda wa wananchi kuchagua anayewafaa,” alisema Profesa
Ngowi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amekitaka kiti cha Spika wa Bunge
kufuata sheria, haki, kanuni na miongozo ya kibunge na si kuegemea
upande mmoja kwa mustakabali wa kulinda heshima ya taasisi hiyo nyeti
kwa taifa.
Pia amemtaka Spika wa Bunge, Anne
Makinda kuwakutanisha viongozi wote wa Bunge kutoka pande zote ili
kutafuta mwarobaini wa kile kinachoendelea hivi sasa bungeni.
Profesa Lipumba akizungumza jijini Dar
es Salaam jana, alisema kinachoendelea bungeni kinatakiwa kutafutiwa
ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
“Kinachotokea bungeni ni matokeo ya
kiti cha Spika kutokutenda haki na wakati mwingine kimekuwa kikiegemea
upande mmoja jambo ambalo linafanya kipoteze mwelekeo,” alisema Profesa
Lipumba
Alisema kiti hicho kinatakiwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Bunge na kutokufuatwa kwa vitu
hivi, matokeo yake ndiyo haya tunayoyashuhudia sasa, lugha chafu
zinazodhalilisha utu wa binadamu.
Mwenyekiti huyo alisema wabunge
wanatakiwa kuwawakilisha wananchi wao ipasavyo na kuepuka kujiingiza
katika mambo yasiyokuwa na tija kwa wapiga kura wao.
Makinda juzi alilazimika kutoa
mwongozo baada ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman
Mbowe kumtaka aeleze, Ndugai alitumia kanuni gani kuwasimamisha wabunge
hao.
Baada ya kipindi cha maswali na
majibu, Alhamisi iliyopita, Mbowe alisimama na kuomba mwongozo wa Spika
akitumia Kanuni ya 68(7).
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment