MKANGANYIKO wa gredi za ufaulu, pamoja na
mambo mengine, ulichangia kuleta matokeo mabaya ya wahitimu wa kidato cha nne
mwaka 2012, imebainika.
Aidha, utafiti wa Raia Mwema uliofanyika
katika mikoa 13 nchini, umebaini pia kwamba mabadiliko ya ufundishaji na
utungaji mitihani kutoka kwenye msisitizo wa nadharia kwenda kwenye msisitizo
wa ujuzi, na usahihishaji, nayo ni kati ya sababu nyingi za matokeo hayo
mabaya ya wahitimu wa mwaka jana na mengine ya miaka kadhaa ya nyuma.
Timu ya uchunguzi wa kiuandishi wa habari
ya Raia Mwema mwanzoni mwa mwezi huu ilizuru Mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera,
Kigoma, Mbeya, Manyara, Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Rukwa, Singida,
Pemba na Shinyanga ikitembelea shule za sekondari 48, zikiwamo zilizoshika
nafasi za chini kabisa katika matokeo hayo na ikihojiana na baadhi ya walimu
wakuu, walimu, wanafunzi, wadau mbalimbali wa elimu na jamii inayoishi jirani
na shule hizo.
Taarifa zinaonyesha kwamba kwa maeneo
makuu: Gredi, ufundishaji na utungaji mitihani kulenga wanafunzi kutumia zaidi
ujuzi; si walimu wala wanafunzi waliopewa taarifa rasmi ya kutosha ili
wajiandae kwa mabadiliko hayo makubwa katika maeneo ya kutahini na ufundishaji.
Utafiti huo pia umeonyesha ya kuwa shule
nyingi zilizofanya vibaya sana katika matokeo hayo ya mwaka jana ni za Kata,
ambazo wahitimu wake, kama walivyokuwa wa shule nyingine zilizofanya
vizuri kiasi mwaka 2012, ni wale ambao wakiwa kidato cha pili walifanya mtihani
wa mchujo, wakashindwa, lakini wakaruhusiwa kuendelea na shule kwa uamuzi wa
Serikali.
Lakini ukiacha sababu hizo za gredi,
ufundishaji na utungaji mitihani, nyingi za shule hizo zina upungufu mkubwa wa
walimu, ama walimu waliopo hawana hamasa kwa kukosa maslahi; wengi wao wako
katika mgomo baridi tangu katikati ya mwaka jana pale Serikali ilipotungua
katika Mahakama Kuu madai yao yaliyoendana na mgomo mkubwa wa nchi nzima; ni
shule ambazo hazina nyumba za walimu zinazoweza kuitwa kuwa ni nyumba; hazina
maktaba; hazina maabara; hazijawahi kufikiwa na wakaguzi; ziko kwenye mazingira
mabaya; na jamii inayozizunguka haina mwamko wa kutosha wa elimu.
Si tu kwamba shule hizo hazina miundombinu
hiyo ya ufundishaji na mazingira mazuri, bali pia hazina wafanyakazi ambao si
wa taaluma ya ualimu, kama wa maabara, uhasibu, afya na walinzi, jambo ambalo
hufanya wakuu wa shule kufanya kazi za ziada katika mazingira ya upungufu
mkubwa wa walimu huku na wao wakihitajika kufundisha.
Ni katika mazingira hayo taarifa ya
mabadiliko katika utaratibu wa muda mrefu wa gredi za ushindi inakuwa habari
kubwa. Alama zinazofahamika kwa muda mrefu ni A- alama 81 hadi 100; B- alama 61
hadi 80; C-alama 41 hadi 60; D- alama 21 hadi 40 na F- alama 0 hadi 20.
Kwamba alama hizo zimekuwa zikibadilishwa
na Baraza la Mitihani (NECTA) katika kile kinachojulikana kuwa ni
standardisation ni taarifa iliyowatisha wengi. Ni hali iliyowaathiri kwa aina
ya pekee watahiniwa wa mwaka 2012, hata kama kwa miaka karibu mitano ya nyuma
matokeo ya kidato cha nne, na hata ya kidato cha sita, yamekuwa yakionyesha kuserereka
kuelekea chini.
Vyanzo kadhaa vya habari vinasema alama
hizo sasa ziko katika makundi ya A-alama 85 hadi 100; B-alama 65 hadi 84;
C-alama 50 hadi 64; D-alama 35 hadi 49 na F alama 0 hadi 34.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Azania, Dar es
Saalam, Bernard Ngozye, anasema matokeo hayo mabaya yaliwashangaza wadau wa
elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam kiasi cha wao kukutana na kuhoji Baraza la
Mitihani kujua chanzo ni nini.
Anasema Machi mwaka huu walikutana na
maofisa wa Baraza la Mitihani na ndipo hapo walipoambiwa kwamba Baraza
lilirekebisha gredi, taarifa hiyo wakiisikia kwa mara ya kwanza.
“Matokeo hayo yalitufadhaisha sana. Ni
kweli hapa hatuna walimu wa kutosha. Watahiniwa hawakusoma vizuri masomo ya
sayansi kwa kuwa sisi sote hapa ni walimu wa masomo ya sanaa. Lakini tulikuwa
tunataraji walau wachache watapita katika madaraja ya nne au tatu.
“Walikuja hapa wenzenu. Niliwaambia haya
haya. Mmoja baadaye akaniuliza kama nilikuwa ninajua kwamba gredi za Baraza
ziko juu, nikasema hapana,” anasema Fredy John, Mkuu wa Shule ya Sekondari
Chitekete, Newala, Mtwara, ambayo ni kati ya shule 10 zilizofanya vibaya zaidi
kitaifa.
“Nami matokeo haya yamenishangaza
sana. Shule yangu haina matatizo ya walimu, maabara wala maktaba, lakini
imefanya vibaya tofauti na matarajio yetu,” anasema Sid Moir, Mkuu wa Shule ya
Sekondari ya Katoke Lweru, Muleba, Kagera.
Anaongeza Moir: “Kilichonisikitisha ni
kuona wanafunzi ambao tangu kidato cha kwanza hadi cha nne walionyesha uwezo
mkubwa kimasomo wanatoka na ufaulu wa daraja la nne. Ndoto zao zote za kusomea
udaktari zimeyeyuka.”
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa
Mwanza, Hamisi Maulidi anasema hakuna mabadiliko yoyote katika alama za
madaraja ya ufaulu wa wanafunzi na kwamba kama kuna taarifa hizo, ni za
kupuuza.
"Hicho kitu umekitoa wapi? Hizo ni
habari za kupuuza, alama hazijabadilika zimebaki kuwa zile zile
hazijabadilika" alisema Maulidi.
Lakini habari kutoka ndani ya Idara ya
Ukaguzi Elimu, Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza, zinasema uko mchakato unaoendelea
wa kufanyia mabadiliko alama hizo ndani ya Baraza la Mitihani huku Mkuu wa
Shule ya Sekondari Mukituntu, Ukerewe, Mwanza, Valence Magesa, akisema hawana
taarifa za ukweli wa mabadiliko hayo, wao wanajua zinazotumika ni zilizokuwapo
tangu zamani.
"Hapana. Hatujui kama kuna mabadiliko
hayo ya alama za madaraja ya ufaulu. Wakibadili si lazima walimu na wanafunzi
wawe na taarifa? Haya mabadiliko hayapo," alisema Magesa.
Habari kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi zinasema hata hivyo kwamba kwa muda sasa imekuwapo tofauti kubwa
kwenye mfumo wa kupanga alama na madaraja ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya
sekondari kati ya Baraza la Mitihani na shule.
Raia Mwema limeambiwa kutoka wizarani
kwamba zipo tofauti katika viwango vya alama zinazotumika, vya shuleni vikiwa
chini ya vile vinavyotumiwa na Baraza hatua ambayo inatafsiriwa na baadhi ya
walimu kuwa inachangia katika matokeo mabovu ya wanafunzi wao.
Taarifa zinasema kinachoichanganya zaidi
wizara sasa ni ukweli kwamba standardisation imekuwa ikifanyika kwa miaka nenda
rudi lakini matokeo hayakuwahi kuwa mabaya kama ilivyotokea mwaka jana.
Lakini msemaji wa Baraza la Mitihani, John
Nchimbi, katika kukoleza mkanganyiko wa matokeo hayo ya mwaka jana,
ameliambia Raia Mwema kwamba Baraza halijawahi kubadili alama za ufaulu.
“Sisi tangu Baraza lianzishwe hatujawahi
kubadili wastani wa masomo, wastani bado upo uleule. Hatuwezi kubadili bila ya
kuwashirikisha watu wa Wizara ya Elimu. Lazima tupate baraka zao, hata huko
nenda ukaulize watakueleza hivyo hivyo. Sijui kwa sasa wastani unaanzia
ngapi, lakini nitakufahamisha baada ya kupitia. Kwa sasa sina uhakika sana,”
alisema Nchimbi.
Mbali na mabadiliko ya gredi, mabadiliko
mengine yanayoelezwa kuchangia katika matokeo mabaya ya mwaka jana ni ya
ufundishaji na utungaji mitihani ambayo nayo hayakufanyiwa maandalizi ya
kutosha.
Chini ya mabadiliko hayo mwanafunzi
anayehitimu anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza, si kukariri, na
ufahamu wa masuala mbalimbali yakiwamo ya kitaifa na kimataifa.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Aquinas,
iliyoko Halmashauri ya Mtwara, Sister Maureen Cariaga OSB, anasema kubadili
mitaala ni jambo la kawaida kulingana na mazingira ya wakati husika, lakini
mabadiliko hayo yawe yamefanyiwa maandalizi ya kutosha.
“Hapa kwetu matokeo hayakuwa mabaya. Tuna
walimu wa kutosha na mahitaji yote yapo. Tunachuja vizuri wanaoingia kidato cha
kwanza, tunafuatilia maendeleo yao mpaka juu. Hata mchujo wa walimu ni mgumu
kidogo. Ninaweza kusema kwamba mabadiliko kutoka kwenye nadharia kwenda kwenye
ujuzi nayo yatakuwa yamechangia ushindi kushuka.
“ Hapakuwa na muda wa kutosha wa maandalizi
kwa walimu na wanafunzi. Si kwamba hili la mabadiliko ni jambo baya, hasha.
Lakini maandalizi ya kutosha ni muhimu. Tulitakiwa tujiandae pengine kuanzia
mwaka 2009,” anasema Sister Maureen ambaye shule yake ni kati ya zilizofanya
vizuri mkoani Mtwara.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bureza, Muleba,
Theonestina Deogratias, na makamu wake, Fredius Banywani,
wanalalamikia utungaji wa mitihani.
“Setting (utungaji) wa mitihani ulikuwa
tofauti na uliozoeleka,” anasema mwalimu Theonestina.
Alitoa mfano wa somo la Historia
kwamba mtihani ulitungwa kwa namna ambayo mwanafunzi alitakiwa ajieleze
kwa maneno yake kwa kuingia ndani zaidi na si kutegemea maelezo
aliyoyasoma kwenye kitabu peke yake.
Jambo kama hilo pia lililalamikiwa na Mkuu
wa Shule ya Katoke Lweru, Moir, ambaye alisema ya kuwa katika
mtihani wa Uraia, yalitungwa maswali yanayoegemea zaidi uelewa wa masuala
yanayotokea nchini na duniani kwa ujumla, masuala ambayo yanahitaji mwanafunzi
kuwa mfuatiliaji mzuri wa magazeti, redio na televisheni.
“Mwanafunzi anayesoma shule ya bweni si
rahisi kuwa mfuatiliaji wa vitu hivyo,” alisema.
Lakini ofisa mmoja wa elimu kutoka Ofisi ya
Elimu ya Mkoa wa Lindi ameliambia Raia Mwema kwamba matokeo mabaya ya wahitimu
wa mwaka 2012 hayawezi kuelezwa kwa sababu moja tu au mbili.
“Tunaweza kutaja mitaala au hata mabadiliko
hayo ya ufundishaji na utungaji, lakini ukweli unabaki kwamba hatutapata jibu
la hakika la nini kinachotokea mpaka sote tuamue kushughulikia elimu kwa jinsi
inavyopasa.
“Kwa hiyo ofisa elimu hana jibu la moja kwa
moja la nini hasa chanzo cha matokeo mabaya. Huko nyuma tulikwisha kusema
kwamba kwa Mikoa kama hii ya Lindi, iliyo pembezoni, ipewe upendeleo wa
kibajeti. Uamuzi huo ukakubalika lakini ukabaki kwenye nyaraka tu.
“Tuna Wakaguzi wa Kanda, lakini kawaulize
kwa mwaka jana walikagua shule ngapi? Hawana usafiri, na hata kama wakipata
gari, hawawezi kupata mafuta kwa sababu hakuna bajeti ya mafuta,” anasema ofisa
huyo akiomba asitajwe.
Msemaji wa Baraza la Mitihani, John Nchimbi
anasema Baraza la Mitihani halihusiki na mabadiliko katika ufundishaji. Kazi
hiyo ni ya taasisi nyingine.
“Sisi hatuhusiki katika mabadiliko ya
ufundishaji. Lakini Taasisi ya Elimu watakusaidia. Nakumbuka utaratibu wa
ufundishaji na kuandaa maswali ulibadilika tangu mwaka 2005, lakini mtihani wa
kwanza uliotungwa kwa muundo huo ulikuja miaka mitatu baadaye (2008).
“Katika mtindo huu mwanafunzi anafundishwa
kuelewa, si kukariri, yaani mwanafunzi anatakiwa kuelezea kwa kina namna
alivyoelewa. Hiyo ni tofauti na zamani kwani wakati huo mwanafunzi alikuwa
anaelezea kwa ufupi tu.
“Walimu walipewa semina na sisi baada ya
hapo tukaliacha suala hilo kwa Taasisi ya Elimu. Hatuhusiki tena, tunachosubiri
ni kuwatahini tu na kutoa matokeo,” alisema Nchimbi.
Wakufunzi wa Chuo cha Ualimu Katoke,
Muleba, Kagera, wanaeleza kasoro nyingi zilizosababisha ufaulu mdogo zikitokana
na elimu nchini kushuka kwa jumla.
Wanasema nia ya Serikali ya kutaka kila
mtoto afike sekondari bila kujali uwezo wake, imechangia pia kwa kiwango
kikubwa kufeli kwa wanafunzi wengi.
Wanasema ya kuwa nia ya Serikali ilikuwa ni
nzuri lakini utekelezaji wake umekuwa mbaya kwani uliingiliwa na
wanasiasa ambao wengi walifanya mbinu za kulazimisha wanafunzi wa
darasa la saba wafaulu kwa wingi kuingia sekondari.
Wanasema ya kuwa baadhi ya madiwani na hata
wakuu wa wilaya, walifanya kila linalowezekana kufaulisha wanafunzi wengi kama
mtaji wao wa kisiasa ili waonekane kuwa ni wachapa kazi hodari.
“Inapendeza masikioni kusikia kwamba shule
imefaulisha wanafunzi kwa asilimia 80 au 90, lakini hao wanafunzi wamefaulu kwa
kiwango cha kuridhisha au wamesukumwa tu?
“Hilo ndilo jambo la kujiuliza, na
ukichunguza utakuta wengi walisukumwa ili wanasiasa na watendaji waweze kutamba
kwenye majukwaa ya kisiasa,” alisema mwalimu mmoja wa Shule ya
Sekondari ya Bwanjai iliyoko Mugana, Wilaya ya Misenyi, Kagera, ambaye
hakutaka jina lake litajwe katika suala hilo.
Aliongeza: “Serikali inatamba kwamba
imeongeza shule za sekondari kutoka 1,700 hadi 4,000 ili wote waliofaulu
waingie sekondari, lakini ilijiandaa na changamoto za kuwa na walimu wa
kutosha? Kuwa na shule zenye maabara na maktaba? Jibu ni hapana. Sasa
tunashangaa vipi tunapokuwa na idadi kubwa ya waliofeli?”
Alisema ya kuwa shule nyingi zimejengwa
lakini nyingi zina matatizo mengi kama vile ukosefu wa nyumba za walimu na
hazina maabara wala maktaba kwa ajili ya watoto kujisomea.
“Mazingira kwa ujumla hayatoi nafasi kwa
mwanafunzi kuwa na ari ya kusoma, hivyo anakuwa pale shuleni kwa ajili ya
kuhudhuria tu masomo na si kusoma kwa nia ya kufaulu ili aendelee na elimu
ambayo tunasema haina mwisho,” aliongeza.
Ni habari ya wazi kwamba kwa muda
mrefu nchi ina upungufu mkubwa wa walimu, utafiti wetu kuhusu walimu,
hata hivyo, umeonyesha kitu cha ziada: Katika upungufu huo mkubwa, walimu wa
sanaa ni wengi kuliko wa sayansi, kiasi kwamba katika shule nyingi
zilizotembelewa na waandishi wetu, masomo ya fizikia, kemia, baiolojia na
hesabu hayafundishwi kwa vidato vya tatu na nne.
Shule ya Sekondari Rungwa ya
Manyoni, Singida ni kati shule zilizofanya vibaya katika mtihani wa kidato cha
nne mwaka 2012 kwa watahiniwa wote 18 waliofanya mtihani huo kupata daraja
sifuri.
Shule hiyo ambayo inamilikiwa na serikali,
ilianzishwa mwaka 2007 kwa nguvu za wananchi wa vijiji vitatu vya Rungwa,
Magembe na Kintanula ambavyo kwa pamoja vinaunda Kata ya Rungwa.
Ina upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi
na hesabu. Wanafunzi waliotahiniwa mwaka jana wanasema katika kipindi chote cha
miaka minne hawakuwahi kufundishwa masomo ya hesabu, fizikia, kemia na baolojia
kutokana na masomo hayo kukosa walimu.
Mmoja wa watahiniwa wa mwaka jana, Daudi
Reffi (23) anasema: “Waalimu wawili waliopo wanafundisha masomo ya sayansi ya
jamii tu kama historia, jiografia na yale ya lugha kama Kiingereza na
Kiswahili. Hatukuwahi kufundishwa masomo mengine.”
Daudi sasa ni dereva na fundi wa pikipiki
(bodaboda) na anasema hana mpango wa kusoma tena. Amekatishwa tama na hali ya
mambo.
Anaeleza: “Masomo tuliyofanyia mitihani ni
Historia, Kiswahili, Uraia na Kiingereza lakini hayo mengine ya sayansi hakuna
aliyefanya mtihani wake kwa kuwa hatukuwahi kufundishwa.”
Maneno ya Daudi yanathibitishwa na Kaimu
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mhangwa Masanja, ambaye anaeleza kuwa tangu
mwaka 2007, baada ya kuanzishwa, shule hiyo haikuwahi kuwa na walimu zaidi ya
wawili kwa wakati moja kwani kila walimu waliopangwa shuleni hapo hutafuta
uhamisho kabla hata ya mwezi kumalizika.
“Kwa sasa tupo walimu wawili tu ambao
tunalazimika kufundisha wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne,
na bado pia hakuna walimu wa masomo ya sayansi na hesabu ingawa kuna taarifa
kuwa wanakuja walimu wapya watatu,”anaeleza mwalimu Masanja.
Anaongeza mwalimu Masanja: “Kwa kweli hali
ni ngumu. Walimu wawili hawawezi kufundisha wanafunzi 113, kwa masomo yote, na
kumaliza syllubus itakayomfanya mwanafunzi kufanya mitihani yake kwa mafaniko”.
Moja ya sababu zinazofanya walimu kuikimbia
shule hiyo ni mazingira magumu ya shule hiyo ambayo iko zaidi ya kilomita 350
kutoka Makao Makuu ya Mkoa wa Singida, na kilomita 250 kutoka Manyoni, ambako
ni Makao Makuu ya Wilaya. Takwimu katika Mikoa ya Mbeya na Rukwa zinaonyesha
kuwa zaidi ya asilimia 90 ya walimu wa sekondari ni wa masomo ya sayansi jamii
ama sanaa. Walimu wa masomo ya sayansi hawazidi asilimia tano.
Miongoni mwa shule za sekondari
zilizotembelewa na waandishi wetu katika mikoa hiyo ni Shule ya Sekondari
Sumbawanga yenye walimu 37 na kati ya hao 32 ni walimu wa masomo ya sanaa,
lakini hayo ndiyo masomo ambayo wanafunzi wamefeli zaidi ikilinganishwa na ya
sayansi yenye walimu watano lakini wanafunzi wakifaulu zaidi.
Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Sumbawanga,
Modesta Kivagala, anathibitisha hoja ya wingi wa walimu wa masomo ya sanaa
katika shule yake na matokeo mabovu ya wanafunzi katika masomo hayo.
“Walimu wa arts ni wengi lakini ndiyo
masomo ambayo wanafunzi wanafeli zaidi, walimu wa sayansi ni wachache lakini
wanafanya kazi, hapa shuleni tupo walimu 37, kati ya hao walimu 32 ni wa masomo
ya arts,” anasema.
Kwa mujibu wa matokeo ya elimu ya kuhitimu
kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Sumbawanga, kati ya
wanafunzi 151 waliofanya mtihani, 85 walifeli, 61 waliambulia daraja la nne,
sita daraja la tatu na wanne daraja la pili.
Hali hiyo ya kuwa na walimu wengi wa masomo
ya sanaa katika shule za sekondari nchini inajitokeza hata katika Shule ya
Sekondari Ipepa iliyopo katika Kata ya Molo eneo la Makuzani, wilayani
Sumbawanga. Pamoja na na shule hiyo kuwa na idadi nzuri ya walimu, wanafunzi 62
kati ya 87 waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya sekondari mwaka jana
walifeli. Alifaulu mmoja kwa kiwango cha daraja la tatu, 13 daraja la nne huku daraja
la kwanza na la pili wakikosekana.
Akizungumzia hali ya matokeo katika shule
hiyo, mwalimu Diwed Kikoti anasema: “Walimu wapo wa kutosha. Lakini wengi ni wa
masomo ya arts.”
Tatizo la bajeti ya elimu limekuwa
likijirudia katika maoni ya utafiti na hali mkoani Shinyanga inaelezea jinsi
bajeti ilivyo na umuhimu.
Kwa Wilaya ya Shinyanga; mwaka 2012/2013,
wakati shule za msingi zilitengewa Sh. bilioni moja kwa mwaka huo, na Sh. 25m
za matumizi mengine kwa mwezi, shule za sekondari zilitengewa Sh. 309m kwa
mwaka na Sh. 2m tu za matumizi mengineyo kwa mwezi, kiasi ambacho hakiwezi
kukidhi ukaguzi na uendeshaji wa shule hizo, licha pia kwamba fedha
hazipatikani kwa wakati mwafaka; na hata zinapopatikana mara nyingi zimetumika
kwa shughuli tofauti kwa Halmashauri za Wilaya na Miji zenye kukabiliwa na
ukata mara kwa mara, kwa lengo la kuzirejesha baadaye, wakati huo huduma kwa
shule hizo zikiendelea kudidimia.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya
Kasulu, Kigoma, Simoni Humbi anasema tatizo jingine ni kwamba baadhi ya walimu
kuanzia ngazi ya msingi na sekondari hawana moyo wa uzalendo kwa Taifa lao na
ndiyo maana hata shule zao zinapofanya vibaya wanashangilia badala ya
kusikitika.
Anasema zamani wakati Watanzania wamejawa
na uzalendo kwa Taifa lao, walimu walikuwa wakisikitika na baadhi yao kufikia
hata hatua ya kutoa machozi pindi shule zao zinapotoa matokeo mabaya, lakini
katika miaka hii ya sasa hakuna mwalimu anayeshtuka wala kusikitishwa na
matokeo mabaya.
Akizungumzia hoja za kwamba mishahara
midogo kwa walimu na Serikali kutowajali na kutowalipa stahili zao ndicho
chanzo cha kuporomoka kwa elimu nchini alisema kwa uzoefu wake wa takriban
miaka 40 katika utumishi wa umma, hakuna watumishi serikalini wanaopewa
kipaumbele katika madai yao kama kada ya ualimu.
“Dhana ya uzalendo imeshuka. Siku hizi
hakuna uzalendo wa mwalimu kwa mwanafunzi wake. Zamani mwanafunzi akifeli,
mwalimu anasikitika kweli kweli…lakini leo, mwanafunzi akifeli walimu
wanapongezana. Tukiweka utaifa mbele, elimu yetu itarejea kwenye mstari. Kuna
shule zina kila kitu, lakini wanafunzi wamefeli,” alisema Humbi.
Mmoja wa wadau wa elimu nchini, Mwenyekiti
wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, anasema dawa ya matatizo ya elimu
nchini ni kuirejea ripoti ya Tume ya Makweta.
“ Mwishoni mwa miaka ya 1970, na mwanzoni
mwa miaka ya 1980, Mwalimu Julius Nyerere aliona matatizo ya mfumo mbovu wa
elimu na ndiyo maana kabla ya kuondoka madarakani, yaani mwaka 1981, aliunda
tume ya Jackson Makweta, kuangalia namna ya kupata mwongozo sahihi kwa mfumo wa
Kitanzania unaoendana na desturi zetu, ili tushindane na ulimwengu kupambana na
maadui watatu.
“Miaka miwili baadaye tume ya Makweta
ilikamilisha kazi yake lakini ripoti haikufanyiwa kazi mpaka 1995 ndipo
ikaandikwa Sera ya Elimu ya Taifa ambayo chini ya aliyekuwa waziri wa elimu
wakati huo, Profesa Philemon Sarungi, “ anasema Mbatia.
Anasema Mbatia kuhusu ripoti hiyo ya
Makweta: “ Ripoti hiyo ya wakati wa Sarungi ilikuwa na makosa sana, yaani kwa
kifupi ilichakachuliwa.”
Kwa mujibu wa Mbatia, bila pia kuwahudumia
ipasavyo walimu ni ndoto kuirejesha elimu mahali pazuri kwa vile matatizo
yanayowakumba walimu ni kukosa kuthaminiwa, mazingira mazuri ya kufanya kazi
ikiwemo kulipwa stahili zao kwa wakati na makazi.
“Hakuna uwiano sawa wa walimu na wanafunzi.
Ni kawaida mwalimu mmoja wanafunzi 25, lakini huko mikoani na hata Dar es
Salaam kuna shule zina walimu wawili tu ama watatu, walimu vijijini wanakimbia
kwa sababu hakuna heshima, hawapewi motisha, mazingira ya kazi ni mabovu.
“Niliwahi kutembelea Mkoa wa Kigoma, Kata
ya Nyangabo, Shule ya Msingi Reli Mpya, pale mwalimu mkuu hana pa kulala,
kuna kibanda ni ofisi ya mtu anasubiri ofisi ikifungwa ndipo alale. Nimekagua
madaftari ya wanafunzi wameandika makosa na wamewekewa tiki. Unamuandaa vipi
mtu huyu kufaulu mtihani wa kidato cha nne,” alihoji Mbatia. Wadau wa elimu
wakiwamo walimu wa muda mrefu, maofisa wa elimu na hata watumishi wa idara
mbalimbali zinazosimamia elimu wanalinyooshea kidole Baraza la Mitihani la
Taifa, wakielezea kuwa limechangia kwa kiasi kikubwa matokeo mabaya na
mkanganyiko katika matokeo.
Maeneo ambayo wadau hao wanayataja ni
pamoja na ubadilishaji wa mifumo na wataalamu bila kuwapo maandalizi ya kutosha
pamoja na kutokuwapo kwa umakini miongoni mwa watendaji wa Baraza katika kusimamia
mifumo mipya iliyoingizwa kwa nia ya kuboresha mitihani.
“Hadi sasa mitambo mipya iliyofungwa na
baraza inasumbua kwa sababu tu uongozi ulilazimisha kuondoa mifumo ya zamani
kwa haraka badala ya kufuata ushauri uliotolewa na wataalamu kwamba mitambo mipya
ifanye kazi sambamba na mifumo ya zamani ili kuepuka mikanganyiko inayotokea
sasa,” anasema mtaalamu mmoja ambaye ni mtumishi mwandamizi serikalini.
Anasema pamoja na kufungwa kwa mitambo
mipya, wataalamu ambao waliandaliwa kwa kazi hiyo waliondolewa na kuwekwa wapya
ambao hawajaandaliwa wala kufanyiwa tathmini ya weledi na maadili yao na hivyo
wanashindwa ama wanafanya kazi chini ya kiwango. Mfano wa matatizo ya wataalamu
hao ni mkanganyiko uliotokea kwa matokeo ya mitihani ya elimu ya Dini ya Kiislamu
na matokeo mengine ambayo baadhi ya wanafunzi walibainika kupewa alama
wasizostahili.
Mkanganyiko katika mitihani ya elimu ya
Dini ya Kiislamu ulitokana na uzembe katika kuingiza alama katika mitambo bila
kubadili kifaa cha kufanyia hesabu na hivyo kusababisha kuwapo kwa hisia potofu
kwamba wahitimu walionewa kwa sababu ya imani zao.
“Islamic Knowldge walifanya mitihani miwili
badala ya mitatu iliyozoeleka, sasa mashine ya kugawanya haikurekebishwa
ikaachwa igawanye mara tatu wakati mitihani ilifanywa miwili, matokeo yake
wahitimu wote walipunjwa alama za jumla,” anasema mtumishi huyo wa serikali.
Msemaji wa Baraza la Mitihani, John
Nchimbi, anakiri tatizo hilo akisema, “Mashine inasetiwa kuchakata matokeo,
miaka yote mtihani wa dini ya Kiislamu ilikuwa inafanyika kurasa tatu, baada ya
mtaala kubadilika ikawa inafanyika karatasi mbili. Na mashine ikawa imezoea
kuchakata karatasi tatu ikawa inagawanya kwa tatu badala ya mbili.
“Kulikuwa na technical problem wanafunzi wa
somo la Dini ya Kiislamu wanafunzi wakawa wanapata alama pungufu. Lakini tatizo
hilo tulilibadilisha haraka baada ya kuligundua,” anasema Nchimbi bila kueleza
hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika, ambao wanahusika pia na kuathiri
watahiniwa katika mitihani mingine.
Eneo la usahihishaji nalo limezungumzwa na
wadau mbalimbali wakiwamo watumishi wa idara za elimu katika wilaya mbalimbali
na walimu, ambao wanasema kwa sasa utaratibu wa upatikanaji wa wasahihishaji
umekuwa hauzingatii viwango kama zamani na hivyo kujikuta wakienda wasahihishaji
wasio na uwezo na wasio waadilifu.
“Kwa kweli sasa ni tatizo maana walimu
wenye uzoefu na waadilifu siku hizi wanaachwa na wanakwenda watoto wadogo ambao
hawana uwezo na wasiojali maadili ya kazi na hivyo kwenda kufanya kazi kwa
maslahi yao na si kuzingatia maadili,” anasema Ofisa Mwandamizi wa serikali
kisiwani Pemba, ambaye ni mwalimu kitaaluma.
Kutokana na baadhi ya wasahihishaji
kutokuwa na uzoefu, na kulipwa kwa kila nakala za mtihani wanazosahihisha,
baadhi wamekuwa wakifanya kazi kwa haraka kiasi cha kupoteza umakini ili waweze
kupata malipo zaidi.
Msemaji wa Baraza, John Nchimbi anakiri
kuhusu wasahihishaji kulipwa kwa jinsi hiyo lakini anasema hana takwimu ni
kiasi gani wanalipwa kwa kila mtihani lakini akitaja vigezo vya walimu
wanaopewa kazi ya kusahihisha mitihani kuwa ni:
“Anayefaa kusahihisha kidato cha nne awe
mwalimu ambaye ameshafundisha miaka mitatu tangu amepata diploma ya ualimu. Kwa
kidato cha sita ni yule ambaye amefundisha miaka mitatu tangu amepata shahada
ya ualimu.
“Namna tunavyowapata tunatuma barua kwa
mikoa yote na katika barua hiyo tunaambatanisha vigezo vyetu. Mwalimu Mkuu
anapendekeza majina na sisi tunatuma katika kamati za mitihani mkoa, wao
wanaangalia nidhamu na vigezo vingine.
“Pia tunataka mwalimu awe na afya nzuri
maana zoezi la usahihishaji linachukua muda mrefu, ni mwezi mmoja kwa kidato
cha nne, kidato cha sita ni siku 19 mpaka 20. Lakini chochote kinaweza kutokea
kutokana na jinsi mitihani ilivyo,” anasema Nchimbi.
Hayo yakiendelea timu yetu ya watafiti
imepata taarifa kwamba baadhi ya wasahihishaji wa mitihani ya mwaka jana
walirejeshwa vituoni kwao kutokana na kugundulika kuwa hawakuwa na vigezo
tosha.
“Kwa kawaida mwalimu akija kituoni kuanza
zoezi la usahihishaji lazima awe na barua kutoka kwa Mwalimu Mkuu, na akija
mwalimu ambaye hana utambulisho huwa tunamrudisha alikotoka. Sijasikia kuhusu
walimu waliorudishwa mwaka jana lakini kama walikuwapo sishangai maana
walisharudishwa wengi kwa mtindo huo wa kudanganya.
“Kwa kawaida walimu ambao watafukuzwa kwa
kutotimiza vigezo tunachukua walimu wengine walio katika (data base yetu),
maana tuna taarifa za walimu waliowahi kuitwa miaka ya nyuma. Tunaagiza walimu
wakuu wa shule husika ili kama walimu hao wapo kazini
tunawaita kuziba ombwe hilo.”
source: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment