Mwandishi wa safu katika magazeti
mbalimbali nchini, Maggid Mjengwa amekamatwa na polisi kwa tuhuma za
kuhusika na tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana
mchana na baadaye kuthibitishwa na polisi zinasema Mjengwa alikamatwa
muda wa asubuhi na kwamba alikuwa akihojiwa na makachero wa jeshi hilo
hadi alasiri kuhusu tukio la kuteswa kwa Kibanda.
Msemaji Mkuu wa Polisi Advera Senso aliliambia Mwananchi kwamba:
"Ni kweli kwamba tunaye, tunaendelea
kumhoji, tunachoomba ni kwamba mtupe nafasi ili tufanye kazi yetu na
kukiwa na jambo lolote tutawajulisha."
Hata hivyo, Senso hakuwa tayari
kueleza kwa undani muda aliokamatwa Mjengwa wala sababu za kukamatwa na
kuhojiwa kwake, lakini chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi
kilithibitisha kwamba pamoja na mambo mengine kuhojiwa kwake kulihusu
uteswaji wa Kibanda.
Jumatatu wiki hii, Kaimu Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai Nchini, Issaya Mngulu alisikika akizungumza na Kituo
cha Radio One cha Dar es Salaam kwamba kesho Jumatatu (April 15, 2013)
polisi watatoa taarifa rasmi ya hatua waliofikia katika upepelezi wa
kesi ya Kibanda.
Kwa upande wake Mia Mjengwa ambaye ni
mke wa Mjengwa, alisema mumewe alipata wito kutoka polisi makao makuu
Alhamisi na kwamba juzi Ijumaa alisafiri kutoka Iringa kwenda Dar es
Salaam kuitikia wito huo.
"Ninachojua ni kwamba aliitwa kwenda
polisi na leo (jana) alinipigia simu kama saa 7:00 mchana na aliniarifu
kwamba yupo polisi, sasa tangu wakati huo sijaongea naye tena na wala
simu zake hazipatikani," alisema Mia na kuongeza: "Kwa hiyo mimi kwa
kweli sifahamu kwamba anahojiwa kwa sababu gani."
Taarifa za kukamatwa kisha kuhojiwa
kwa Mjengwa ambaye pia ni mmiliki wa Mjengwa Blog, zimekuja siku chache
tangu msaidizi wake katika Blog hiyo, Joseph Ludovick akamatwe, kuhojiwa
kisha kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.
Ludovick alifikishwa mahakamani pamoja
na Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Willifred Lwakatare wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi na
kupanga kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky.
Kuteswa Kibanda
Machi 5, mwaka huu saa 5.30 usiku,
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Kampuni ya New
Habari (2006) Ltd, alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu
wasiojulikana nyumbani kwake kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.
CHANZO
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment