Ndugu zangu,
Ndugu yangu January Makamba alipata kuyasema haya, Desemba 9, 2012 pale Nkrumah Hall;
“ Msituone sisi wanasiasa
tunakumbatiana mkadhani wote tunapendana. Tukivua mashati mkaangalia
migongo yetu mtaona alama za mikuki!”- January Makamba
Nilikuwepo pale Nkrumah Hall,
nilimsikia ndugu yangu January Makamba akiyatamka hayo. Kuna waliocheka,
lakini kuna tuliobaki tukitafakari. Nitarudi kwenye tafsiri ya kauli
hiyo ya January.
Lakini kwanza, nianze kwa kukiri kuwa
nimechelewa kufuatilia mjadala huu hapa jukwaani juu ya ‘ Ludo
kurubuniwa’ na mengineyo kuhusiana na sakata la Ludo kama anavyojulikana
humu na Lwakatare.
Ukweli nilikuwa mapumziko ya Pasaka
mbugani Ruaha kwa siku kadhaa nikiwa na familia yangu. Hivyo, kuwa mbali
na mitandao na habari nyingine za dunia.
Ndugu yangu Zitto,
Umeandika yafuatayo kwenye jukwaa hili, nakunukuu;
“Nimeshtushwa sana na habari
ninazoendelea kuzipata kuhusu bwana huyu. Nimesoma pia maandiko yake
hapa na hasa maandiko dhidi yangu yenye maneno makali kweli. Kikweli
sikujua kabisa kama bwana huyu alikuwa kitengo muhimu kama cha usalama
kwenye chama changu ambacho mimi ni Naibu Katibu Mkuu.
Hata hivyo muhimu kuacha haki itendeke. Sio vema kumhukumu sasa mpaka ukweli wote ujidhihirishe.
Napenda kukumbusha kwamba Ukweli
hautengenezwi, bali hutafutwa. Mwisho wa siku tutajua huyu bwana alikuwa
anafanya kazi ya nani na kwa nini? Kwa nini yeye atekwe siku moja na
Mhariri Kibanda na awe miongoni mwa watu wa mwanzo kufika hospitali
kumwona Kibanda.
Ningependa pia ndugu yangu Maggid aweke wazi na kinaga ubaga mahusiano yake na bwana Ludovick. “
Ndugu yangu Zitto,
Nimeamua kwa makusudi kukaa kimya na
kutoshiriki kuchangia au kujibu michango ya wengine na haswa linapotajwa
jina langu kwa namna moja au nyingine. Nafanya hivyo sasa nikiamini,
kuwa Zitto hukuwa mitandaoni, kwamba ulikuwa kambini ( JKT) na pengine
hukuweza kuyasoma maelezo yangu ya ufafanuzi wa jinsi nilivyofahamiana
na Ludovick na hata hatua nilizochukua mara sakata la Ludovick na
Lwakatare pale Machi 17 lilipowekwa wazi kwenye moja ya magazeti kuwa
ni ‘ tuhuma dhidi ya kushiriki kupanga njama za ugaidi’.
Ndugu yangu Zitto,
Nakufahamu zaidi wewe kama Zitto
kuliko ninavyomfahamu Ludovick ambaye nilimfahamu kaka kijana
mwanaharakati aliyekuwa akifuatilia makala zangu tangu jarida la Rai.
Alipata kunipigia simu na kuniomba kukutana nae kama ilivyo kwa wengi
ambao hupenda wakutane na kuzungumza nami mbali ya kusoma makala zangu
au kunifuatilia kwenye blogu. Bila shaka hali hiyo inakukuta wewe Zitto
pia.
Ni katika namna hiyo, ikatokea kwa
Ludovick kunisaidia na kazi za kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog na
kunisaidia kunipelekea, kwa niaba yangu, ankara zangu kwa Watangazaji
wa kwenye Mjengwablog kama vile Vodacom na Benki ya Azania. Ni kwa
sababu mimi kwa miaka kumi sasa naishi na kufanya kazi nikiwa Iringa na
kwamba ofisi nyingi ziko Dar.
Ndugu yangu Zitto,
Kwa zaidi ya miaka 25 sasa, kupitia
kalamu yangu ninekuwa nikifanya kazi ya jamii. Na jamii ina maana ya
watu. Kuna wakati nilimwambia jamaa yangu mmoja, kuwa leo hii
nikitembelea Gereza lolote lile hapa Tanzania, yumkini nitakutana na
maafande wawili au watatu wa Jeshi la Magereza wanaonifahamu kupitia
makala zangu pengine tangu enzi za Rai. Na kwamba, kama nitaingia
kutembelea ndani gerezani, yumkini nitakutana na wafungwa hata kumi
ambao wananifahamu kupitia makala zangu za tangu enzi za Rai.
Sasa nikisimama na kuongea na wafungwa
hao ambao wengine wamefungwa kwa makosa ya ujambazi kuna atakayedhani
kuwa Maggid huyu lazima atakuwa mhalifu na pengine jambazi, maana
inakuwaje amefahamiana na wahalifu walio gerezani!
Naam, kwa kazi zetu hizi za kijamii,
huwezi ukamtilia mashaka kila mwanajamii unayekutana nae barabarani,
anayeongea nawe kwenye simu au anayetaka kukutana nawe mzungumze.
- mimi kama mtu mzima, ninapokutana na kijana wa Kitanzania anayeonyesha kufuatilia maandiko yangu na kazi zangu za kwenye blogu, kisha akaonyesha kuwa na utayari wa kunisaidia kutuma picha au ku-upload kazi za mtandaoni ikiwamo magazeti ambayo Dar yanapatikana mapema zaidi, na mimi nina shida ya usaidizi huo, ni kwa nini basi nishindwe kushukuru kujitolea kwake?
Mjengwablog inatembelewa na watu
wengi. Kazi zimekuwa nyingi sana. Ni chombo cha habari kama vingine,
lakini, hakifanyi mauzo kama ya magazeti na wala hakipewi ruzuku ya
Serikali, na mara nyingi hata matangazo hatupati tukaweza kujiendesha
ikiwemo kuajiri.
Hivyo, tunategemea pia watu wa
kujitolea katika kuifanya kazi yetu ya kijamii. Na pale inapopatikana
posho kidogo tunawapa wanajiotolea lakini hatuwezi kuita ni mishahara.
Ninao vijana wanaoendelea kujitolea kwenye Mjengwablog na gazeti la
mtandaoni la Kwanza Jamii, wawili wako Iringa, na kwa sasa Dar sijapata
mtu wa namna hiyo. Namtafuta.
Ndugu yangu Zitto,
Katika Tanzania hii, kama wanahabari
na wanaharakati wa mitandaoni wangepewa jukumu la kutuhumu, kukusanya
ushahidi, kuendesha mashtaka na kuhukumu, basi, Watanzania wengi
nikiwamo mimi nduguyo tungeshakuwa gerezani siku nyingi sana.
Ni bahati njema vyombo vyetu vya
usalama, licha ya kufuatilia ya magazetini na kwenye mitandao, vinafanya
kazi zao kwa weledi. Naamini kabisa, siku ambayo vyombo vyetu vya
usalama vitaona haja ya kuniita na kunihoji kuhusiana na nilivyomfahamu
Ludovick, vitafanya hivyo kwa kuzingatia taaluma yao inavyowaelekeza na
si kwa mashinikizo ya magazetini na mitandaoni. Mpaka sasa sijapata hata
‘ miss call’ moja ya kutoka vyombo vya usalama, na hiyo haimaanishi
kuwa hawaijui kazi yao. Kama kutakuwa na haja ya wanazo namba zangu na
wanajua hata ninapoishi.
Ndugu yangu Zitto,
Nilichojifunza kutoka kwenye kauli ya
January Makamba ni ukweli, kuwa si wanasiasa tu ambao hampendani, bali
hata baadhi yetu wanahabari na tunaojiiita wanaharakati hatupendani pia.
Katika hili la Ludovick na Lwakatare
kuna miongoni mwetu waliohangaika na wanaozidi kuhangaika kutafuta hata ‘
link nyepesi’ tu ya kumwuingiza, kwao wao, ni ‘ Mwanahabari na bloga
maarufu Maggid Mjengwa’ kwenye hili sakata la Ludovick na Lwakatare.
Na ikiwezekana, mimi Maggid,
niorodhoshwe kama mtuhumiwa wa kupanga njama za kumdhuru Kibanda na
wanahabari wengine. Tukifika hapo ndipo kitakuwa kilele cha furaha yao.
Watakunywa mvinyo na bia. Watafurahi. Halafu iweje? Unajiuliza.
Ndugu yangu Zitto,
Ndivyo Watanzania tulivyo. Tunafurahia
maanguko ya wenzetu, na hasa wale tuliotoka nao chini kwenye taaluma na
wakaonekana kupanda chati kwa haraka. Mimi Maggid ni raia wa kawaida tu
ninayejitahidi siku zote kuishi maisha adilifu na ya kujikimu.
Lakini, kwa wengine, mimi kuwa na
Mjengwablog yenye umaarufu na hata kuanzisha kijarida cha kijamii cha ‘
Kwanza Jamii’ ni nongwa kwao. Ni yale yale ya mafarisayo walipomshangaa
Yesu kwa kusema; “ Hivi ni Yesu huyu huyu mwana wa Joseph Fundi
Seremala?!”
Ndio, moja ya matatizo yetu ni kutokuwa na wivu wa maendeleo, bali wivu dhidi ya wenye kujaribu kupiga hatua za maendeleo.
Ndugu yangu Zitto,
Kufikiri tu wazo la kutuhumu nayo ni
tuhuma. Wanaonifahamu, bila shaka nawe ukiwemo, hawawezi kufikiri wazo
la mimi kushiriki kupanga njama ya kumdhuru mwanahabari wa Tanzania au
popote pale duniani, kumdhuru raia wa Tanzania au popote pale duniani.
Ukweli huo hapo juu nilipata kumweleza ndugu yangu Ansbert Ngurumo
kupitia jukwaa hili alipohoji mimi kusitisha rasmi usaidizi wa Ludovick
kwenye Mjengwa blog kuanzia Machi 17.
Ansbert pia aliniuliza; je, kama wewe ( Maggid) utahisiwa au kutuhumiwa kuhusika na suala la Kibanda ina maana utaacha kublogu?
Ndipo nikamjibu;
Kuwa kusitisha usaidizi wa Ludovick
kwenye Mjengwablog ni kumsaidia Ludovic kutokuhusishwa na yanayofanyika
Mjengwablog kwa sasa ikiwamo machapisho wakati yuko kwenye kesi.
Nikasema, kuwa sisi wenyewe (
wanahabari) kilio chetu siku zote kimekuwa kuwataka watendaji Serikalini
an kwingineko wanapokumbwa na tuhuma wakae pembeni kwa maana ya
kujiuzuru kupisha uchunguzi, lakini, katika hili la Ludovick hatuoni
kama hilo ni muhimu!
Kwenye hoja yake ya pili nikamjibu;
Kuwa kama atatokea Mtanzania mwenye
akili timamu, akatoa tuhuma dhidi yangu, mimi Maggid Mjengwa, kuwa
nahusika na kuratibu au kupanga njama za kumdhuru mwanahabari wa
Tanzania au popote pale duniani. Kumdhuru raia wa Tanzania au popote
pale duniani, basi, hata kama atakuwa na ushahidi mmoja tu wenye
mashiko, itatosha kwangu kuacha mara moja kufanya yote yale ya kijamii
kwa kutumia kalamu yangu. Bahati mbaya au nzuri, ndugu yangu Ansbert
hakurudi tena kuendelea na mjadala ule.
Ndugu yangu Zitto,
Ndio, mwenye kunifahamu hawezi
kufikiri wazo la mimi kupanga njama za kumtendea uovu mwanahabari au
raia wa Tanzania. Ndio maana kuna wengi pia wamenipigia simu za kunipa
pole ya juu ya kilichotokea na jina langu linavyotajwa kwa dhamira ovu.
Alfred Mwambeleko ni kijana kada wa
Chama Cha Mapinduzi. Huyu ananifahamu tangu tukiwa wote Sangu Secondary
‘ A’ Level. Yeye na mimi, tukiwa wanachama wa CCM-Youth mwishoni mwa
miaka ya 80, tulishirikiana kuandaa mijadala ya wazi pale shuleni ili
vijana wajizoeshe kutoa fikra zao huru mbele ya watu.
Majuzi hapa Mwambeleko alinipigia
simu nikiwa Iringa. Alisoma jarida la moja la kila wiki akiwa na wenzake
kwenye ofisi ndogo ya CCM, Lumumba. Ni kuhusiana na sakata la Ludovick
na Lwakatare. Alfred Alinipigia simu kunipa pole na akatamka;
“ Nimewaambia jamaa zangu hapa, kuwa Maggid is innocent”
Ni kwa nini basi ndugu yangu Alfred awaambie wenzake kuwa mimi ni ‘ innocent’?
Jibu; ni kwa sababu , coverage ya
jarida lile ilionyesha kunituhumu mbele ya jamii. Na kuna jarida
lingine la kila Jumapili lilifanya hivyo pia. Niliongea na wahariri
wake kuwaeleza masikitiko yangu. Walikuwa waungwana, walinielewa. Maana,
huwezi kuandika fulani ni mtu wa karibu wa fulani wakati unajua kabisa
maana ya ‘ Mtu wa karibu’. Huwezi pia kuandika fulani ni mwajiriwa wa
kampuni fulani wakati huna ushahidi huo na Mkurugenzi wa kampuni
anapatikana kuweza kuthibitisha au kukanusha.
Ndugu yangu Zitto,
Wewe pia ni mhanga wa ninaouita
‘Uandishi wa habari usio wa kuwajibika’. Juzi tu umekanusha habari kuu
kwenye moja ya majarida yetu ikidai kuwa kulikuwa na njama za wewe
kuwekewa sumu. Ukatamka kuwa ni Uongo Mtupu! Nilidhani gazeti lile
lingethibitisha ilichoandika ili tujue nani mkweli na nani mwongo.
Halikufanyika- Irresiponsible journalism!
Imefika wakati magazeti
tuliyoyategemea yatuletee habari za kina na zilizofanyiwa uchunguzi
kimsingi wanatuletea ‘ udaku’. Na wenye kuandika udaku mara nyingi huwa
hawataki – ku-balance story. Kwenye udaku kubalance story ina maana ya
kuua udaku wenyewe, maana hakutakuwa na story ya kidaku. Inasikitisha
kwamba tumefika hapa.
Ndugu yangu Zitto,
Hata mimi nastushwa na habari
ninazoendelea kuzipata kuhusu Ludovic. Sijutii kuyafanya maamuzi
niliyoyafanya ya kumsitisha mara moja Ludovic kufanya usaidizi kwenye
Mjengwablog.
Inatosha tu mtu kutuhumiwa ili kuchukua hatua. Ni kumpa nafasi pia mtuhumiwa, ni kumsaidia. Ni wajibu wa kiraia. Kizalendo.
Pale Oyesterbay Police kuna rekodi
yangu ya kumripoti mdogo wangu wa tumbo moja; baba mmoja na mama mmoja,
kwa kutuhumiwa kutenda kosa la jinai.
Ni miaka kadhaa iliyopita, nilimkamata na kumpeleka mwenyewe kituoni akaandikishwe maelezo na afunguliwe mashtaka na Jamhuri.
Ndugu zangu hawakuinelewa. Lakini leo
wamenielewa. Kuwa kijana yule ndugu wa damu sasa amejitahidi kuwa raia
mwema. Hajapatikana na makosa mengine ya jinai. Na kijana mwenyewe, kwa
maana ya mdogo wangu, anatambua sasa kuwa nilimsaidia.
Nayasema nikiwa na maana, hakuna
Mtanzania au mtu mwingine yeyote ninayeweza kushirikiana nae kufanya
uhalifu au kumlinda nikigundua kuwa amefanya uhalifu. Nitamripoti.
Siku ile ya Desemba 9, pale Nkrumah nami nilipata fursa ya kuongea. Nilizungumzia mambo mamkubwa mawili; haki na wajibu.
Nikatoa mfano wa kisa cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wakati wa Tony Blair, aliitwa Jack Straw.
Ilitokea asubuhi moja, Jack Straw
alisoma gazetini kuwa mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani amewatoroka
maaskari wa barabarani baada ya kutenda kosa la barabarani.
Jack Straw baada ya kusoma hayo,
akamchukua mwenyewe mtoto wake na kumpeleka kituo cha polisi. Waandishi
wa habari walikusanyika kutaka kumsikia Waziri mwenye dhamana ya
Usalama.
Jack Straw akatamka; “ Nimemkabidhi
mwanangu kwenye mikono ya polisi, nikiamini kuwa atashughulikiwa kwa
mujibu wa sheria za nchi bila kujali kuwa ni mtoto wa Waziri wa Mambo ya
Ndani. Lakini, nimewaambia pia Polisi, kuwa wasimkandamize mwanangu ,
kwa vile tu ni mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani.”- Jack Straw.
Hapo tuna ya kujifunza juu ya haki na wajibu.
Ndugu yangu Zitto,
Nimeandika sana. Lakini nimalizie na kauli yako kuwa; Ukweli hautengenezwi, bali hutafutwa”. Ni sahihi kabisa.
Lakini labda nichokoze swali la
kufikirisha; Tunafanyaje basi pale tunapotambua ukweli mwingine, kuwa,
kwa wengine, ukweli wanauumba. That, they are simply crafting lies!
Sijaufunga mjadala, ingawa sitajadili yaliyo mahakamani.
Maggid Mjengwa,
Iringa
No comments:
Post a Comment