WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, April 2, 2013

Tunatembea duniani kote lakini hatuoni, hatujifunzi mbali na kununua bidhaa dhaifu

 
Hadi sasa rai yangu imekuwa kwamba hatuna budi kujifunza kujenga mitazami ya mbali, mitazamo inayotia maanani kwmaba sisi si wageni hapa, siis si watu wa kupita, sisi ni watu wa kudumu na tumedhamiria kuwa tutaendelea kuishi hapa kwa muda mrefu ujao, hata miaka milioni ijayo, kizazi kimoja kikikirisha kizazi kifuatacho nchi iliyo bora kuliko kilichoirithi chenyewe.

Uimara wa fikra za jamii inayojoona kama ya kudumu hujidhihirsha katika fikra za watu wake lakini pia katika matendo watendayo kutokana na fikra hizo. Jamii ya kudumu haiamki siku moja na kuamua kufanya jambo ambalo haijalitafakari kwa muda muafaka na kwa mashauriano maridhawa. Haikurupuki na kufanya maamuzi ya kukidhi haja ya leo bila kaungalia maslahi yake yataathirika vipi kutokana na maamuzi ya muda mrafu yaliyoangalia matatizo ya mpito.

Kweli, mara kwa mara, hutokea kwamba matatizo ya mpito yakawa ni kikwazo muhimu kinachoathiri maendeleo katika mtazamo wa masafa marefu, mbali, na hayana budi kushughulikiwa kama matatizo ya mpito. Hata hivyo jamii makini itayaweka bayana, na itakuwa ikijikumbusha kila mara, kwamba hatua zinazochukuliwa sasa ni za mpito zinazoshughulikia tatizo la mpito ili kupisha njia kwa hatua za kudumu kuchukuliwa.

Miaka nyuma nilikwisha kutoa mfano (katika safu hii hii) wa usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na kuporomoka kwa shirika la Usafiri Dar es Slaaam (UDA) mwanzoni mwa miaka ya 1980, baada ya kuwa limelirithi Dar Motor Transport (DMT), lililokuwapo tangu enzi za ukoloni.

Hapa ningependa kurejea wazo langu la siku zote, kwamba katika jamii ya maendeleo, ni marufuku kabisa kwa leo kuwa duni kuliko jana kwani kila siku mpya haina budi kuwa bora kuliko ilyoitangulia, na inapotokea kwamba jana ikawa bora kuliko leo na kesho ikawa duni kuliko leo, ni dhahiri kuna ugonjwa ful;ani katika jamii husika ila tu iwapo kuna maelezo mahsusi ya hali hiyo siyo ya kawaida.

Sasa, mwaka 1983, aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania, hayati Edward Sokoine, alitangaza kuruhusu magari madogo ya abiria kutoka miji ya Moshi na Arusha kutoa huduma ya “muda wa mpito” kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam wakati serikali ikifanya “mipango ya kudumu” ya usafiri wa umma katika jiji hili linalokua kila uchao.

Leo, miaka 30 u shei imepita, na zile “dala dala” za “mpito”  za Sokoine zimekuwa ni sehemu ya sura ya kudumu ya Dar es Salaam, kama ilivyo katika miji mingine ya bara, na juhudi za kutengeneza utaratibu kudumu wa usafiri wa umma katika jiji hili ni kama vile unapigwa vita, au umeota matende, au umepatwa na kigugumizi. Alimradi, tunaweza kusema, mradi huo hauendi ilivyotarajiwa na badala yake umekuwa ni chanzo cha kero wa watumiaji wa barabara wa kila aina.    

Huwa nasema kwamba faida mojawapo ya kusafiri ughaibuni ni kujifunza kutokana na jamii nyingine zinavyofanya mambo yake na kuiga kutokana na mambo anayoyaona msafiri. Hili ndilo fundisho kubwa tunalolipata katika simulizi ya “Kusadikika” ya Shaaban Robert , ambaye (nakumbushia tena, wasanii wamejikusanya mwaka juzi wakapanga kupeana nishani za miaka50 (ya kitu gani, hata wao hawakujua), lakini yeye wakamsahau) alitufundisha kile ambacho Wazulu wa Afriki Kusini hukisema:  Ukuhamb’ukubona; kutembea ni kuona.

Sisi tunatembea lakini hatuoni, kama vile tunakwenda “shopping,’ ambayo isingekuwa  mbaya sana kama ingejumuisha pia na “kununua’ maarifa ya wenzetu ili tuyatumie na sisi kujiendeleza. Hapana, “shopping” yetu sisi ilikuwa zamani ni “sistemu” za muziki na video; hii leo ni vitasa vya milango, bawaba na taili za sakafu

Zipo nchi zilizoendelea kiasi kwamba ni kwao ndiko tunapata vifaa kama hivyo. Lakini tukiangalia kidogo tu historia tunatambua mara moja kwamba nchi hizi zimetuacha katika miongo mitatu iliyopita, kwani mnamo miaka ya 1960 tulikuwa sambamba nazo: Malaysia, Indonesia, Thailand na nyingine nyingi.

Hatuna budi kujiuliza ni kwa nini nchi hizi ambazo zilifanana na sisi si miaka mingi iliyopita leo zinatuzidi katika maendeleo, tena kwa mbali. Bila shaka yapo mambo wanayoyafanya na sisi hatufanyi Tujiulize ni nini hicho ambazo nchi nyingine zimeendelea kutoka hali zilizokuwamo pamoja na sisi na leo tunazishangaa, tukiwa tumebaki pale pale na wakati mwingine tukiwa tunarudi nyuma.

Zitakuwapo sababu nyingi mno za kujaribu kuelezea hali hii, lakini bila shaka mojawapo ni kwamba hatujajenga saikolojia ya kudumu hapa tulipo, na ishara moja ni kwamba utashi wa kujenga makazi ya kudumu. Tunajenga vibanda vyetu vya zamani, hata kama tunavijenga kwa matofali ya “blok.”  Bado tuko kwenye misonge na tembe, hatujafikia hatua ya kusimamisha majengo ya kudumu, majengo ya aushi, ya mawe na chuma, yatakayodumu miaka mia tano hadi elfu.

Katika ujenzi tunaofanya leo hii ni wa mpito, kama nilivyosema mara kadhaa. Lakini katika kufanya ujenzi huo tunasafiri kwenda kupata vifaa vya ujenzi kutoka nchi zilizokwisha kujenga majengo ya kudumu, lakini hatuoni uhusiano uliopo baina ya sisi kwenda kufuata vifaa vya ujenzi wa majengo ya muda na uwezo mkubwa wa viwanda vyao wa kuzalisha vifaa tunavyohitaji kwa vijumba vyetu hafifu.

Tunakwenda Uchina, tunakwenda Hispania, tunakwenda Italia. Huko tunanunua vigae vya sakafu, madirisha, milango,    vyote hafifu tukivilinganisha na vifaa vinavyopatikana hapa nyumbani na ambavyovingefaa zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya kudumu.

source: Raia Mwema:  Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment