KWAKO Komredi Profesa Issa Shivji, Shikamoo! Ni matumaini yangu u mzima
wa siha njema na unaendelea vyema na harakati za kutuamsha wanyonge
tuliolala usingizi fofofo wakati rasilimali na utajiri wetu ukipokwa na
mabeberu mamboleo kwa kushirikiana na ‘’makuwadi wa soko huria’’ kama
alivyowaita swahiba wako mpendwa marehemu Profesa Chachage (Mungu ailaze
roho yake ya kizalendo mahala pema peponi).
Pia nichukue fursa hii kukupongeza kwa jinsi unavyoitumia kalamu na
taaluma yako kutukomboa kifikra sisi ‘’wasakatonge’’ tulio kwenye giza
totoro. Naamini bado unazikumbuka nasaha za Mwalimu Julius Nyerere
alivyowaasa wasomi kwenye kongamano la wanazuoni (Juni 27, 1966), Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam kwamba jukumu kuu la mwanazuoni wa Chuo Kikuu
ni kuutafuta ukweli; kuuzungumza kadiri anavyouona na kuusimamia kwa
uthabiti bila kujali gharama yake. Je, na wewe upo tayari kuuzungumza
na kuusimamia ukweli mpaka mwisho wa dahari?
Kwa hakika nafahamu kwamba kuusimamia ukweli kuna gharama kubwa.
Lakini, kama inavyofahamika tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa, hakuna
jipya linaloweza kumwandama mzalendo yeyote ambalo wasemakweli wengine
duniani hawajalipitia. Wanatheolojia wanatujuza kwamba hakuna jipya
chini ya jua kwa sababu yaliyokuwapo ndiyo yatakayokuwapo; na
yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka.
Tangu dunia ya kale historia imetufunza kwamba ipo gharama ambayo
kila msemakweli duniani anapaswa kuwa tayari kuilipa kwa kujiingiza
kwenye jukumu la kuwa sauti ya wanyonge wasio na sauti.
Ni hatari gani inayoweza kumkabili msemakweli hapa duniani kushinda
dhoruba ya mlipuko garini iliyotupokonya kipenzi chetu Profesa Walter
Rodney na unyama wa maharamia wa Kenya waliomuangamiza Komredi Tom
Mboya kwa sababu ya uchu wa madaraka?
Au kuna shubiri chungu namna gani anayoweza kuinywa mwanazuoni
mzalendo kupita uchungu wa korokoroni aliyoipitia Ngugi wa Thiong’o na
masaibu yaliyomuandama mwana-umajumui wa Afrika Kwame Nkurumah?
Nieleze alipo mwana wa Afrika anayeweza kutoa ushuhuda wa ukatili kwa
wazalendo wa Afrika kuliko unyama aliofanyiwa Patrice Lumumba wa Kongo
na mamluki Mobutu Sese Seko na Bwana zake wa ng’ambo kwa sababu tu
Lumumba, chambilecho Rais Eisenhower wa Marekani, alikuwa Fidel Castro
wa Afrika aliyestahili kung’olewa madarakani?
Nakuuliza profesa! Ni vioja gani vinaweza kumsibu mwanazuoni kushinda
vitimbi vya Rais Mobutu Sese Seko kwa Profesa Wamba Dia Wamba na vile
vya Rais Milton Obote kwa Profesa Nabudara Wadada? Ni wapi ulipo msiba
utakaotutoa chozi la uchungu kuliko ule wa Steve Biko aliyepokonywa
uhai kikatili na makaburu?
Nijibu komredi! Kuna changamoto gani vijana wa leo tunaweza kuzipata
kuliko zile mlizopitia zama za harakati zenu za ujanani kupitia chama
chenu cha kiharakati cha University Students African Revolutionary Front (USARF)
wewe na wenzio kina Profesa Karim Hirji, Henry Mapolu na Liundi pale
Chuo Kikuu Mlimani?Niwie radhi;nilitaka kuwasahau kina Yoweri Kaguta
Museveni, Zakia Meghi na Omari Mapuri! Kwa kweli siwezi kuimaliza
orodha yenu.
Wakati unastaafu uhadhiri mwaka 2006, ulitueleza kinagaubaga kwamba
katika kipindi chote cha maisha yako, unajivunia sana kipindi hiki cha
harakati za ujanani. Lakini, kama ulivyofafanua, makomredi wengi wa
miaka ile mkiwa makinda wa Chuo Kikuu ambao sasa ni wakuu wa nchi,
wanasiasa nguli na maulamaa wabobezi wa fani mbalimbali, hivi sasa
wanauonea soni ukweli kwamba na wao walikuwa wanaharakati wakubwa wa
ujamaa enzi za ujanani kwa vile sasa wameipokea dini mpya; dini ya
ubeberu inayowashushia pepo, neema na ukwasi hapa hapa duniani!
Tunafurahi kuona umechagua kuwa upande wa wanyonge. Hivi karibuni
umewahi kutufunda kuhusu thamani ya kalamu ya mwanazuoni (Rejea kitabu
chako cha Insha za Mapambano ya Wanyonge). Ulisema
bila kumung’unya maneno kwamba silaha pekee ya mwanazuoni ni kalamu
yake na kwamba ni lazima mwanazuoni aitumie kalamu yake kwa uthabiti
kila anapopata nafasi kuwasemea wanyonge wasio na sauti hususani
wakulima na wafugaji. (Naomba unipe ruksa niongeze ‘’na machinga wa Tandika, Ubungo na kwingineko Tanzaniawanaofurushwa na wanamgambo bila ya kuelekezwa pa kwenda!”)
Binafsi sina maneno toshelezi kuipambanua thamani ya kalamu ya
mwanazuoni wa wanyonge zaidi ya sifa zilizotolewa na ndugu Kajubi
Mukajanga kwenye Shairi lake la ‘’You write’’ (Rejea kitabu cha ‘’Summons: Poems from Tanzania’’ )
Inanilazimu kuzitafsiri beti za ndugu Kajubi kwa Kiswahili kwa
sababu nakala ya barua kwako nimeisambaza pia kwa umma wa wanyonge wa
uswahilini na vijijini: wanyonge ambao mfumo wetu shelabela wa elimu
umewafanya wengi wao kuwa wahitimu wa shule za kata wasioweza
kuunganisha hata sentesi tatu za kizungu kwa ufasaha! Ndugu Kajubi
anamsifia msomi wa wanyonge kwa maneno yafuatayo;
You weep with them
Unalia pamoja nao (wanyonge)
You sigh with them
Unahema nao (wanyonge) You suffer with them Unataabika nao(wanyonge) But you lift high Lakini unainua juu The banner of their struggle
Bendera ya harakati yao
With your sacred pen Kwa peni yako takatifu!
Naam, hayo siyo maneno yangu. Hayo ni maneno ya Kajubi kuhusu msomi
wa wanyonge. Wanyonge wakiteseka, na yeye anahisi kuteseka; wakihema na
yeye anatweta; wakilia na yeye anabubujikwa machozi ya uchungu! Ndiyo,
ni kupitia kalamu yake iliyotukuka , bendera ya harakati za wanyonge
inainuliwa juu zaidi na kupepea kudhihirisha ushindi wa umma wa
walalahoi.
Kwa hakika beti hizi za Kajubi zinawahusu waandishi sampuli ya
Komredi Abdilatif Abdallah. Si unakumbuka huyu bwana alipowekwa
gerezani na Mzee Jomo Kenyata kwa kuhoji Kenya inakokwenda? Je,
alitokwa na machozi kwa kadhia na misukosuko ya kuswekwa korokoroni?
Upweke wa gerezani ulimkatisha tamaa? La hasha, si unakumbuka
alivyoendelea kuandika kazi zake za kiukombozi akiwa jela kwa kutumia
karatasi za chooni (toilet paper)?
Sasa turudi kwenye kiini cha barua yangu. Ili kuelewa vyema usuli
wake, inanipasa nirejee nyuma kidogo. Nikiwa sekondari, nilipata bahati
ya kusoma na kusimuliwa habari kuhusu weledi wa baadhi ya wahadhiri wa
UDSM. Na kwa kweli baada ya kuja chuoni, nimejionea wana-akademia
waliobobea kwenye fani mbalimbali.
Wakati ule wa sekondari nilivutiwa sana niliposimuliwa habari ya
Profesa Haroub Othman na wewe. Kwa kweli nilipata mshawasha mkubwa wa
kukutana nanyi na kupata darasa maridhawa kutoka kwenu.
Kwa bahati mbaya, mauti yalitupokonya kipenzi chetu Profesa Haroub
Othman hata kabla sijamuona. Mauti hayakutaka nipate walau nafasi ya
kumtunukia kwa kupigania bila kuchoka mustakabali wa haki za binadamu,
hasa upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wanyonge wasio na
uwezo huko Zanzibar. Hebu haya tumuachie Rabana kwa sababu imeshanenwa
kwamba kazi yake haina makosa.
Hata wewe nilikuta umekwishastaafu shughuli ya uhadhiri. Sikubahatika
kukaa darasani ambamo mbele yake kuna mhadhiri aliyeitwa Prof. Issa
Gulamhusein Shivji!
Mwishowe niliamua kujifariji kwa kufuata nyayo zako kila mahali.
Nilinunua vitabu vyako na kuhudhuria makongamano mengi uliyohutubu.
Nisingekosa mhadhara wako kirahisi, labda niwe hoi bin taabani
kitandani! Swahibu zangu wanajua jinsi nilivyomkereketwawa kazi zako.
Hivyo basi mimi ni mwanafunzi wako wa nje ya darasa. Kama
unavyofahamu, ulimwengu wa wanafunzi umejaa maswali: maswali yenye
kufikirisha na wakati mwingine maswali yasiyo na kichwa wala miguu!
Wanafunzi wasipodadisi na kuuliza maswali basi hapo hakuna uanafunzi
(bila shaka kuna ububusa au labda wanafunzi wamekuelewa kwa asilimia mia!)
Si unakumbuka wanafunzi wa Yesu walivyomsonga Masihi kwa maswali na
jinsi Masahaba walivyomuandama Mtume Muhamad (S.A.W) kwa maswali ya
kufikirisha? Hata wewe mwenyewe umerudia mara chungu tele kwamba
tofauti ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu na wale wa chini yake ni kwamba
mwanachuo anapaswa kujipambanua kwa kufanya tafiti, uchambuzi na
tafakuri ya kina kwenye masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Nami mwanafunzi wako nina maswali. Barua yangu imejaa maswali ambayo
ningekuuliza darasani kama ningepata bahati ya kufundishwa nawe. Na
kama asemavyo Okot P’ Bitek (Rejea shairi lake la ‘’From the Mouth of Which River?), maswali yanapokosa wa kuyajibu, yanaumiza kichwa na kuchoma ndani kwa ndani zaidi ya kichomi!
Sasa ngoja nianze maswali yangu.
Wakati fulani nilikuwa wilayani kwetu Tunduru, himaya ya Chifu
Machemba. Si unakumbuka jinsi huyu Bwana alivyowakoromea Wajerumani
walipomtaka kusalimisha himaya yake kwao wakati ule wa kinyang'anyiro
cha mabeberu kuigombea Afrika? Nayakumbuka majibu yake kwa Gavana wa
Kijerumani mwaka 1890, ''Nimeyasikiliza maneno yako lakini sioni sababu
ya kukunyenyekea. Bora nife kwa sababu mimi ni sultani hapa kwenye
nchi yangu nawe ni Sultani kwenye nchi yako..kama una nguvu njoo
mwenyewe unikamate''.
Naam, hayo yalikuwa maneno ya Chifu Machemba ambaye wajerumani
walipomvamia alipambana nao mpaka tone la mwisho na kuamua kutimkia
Msumbiji pale maji yalipozidi unga!
Angekuwa mbinafsi, Chifu Machemba angeweza kuingiwa na uchu na kuiuza
himaya yake kwa Wajerumani lakini akachagua maisha ya upweke ya
uhamishoni. Mbona watawala wengi wa Afrika ya leo hawalikumbuki darasa
hili maridhawa kutoka kwa Machemba? Kwa nini washirikiane na mababeru
kutorosha vito , nyara za serikali na utajiri wetu kwenda ng’ambo?
Basi nikiwa na vijana wenzangu pale Tunduru , niliwasisitizia umuhimu
wa kuwa na msimamo kama ule wa Chifu Machemba. Kwamba kama wanauchukia
ufukara basi wakati wa uchaguzi, wasikubali kurubuniwa.
Lilipokuja suala la msimamo, nikakikumbuka kile kisa cha wewe
kuukataa mwaliko uliopewa na Prof.Keneth King wa Uskochi na
Prof.Bonaventura De Souza wa Ureno waliokualika kutoa mada kwenye
makongamano huko kwao katika kipindi kile ambacho Marekani na washirika
wao waliivamia kimabavu Irak. Uliwaeleza kinagaubaga bila kumung’unya
maneno kwamba unafanya hivyo ili kuonesha mwitiko wako hasi dhidi ya
uvamizi wa Marekani na washirika wake nchini Irak.
Nakumbuka ulivyotueleza wazi wakati ule kwamba ile haikuwa vita dhidi
ya silaha za maangamizi kama walivyodai mabingwa wa propaganda za
kivita, bali ilikuwa vita ya kugombea mafuta na kujitanua kimabavu kwa
mabeberu. Nakumbuka moto uliwaka hadi ndani ya Umoja wa Wahadhiri wa
Chuo Kikuu Cha Dar es laam (UDASA). Nasikia kipindi kile mulifikia hadi
hatua ya kumpiga marufuku barozi wa Marekani Bwana Robert Royall
kukanyaga Chuoni!
Sasa turudi kwenye kiini cha barua yangu. Kama nilivyokueleza kwenye
barua yangu ya kwanza niliyokutumia wikijana, waraka wangu ni mjumuiko
wa maswali kuhusu taifa letu. Maswali haya yananisumbua sana na
kunichoma ndani kwa ndani kwa kukosa majibu. Nimekuwa nikijiuliza
maswali haya kila wakati: najiuliza asubuhi, mchana na usiku!
Jinamizi la maswali haya linanisonga kila sehemu. kafeteria nikipata
staftahi, ladha ya chakula siipati. Darasani, barabarani, chumbani na
kila sehemu nayawaza maswali haya bila kupata majibu. Sasa naomba
nianze maswali yangu na ni matumaini yangu kwamba utanipatia majawabu
ili kukata kiu yangu.
Swali langu la kwanza linahusu itikadi ya ujamaa na kujitegemea.
kwa miaka nenda rudi, Profesa unahubiri kuhusu Azimio la Arusha.
Ingekuwa kwenye muktadha wa ulimwengu wa kiroho ningekuita nabii wa
Azimio la Arusha! Ni adimu kwa wewe kuwa hatibu eneo fulani bila
kulitaja Azimio la Arusha.
Kwenye Tamasha la pili la kigoda cha Mwalimu Nyerere mwaka 2010
ulikwenda mbali zaidi. Ulichapisha mamia ya nakala za Azimio la Arusha
na kutugawia vijana ili tuidurusu misingi yake.
Kwenye kuta za ukumbi wa Nkrumah pale Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
pakawekwa maneno yenye kutia mshawasha ya Azimio la Arusha; ‘’Tumeonewa
kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi
cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na
kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge (wetu)
ili tusionewe na kunyonywa tena.’’
Swali langu kwako ni kutaka kufahamu kiini cha wewe kuendelea
kulishabikia na kulishadidia Azimio katika zama hizi. Kwa nini
unalitajataja Azimio kwenye zama hizi za utandawazi wa ‘’dunia kuwa
kijiji’’? Umesahau kauli ya Mwalimu Nyerere mbele ya wanahabari kwamba
inahitaji roho ngumu mithili ya ile ya mwendewazimu kulizungumzia
Azimio katika zama za leo? Na wewe umeamua kuivaa roho hiyo Profesa
wangu?
Si bado unakumbuka maneno ya Mzee Ruksa wakati akiling’oa Azimio la
Arusha na kusimika kile walichokubaliana kule Zanzibar kwamba ‘’Likulli Ajalin Kitabun, kila kitabu na zama zake’’?
Hata majuzi wakati tunamuaga nguli wa stadi za maendeleo Profesa
Goran Hyden pale hoteli ya Serena, kuna vijana walizipinga fikra za
usasa za uliberali mamboleo na kukumbushia misingi ya Azimio la Arusha;
misingi ya utu na usawa. Nakumbuka Baroli Mwapachu aliwang’akia vijana
wale kwamba wasiendelee na fikra za Ki-maksi zisizotekelezeka katika
dunia ya leo na aliwaasa wahadhiri wa UDSM waachane na mtindo wa
upandikizaji wa fikra hizo kwa wanafunzi: fikra alizoziita muflisi na
zilizofeli!
Nini lengo lako kulishadidia Azimio la Arusha wakati wanazuoni wa
kimamboleo wanaweka wazi kwamba kwenye dunia ya leo ya utandawazi,
kuacha milango wazi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji ni suala lisilo na
mbadala? Na nadhani unazisikia tambo zao kwamba nchi yetu sasa inatajwa
kuwemo kwenye orodha ya mataifa ya Afrika yaliyopiga hatua katika
kuweka mazingira murua ya kuvutia wawekezaji kutoka nje!
Ukitoa mada kwenye kongamano lililoandaliwa na umoja wa Sauti ya
Vijana Tanzania (SAVITA) mwaka 2011, ulitupatia changamoto ya kupambana
kuirejesha misingi ya Azimio la Arusha na kuisimika kwenye katiba
mpya. Hata Dk. Mkenda (Sasa mwenyekiti wa Bodi ya Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii) alitoa rai ya kuirejesha misingi muhimu ya Azimio la Arusha
wakati akitoa mada kwenye kongamano kuhusu fikra za Mwalimu Nyerere
lililofanyika nchini Urusi mwaka 2010.
Pia nimesoma kwenye kitabu chako cha ‘’Insha za Mapambano ya Wanyonge’’
ukibashiri kuhusu kumea kwa dalili zinazoashiria kurejea kwa misingi
mikuu ya Azimio la Arusha na kwamba dalili za wazi za ‘’ufufuo’’ wa
misingi ya Azimio la Arusha zimeanza kuonekana. Nakumbuka ulisisitiza
kwamba si Azimio lote litarudi bali misingi yake mikuu. Nami naomba
nikueleze mapema kwamba kila nitapozungumzia kuhuishwa kwa Azimio
kwenye waraka huu, namaanisha kuhuishwa kwa misingi yake mikuu na si
Azimio lote.
Unamaanisha nini kuhusu kuhuishwa kwa Azimio? Kwamba viongozi wetu
hawatomiliki tena hisa kwenye kampuni za kibwanyenye? wasipokee
mishahara miwili au zaidi? wasiwe wajumbe wa bodi za mashirika na
makampuni ya kibeberu? Unamaanisha tutarudisha tena vijiji vya ujamaa
na kutaifisha makampuni? Unamaanisha nini unaposema Azimio linarudi?
Au unamaanisha tutarudi nyuma na kuikumbatia misingi ya kujitegemea
iliyosisitiza kuacha kutembeza bakuli la kuomba misaada kutoka kwa
wahisani? Unadhani tutazinduka toka usingizini na kuyakumbuka mahubiri
yaliyotuonya kwamba misaada ya wahisani inahatarisha uhuru wetu? Nijuze
Profesa wangu! Unamaanisha nini kuhusu ufufuo wa Azimio?
Najua hata kama Azimio litarudi, halitowakataza tena viongozi wetu
wafanyabiashara kufanya biashara na kupangisha nyumba. Na sasa
tunaambiwa wana majumba na ‘’miradi’’ mpaka Arabuni na Ulaya. Nina
uhakika Azimio jipya litaporudi halitoweka sharti hilo litalowakosesha
raha viongozi wetu watukufu! Si unakumbuka hata mzee Kingunge
alikueleza kwamba kwa hili la kuwanyima viongozi wetu kufanya biashara
ya kupangisha nyumba wakati ule wa Azimio, ilikuwa ni upotofu? (Rejea
mazungumzo yako na Mzee Ngombale Mwilu kwenye jarida la Chemichem toleo la pili)
Halafu kama Azimio linarudi; ni nani analirudisha? Mmetufundisha
kwamba ujamaa wa kiafrika, tofauti na ule wa kisayansi wa Karl Marx na
Fredrick Engels, uliletwa na viongozi waliopigania uhuru na si vuguvugu
la kimapinduzi la wafanyakazi na wakulima. Uliletwa na kina Nyerere,
Nkurumah na Tom mboya.
Ni viongozi gani wataolirudisha Azimio hivi leo? Ni viongozi hawahawa
wanaopokea posho mbili bungeni kwa kazi ileile? Ni viongozi hawahawa
wanaopayuka majukwaani na kulalama kulaani matumizi mabaya ya serikali
wakati wao wenyewe wakiendesha magari ya kifahari ya serikali na kula
mlungula bila soni?
Kwamba viongozi hawa hawa wanaodaiwa kuficha maburungutu ya ndarama
chafu huko Uswizi na kwingineko wataridhia kupitisha sheria yenye hata
harufu tu ya Azimio la Arusha ; Sheria ya kuwabana wasijilimbikizie
ukwasi wakati masikini wa kijijini kwetu Namasakata na kwingineko
Tanzania wakitaabika kwa ufukara?
Unakumbuka yaliyokukuta miaka ya tisini ulipoteuliwa kuwa mwenyekiti
wa tume ya ardhi? Mimi nakumbuka kilichotekea. Ulizunguka nchi nzima
kukusanya maoni ya wananchi na mwishowe ukaishauri serikali kwamba
udhibiti wa ardhi ( Radical Title) urudishwe kwa umma badala ya
rais kama ilivyo sasa. Ulizawadiwa nini kwa ushauri wako? Nini ulipata
zaidi ya maneno ya wakubwa pale wizara ya ardhi kwamba ''Prof. Shivji was so much against the Excutive, and that he tailored the Report towards this end'', yaani
kwamba wewe ulikuwa mpinzani wa serikali na hivyo basi ukaisuka ripoti
ili kupata hitimisho la kuipinga serikali (kwa kushauri udhibiti wa
ardhi uhamishwe kutoka mikononi mwa rais!)
Una imani watu hawa sasa wamepata ubatizo mpya; ubatizo utaowapa
hamu ya kulirudisha Azimio la Ujamaa? Kwamba watazirudisha zile zama za
''Tanzania ni ya wafanyakazi na wakulima'' badala ya kuziendeleza zama
za ''Tanzania ina wenyewe, na wenyewe ndio wao''?
Yu wapi Nyerere wetu; Moringe wetu; na Kawawa wetu wa kulifufua
Azimio la Arusha? Nionyeshe alipo Nkurumah wetu, Sengor wetu, Kaunda
wetu na Tom Mboya wa kuujenga ujamaa? Anaishi wapi Abdulrahman Babu
wetu wa sasa wa kuwakusanya makomredi wenzie na kuwahubiria ujenzi wa
usoshalisti kule Zanzibar na Tanzania kwa ujumla?
Nieleze Profesa! Nijibu komredi uitibu kiu yangu!
Lakini kabla hatujaendelea na waraka wetu, naomba uniruhusu
nikusimulie mchapo mmoja. Si unajua tena vijana tumejaa michapo! Na kwa
kweli ujana bila michapo basi unapoteza maana yake!
Kwa muda mrefu, nimekuwa nikijishughulisha kudodosa kuhusu maisha
yenu ya ujanani. Ni katika safari hiyo ya kudodosa, nikapata bahati ya
kupitia simulizi za Profesa Karim Hirji (Sasa Profesa wa Biostatistics
Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili). Kwa kweli nilihamasika sana. Mzee
Hirji ametusimulia kinagaubaga kuhusu vuguvugu lenu la miaka ya 1970.
Kwamba mlishiriki kilimo na wakulima katika vijiji vya ujamaa na
kuzunguka mashuleni kuwahamasisha vijana kuhusu ujamaa na kujitegemea
ni habari ya kusisimua kwelikweli!
Nasikia mlijitolea kufundisha vituo vya elimu kwa watu wazima. Siku
hizi, licha ya utitiri wa vyuo vikuu, shule za kata hazina walimu.
Vijana hatuna tena moyo wa kujitolea kama wa enzi zenu. Rafiki yangu
mmoja alinieleza kuwa hawezi kujitolea wakati serikali haionyeshi
kujali mustakabali wa shule hizo. Pia anasema uzalendo wenu ulichagizwa
na ukweli kwamba mukiwa vyuoni serikali iliwapa kila kitu.
Nasikia mlisoma bure; kula bure; kulala bure; usafiri bure; kila kitu
bure! Kama hiyo ni kweli basi uzalendo wenu ulichipua kutokana na
samadi ya huduma bora mulizopewa. Au hili halikusaidia chochote?
Kwamba mlikusanya michango kuchangia harakati za FRELIMO kule
Msumbiji na chama cha MPLA cha Angola ni uzalendo wa kusifiwa
kwelikweli. Sio kwamba vijana wa sasa hatuchangii, la hasha! Tunachanga
sana. Siku hizi vijana tunachangia harusi, kitchen party na
kuwalipia wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi ikiwemo marais!
Naambiwa ninyi mlithubutu kutembelea hadi maeneo ya kivita huko
msumbiji yaliyodhibitiwa na FRELIMO ili kujionea matunda ya mapambano
ya wazalendo wa Msumbiji!
Siku hizi vijana tumejibatiza uanaharakati huku mioyo yetu haina hata
tone la harakati ya kuinufaisha jamii. Tunajivika kiremba cha
uanaharakati kwa kuvaa mashati yenye picha za Che Guevara na mavazi ya
kikomredi waliyovaa kina captain Mao Tse Tung! Harakati zetu ni za
kuvaa mavazi yenye picha za Commandante Che Guevara na
Malcom X huku wengi wetu mioyo yetu imejaa kila dalili za ubeberu na
ndoto za kujilimbikizia ukwasi fursa itapowadia!
Hebu tuziache habari hizi kwa muda. Ni matumaini yangu tutapata fursa
ya kuyazungumzia mambo haya kwa kina. Kama unavyofahamu, kama vijana
wa sasa hatutafanya jitihada kuudurusu ujana wa wazee wa leo, kuna
hatari kubwa ya kutumbukia kwenye mtego wa kushindwa kuyafahamu mazuri
yao na kurudia makosa yale yale waliyoyafanya wakiwa vijana.
Naomba tuendeleze mjadala tuliouweka kiporo wiki jana. Kama
unavyokumbuka, wiki iliyopita tulizungumzia kile ambacho wewe ulikiona
kama dalili za wazi za kufufuliwa kwa misingi mikuu ya Azimio la
Arusha. Swali langu kubwa lilikuwa ni kutaka kufahamu jinsi Azimio la
Arusha litavyohuishwa. Ujamaa na kujitegemea ulikuwa mfumo wa ujamaa wa
kiafrika ambao tofauti na ujamaa wa kisayansi wa Karl Marx uliojengwa
kwa vuguvugu la wafanyakazi na wakulima, wenyewe uliletwa na viongozi
wa kizazi cha uhuru. Nilikuuliza wiki jana kama tunao viongozi wa
kisiasa hapa nchini ambao unawatumaini kulirejesha Azimio. Bado
ninasubiri jibu langu kwa shauku.
Au sijakuelewa Profesa? Pengine unamaanisha watu wenyewe
watarirudisha Azimio. Kwamba umma wenyewe wa wanyonge utapigania
kuirejesha misingi ya usawa? Nimesoma pahala ukirejea vuguvugu la
wavujajasho kwenye maeneo ya Hanang, Loriondo, Rufiji na kwingineko
Tanzania kupinga upokwaji wa rasilimali zao bila wao kushirikishwa
ipasavyo (Na sasa Mtwara hali ilikuwa tete kuhusu uvunaji na
usafirishaji wa gesi asilia) unadhani hizi ni dalili za awali za ufufuo
wa Azimio?
Lakini Profesa, si umetufundisha mwenyewe kwamba vuguvugu la
wafanyakazi baada ya uhuru lilianza kuchipua Tanzania tangu miaka ya
sabini? Nimesoma kazi zako kadhaa kuhusu kumea kwa tabaka la
kibwanyenye na kuchomoza kwa vuguvugu la wafanyakazi. Jitihada
zilifanyika wakati ule kuzima vuguvugu la wafanyakazi. Una hakika haya
hayawezi kujirudia sasa? Ninafahamu kwamba bado unayakumbuka mabavu
yaliyotumika kuwadhibiti wamasai wa Loriondo ili kupisha ‘’mwekezaji’’?
Mh.Shamsa Mwangunga alisema waliofurushwa ni wakenya! Kwa Kweli
nilipomsikia nilibaki mdomo wazi!
Lakini hata kama umma utakuwa na mwamko mkubwa na hamasa, tunaweza
kulirejesha Azimio kama wale wanaouhamasisha umma hawana imani na
Azimio?
Sikuulizi kama vuguvugu linalochipua kwa kasi kwenye kambi ya
upinzani nchini ndilo unalolitumaini kurudisha misingi ya Azimio.
Nimepitia maandiko ya vyama kadhaa kwenye maeneo ya itikadi, falsafa na
sera. Makamanda wa ‘’peoples power’’ wameshaweka wazi kwamba wakipewa ridhaa ya kushika dola wanakusudia kujenga mfumo wa uchumi na siasa za mrengo wa kati. Hata ‘’wanangangari’’ wametueleza kwamba wanaamini katika uliberali.
Majuzi nimebahatika kupitia tamko la Mtandao wa Vikundi vya
Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) walilolitoa pale Morogoro wakati wa
kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wetu.
Naomba nikukumbushe waliyoyasema wakulima wale: kwanza waliweka wazi
sikitiko lao kuhusu kusalitiwa kwa misingi ya Azimio la Arusha na hivyo
basi kukuza pengo baina ya walalahoi na walalaheri.
Pia waliweka wazi kwamba wanapinga kwa nguvu zote ukandamizaji na
unyonyaji wanaofanyiwa wakulima wa Tanzania na wakoloni mamboleo kwa
kushirikiana na makuwadi wa ubeberu. Nilihamasika sana niliposoma
kwamba wameamua kuchukua hatua ya kukuza umoja wa wakulima wanaonyonywa
na kukandamizwa.
Lakini, niligutuka kidogo niliposoma suluhisho walilolitoa
kukabiliana na madhila yanayowakumba. Unajua suluhisho walilolisema
katika kunusuru mustakabali wao? Kwamba watawanyima kura wanasiasa
uchwara wote na pia watapiga kelele dhidi ya dhuluma kwa wakulima. Hapa
nilishangaa kidogo! Ninachojiuliza ni kama wakulima hawa wanalenga
kulirudisha Azimio la Arusha au wanachotaka ni maslahi bora katika mfumo
uleule uliopo? Kama wanataka Azimio, watalirudishaje? Katika vyama
vyetu vya siasa, ni nani watayempa kura ambaye ana ndoto na nia thabiti
ya kulirudisha Azimio la Arusha?
Nitanzulie Profesa! Nitoe kizani Komredi!
Source: Raia Mwema
Bravo !lakini kiswahili mheshimiwa kinakupa tabu L na R , mfano Loliondo Sio liriondo nk
ReplyDeleteFikra pevu ulizoonesha ni msingi wa ukombozi wa vijana kama tukitambua nafasi yetu katika kulitengeneza taifa letu la Tanzania.
ReplyDelete