Na Maggid Mjengwa,
WATANZANIA
tulifanya kosa kubwa. Ni pale tuliporuhusu mfumo wa vyama vingi bila
kufanyia marekebisho makubwa Katiba yetu. Maana, katika nchi zetu hizi,
uongozi umekuwa wa awamu.
Kiongozi anaingia madarakani na kukaa kwa miaka mitano mpaka kumi.
Kwa Mwafrika, hapa ina maana ya kuhamia na kuhama kutoka nyumba za
mamlaka. Ndio, tumejikuta tunaingiza wapangaji kwenye nyumba zetu bila
kuwekeana mikataba. Na kama kuna mkataba, basi umeandikwa na mpangaji
mwenyewe. Hapo utategemea nini?
Katiba tunayokwenda kuiandika itusaidie kwenye kuwadhibiti
‘wapangaji’ wetu kwa maana ya viongozi tuliowapa dhamana za uongozi.
Maana, ilivyo sasa, utakumkuta kiongozi anayejigamba hadharani, kuwa
ameukwaa uongozi kwa vile ni swahiba wa fulani. Kwamba ana miaka mitano
au kumi ya ‘ulaji’. Maana, hata jirani zake watasema ‘jamaa kapata
ulaji’. Na magazeti pia yataandika hivyo, kana kwamba uongozi una maana
ya ulaji na si utumishi wa umma.
Na Afrika wapangaji waliongia kwenye nyumba (mamlaka) kwa staili hiyo
huwa wagumu sana kutoka hata pale wenye nyumba wanapoona wakati
umefika wa kuwaondoa. Wameshaonja tamu ya madaraka. Na kama wataondoka,
basi, watataka wao waingize wapangaji wapya wa kulinda maslahi yao.
Hawataki kazi hiyo ifanywe na wenye nyumba kwa maana ya wananchi
wenyewe.
Tatizo ni sisi Waafrika kukosa imani na Waafrika wenzetu tuliowaweka
madarakani. Kikubwa ni kukosekana kwa maadili ya uongozi. Viongozi
wengi Afrika wamekuwa ni watu wenye tamaa ya madaraka na mali.
Usipokuwa na Katiba yenye kuwadhibiti wanapokuwa kwenye uongozi, basi,
nchi wanaigeuza ‘shamba la bibi’.
Kama mbweha, watakula minofu wakifuta damu midomoni. Ndio, watakula
wakilindana. Kwa baadhi yao, miaka mitano au kumi kwenye uongozi ina
maana ya kujilimbikizia mali, kana kwamba nchi nayo inahama baada ya
miaka kumi. Na siku za kuhama madarakani zikikaribia, itaongezeka,
kasi ya kuvuna vilivyobaki kwenye ‘shamba la bibi’
Swali ni je, Waafrika tuweje? Ni swali la kifalsafa. Inahusu virtue, kwa
maana ya maadili na kutenda yalo ya haki. Kutenda yalo mema. Mtu mwenye
maadili mema utamwamini, ndivyo pia wasemavyo Waingereza; a virtuous person
is someone you can trust.
Mzazi anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kisiasa anapaswa kuwa a virtuous person, kiongozi wa kidini anapaswa kuwa a virtuous person, mwandishi wa habari anapaswa kuwa a virtuous person, vivyo hivyo mwalimu.
Kwa hilo la mwisho, uhusiano wa mwalimu na mwanafunzi kati ya
Mwanafalsafa Socrates na mwanafunzi wake Plato usingepata umaarufu
ulionao sasa kama Plato angebaki kuwa ‘mwanafunzi’ tu. Kubaki kuwa
kivuli cha mwalimu wake Socrates. Na Socrates alitambua, kuwa jukumu
la mwalimu ni sawa na la mkunga. Mwalimu ni mkunga.
Katika mijadala ya siku hizi tunaona hata wale wanaojiona ni viongozi
wasivyo
tayari kukosolewa. Wasivyo tayari kuona upungufu wao. Inasikitisha,
kuona
baadhi ya viongozi hawa ni vijana sana. Wamekuwa wabinafsi zaidi huku
wakijiita ni viongozi. Wanajiita viongozi ilhali, kwa namna nyingi,
hawawatendei haki wanaowaongoza, wanatanguliza zaidi tamaa ya mali na
mamlaka.
Yumkini, kiongozi mtenda maovu kwa watu wake ni ama mjinga au
mgonjwa. Kama ataambiwa bayana, kuwa anatenda maovu, au ana udhaifu wa
kiutendaji, basi, huenda tutamsaidia kujirekebisha. Lakini, kamwe
usishangae, kama kiongozi huyo atatingisha mabega na kucheka tu.
Atacheka na kutushangaa siye tunaomkosoa.
Katika machapisho yake ya "Republic", yaani , "Jamhuri", Plato
anazungumzia kwa kina juu ya ubinafsi na maadili. Je, kuna sababu gani
nzuri na za kimsingi za kuwa mtenda haki na si kinyume chake, yaani
mtenda maovu?
Glaucon, ndugu wa Plato anajibu; "binadamu wote kwa asili yetu tu
wabinafsi, tunajijali sisi wenyewe kila tunapopata nafasi ya kufanya
hivyo. Bila kujali kama jambo hilo si la haki kiasi gani kwa wengine.
Lakini, kwa bahati mbaya, nasi pia hufikwa na hali kama hiyo kwa
kufanyiwa yasiyo haki na wengine. Jambo hilo huwa si la kufurahia,"
anasema Glaucon.
Katika jibu la Glaucon, Plato anatafuta namna ya kuikabili hali hiyo.
Na ubinafsi wa viongozi Afrika huchagizwa na ulevi wa madaraka. Walevi
wa madaraka wako dunia nzima. Katika nchi za wenzetu, wao walau wana
njia za kuwadhibiti, kupitia Katiba zao. Lakini, Afrika ni bara lenye
kuongoza kwa kuwa na walevi wengi wa madaraka. Katiba zetu
tulizorithi kutoka kwa wakoloni zinachangia kuongeza idadi ya walevi
hawa wa madaraka. Ulevi wa madaraka Afrika ni sehemu ya jibu la swali;
Kwa nini sisi ni masikini?”
Hivyo basi, ili kuwepo na mazingira ya kuishi kwa amani na usalama ni
vema, kwa mujibu wa mwanafalsafa Plato, kukawepo na taratibu za
kuishi kistaarabu. Ndipo hapa dhana ya kuwapo kwa Mkataba wa Kijamii
(Social Contract) ikaingia akilini kwa mwanadamu. Ndio chimbuko la
Katiba za nchi. Chimbuko la misingi ya utawala bora.
Nasi tuna nafasi sasa ya kuandika Katiba yetu mpya kwa maslahi ya Watanzania wa sasa na hata miaka mia moja ijayo. Inawezekana.
source: Mjengwa Blog
No comments:
Post a Comment