Kiiza baada ya kufunga bao la pili
Kavumbangu wa pili kutoka kushoto, akishangilia bao lake na wenzake
Kavumbangu wa kwanza kushoto
Kavumbangu akimfunga kipa wa Azam, Mwadini Ali
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga iongoze Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 26, ikiwa imebakiza mechi moja ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Caostal Union mjini Tanga, ikifuatiwa na Simba SC yenye pointi 23, ambayo leo imefungwa 2-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kvumbangu aliyeunganisha krosi ya Simon Msuva kutoka wingi ya kulia dakika ya tisa.
Katika kipindi hicho, Yanga timu zote zilicheza kwa kiwango sawa, isipokuwa Yanga ndiyo iliyokuwa na mashambulizi ya kutisha zaidi.
Mabeki wa Yanga walimdhibiti vema mshambuliaji hatari wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’ na kitendo cha kocha Mholanzi, Ernie Brandts kupanga viungo wawili wakabaji, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo viliisaidia timu hiyo kuwabana Azam katikati ya Uwanja.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi vizuri zaidi na kuifunika kabisa Azam, ambayo leo hakika ilimsononesha kocha wake, Muingereza Stewart Hall.
Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 68, akiunganisha krosi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kutoka wingi ya kulia.
Baada ya bao hilo, Kiiza alivua jezi yake na kubaki na fulana ya njano yenye maandishi; Rest In Peace Mafisango, I miss you So much my brother, maana yake akimuenzi aliyekuwa kiungo wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Mei mwaka huu akiwa mchezaji wa klabu hiyo.
Kwa ujumla Yanga imebadilika mno kiuchezaji na sasa wanacheza kwa kuonana, kupeana pasi za uhakika ndefu na fupi, kuwabana wapinzani na pia bila kuchoka muda wa mchezo.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Simon Msuva/Paul Ngalema, Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima na Didier Kavumbangu.
Azam FC; Mwadini Ally, Erasto Nyoni/Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris na Said Mourad, Jabir Aziz/Ibrahim Mwaipopo, Kipre Balou, Khamis Mcha ‘Vialli’/Abdi Kassim ‘Babbi’, Salum Abubakar, John Bocco na Kipre Tcheche.
Katika mchezo wa utangulizi, Yanga B imewafunga Azam B, maarufu kama Azam Academy mabao 2-0. Mabao ya Yanga B yalifungwa na Joseph Banda na Claver Charles kipindi cha kwanza.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar iliichapa mabao 2-0 Simba SC, Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mabao ya Said Mkopo na Hussein Javu.
Simba inabaki na pointi zake 23, baada ya kucheza mechi 12, ikiipisha kileleni Yanga yenye pointi 26 sasa. Simba itamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kumenyana na Toto African uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment